Tafuta

Mwenyeheri Maria Emilia alikuwa na Ibada ya pekee kwa Ekaristi Takatifu na Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Mwenyeheri Maria Emilia alikuwa na Ibada ya pekee kwa Ekaristi Takatifu na Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. 

Mwenyeheri Maria E. Riquelme: Ekaristi Takatifu na B. Maria

Mwenyeheri Riquelme alikazia: Sala na tafakari ya Neno la Mungu, ili kukuza na kudumisha upendo wa dhati kwa Mungu na jirani; upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Alijipatia neema ya kusonga mbele katika utume wake kutoka katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi na ushiriki mkamilifu wa Ibada ya Misa Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 10 Novemba 2019 amemtaja Mtumishi wa Mungu MarÍa Emilia Riquelme wa Zayas, Muasisi wa Shirika la Masista Wamisionari wa Ekaristi Takatifu na Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, aliyetangazwa kuwa Mwenyeheri kwa niaba yake na Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, Jumamosi, tarehe 9 Novemba 2019 huko Granada, nchini Hispania. Katika mahubiri yake Kardinali Giovanni Angelo Becciu, amekazia umuhimu wa Sakramenti ya Ubatizo, inayomwezesha mwamini kuwa ni Hekalu la Roho Mtakatifu, kielelezo cha uwepo wa Mungu katika maisha ya mwamini, ili kuhakikisha kwamba, anajitahidi kuzaa matunda ya matendo mema: kiroho na kimwili, kwa kutekeleza kwa dhati kabisa dhamana na wajibu aliojitwalia kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo inayomshirikisha: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo katika maisha yao.

Kanisa limetambua fadhila za Kikristo zilizopamba maisha ya Mwenyeheri Maria Emilia Riquelme, aliyejisadaka kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya Mungu na jirani, akayageuzia kisogo malimwengu. Imani ikawa ni dira na mwongozo wa maisha yake hadi kifo kilipomtenganisha na dunia. Alikazia maisha ya sala na tafakari ya Neno la Mungu, ili kukuza na kudumisha upendo wa dhati kwa Mungu na jirani; upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Alijipatia neema, nguvu na baraka ya kusonga mbele katika maisha na utume wake kutoka katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na ushiriki mkamilifu wa Ibada ya Misa Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ibada kwa Ekaristi Takatifu na kwa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, ikamsaidia kukuza na kudumisha ari na moyo wa kimisionari ndani mwake, kiasi cha kuanzisha Shirika, ili kusaidia kutoa elimu makini kwa wasichana na hatimaye, kushiriki katika kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo sehemu mbali mbali za dunia.

Mwenyeheri Maria Emilia Riquelme alitamani kuona kwamba, watawa wa Shirika lake, wanajikita katika Sala na Kazi kama ilivyokuwa kwa Maria na Martha, ndugu zake Lazaro. Kwanza walipaswa kusikiliza Neno la Mungu na hatimaye, kulimwilisha katika huduma, ili kuganga na kuponya madonda ya maisha ya watu: kiroho na kimwili. Alikuwa ni shuhuda makini katika ujenzi wa Kanisa, kwa kuwatangazia wale wote waliovunjika na kupondeka moyo, Injili ya matumaini. Alikuwa ni shuhuda na chombo cha Injili ya upendo kwa maskini: kiroho na kimwili, akawa ni mfano bora wa kuigwa kwa watawa wenzake ambao walimwona kuwa kama ni Mama na dada yao mkubwa. Alihakikisha kwamba, watawa wake wanapata malezi na majiundo makini, ili kukubaliana na changamoto za maisha na utume wa kitawa kwa ujasiri, ari na moyo mkuu. Maisha yake yalisimikwa katika fadhila ya unyenyekevu mbele ya Mungu na kwa jirani zake.

Akasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za Shirika lake. Akawa kweli ni kiongozi na mtetezi wa haki, ili kudumisha amani na utulivu kati ya watu wa Mungu. Katika shida na mahangaiko yake ya ndani, daima alikimbilia kupata faraja kutoka katika Fumbo la Msalaba. Aliposhtumiwa kwa uwongo, alijibu kwa sala pamoja na kujiaminisha katika ulinzi na tunza ya Mungu katika maisha yake. Mwenyeheri Maria Emilia Riquelme ni mfano bora wa kuigwa kwa kukita maisha katika tunu msingi za Kiinjili; kwa kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya Injili ya Kristo na huduma kwa maskini; huduma ambayo iliboreshwa kwa namna ya pekee kwa njia ya sala iliyokuwa inamwilishwa katika haki, furaha na matumaini, kama sehemu ya ushuhuda wa Kikristo. Sala na dua za Mwenyeheri Maria Emilia Riquelme zisaidie kuimarisha maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo.

Papa: Mwenyeheri Maria E. R.
11 November 2019, 10:35