Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 4 Novemba 2019 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Makardinali na Maaskofu waliofariki dunia 2018-2019. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 4 Novemba 2019 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Makardinali na Maaskofu waliofariki dunia 2018-2019. 

Kumbukumbu ya Makardinali na Maaskofu Marehemu: Ufufuko wa wafu!

Makardinali na Maaskofu waliotoka katika maisha ya hapa duniani, ili kwenda kukutana na Kristo Mfufuka, wawakumbushe umuhimu wa kutoka katika ubinafsi, ili kufungua mlango unaoelekea kwa Kristo Mfufuka. Viongozi wa Kanisa wawe na ujasiri wa kuomba neema ya kumwendea Kristo Mfufuka kwa njia pamoja na wandani wa safari wanaotembea nao kila kukicha. Hatima ni Ufufuko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican

Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 4 Novemba 2019 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea: Makardinali na Maaskofu waliofariki dunia katika kipindi cha Mwaka 2018-2019 wakiwa na alama ya imani na matumaini ya ufufuko kutoka kwa wafu.  Hawa ni viongozi waliosadaka maisha yao kwa: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Sasa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo amewaita kwenye makao ya uzima wa milele, kwani yote yamekamilika, “Consummatum est”. Fumbo la kifo, liwe ni changamoto kwa ajili ya kutafakari kuhusu maisha na uzima wa milele, kwani mwanadamu amezaliwa si kwa ajili ya kifo, bali aweze kupata maisha na uzima kwenye makao ya mbinguni. Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kilele cha ukweli wa imani katika Kristo aliyeteswa, akafa na hatimaye kufufuka kwa wafu kadiri ya Maandiko Matakatifu.

Ni ufunuo wa Uungu wa Kristo Yesu unaowapatia waamini maisha ya uzima mpya na hivyo kuhesabiwa haki pamoja na kufanywa wana wateule wa Mungu. Ufufuko wa Kristo ni msingi wa ufufuko wa miili na uzima wa milele ijayo. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amejikita zaidi katika maisha ya mwanadamu tangu anapozaliwa kutoka tumboni mwa mama yake kuwa ni safari ya kutoka; umuhimu wa kuonesha huruma kwa wale wanaosinzia katika kifo na kwamba, ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele ndiyo inayopaswa kuwa ni hatima ya maisha ya mwanadamu. Kristo Yesu anawafundisha wanafunzi wake kwamba, watafufuliwa siku ya mwisho. Huu ni mwaliko kwa waamini  kutafakari kuhusu Ufufuko mintarafu wito wa kila mmoja wao. Watu wote wanaitwa na kualikwa kumwendea Kristo Mfufuka, ili kujipatia ngao salama dhidi ya hofu ya kifo na hatima ya maisha yao. Hofu hii inaondolewa kwa kujenga na kudumisha uhusiano wa karibu na Kristo Mfufuka, kwa njia ya majadiliano katika sala; kwa kumpelekea watu wale wote aliowakabidhi kwao kama viongozi wa Kanisa.

Katika maisha yao kama viongozi wa Kanisa, wanapaswa kujiuliza, Je, wameweza kukabiliana na hali pamoja na mazingira yao kwa kushikamana na Kristo katika magumu na furaha ya maisha? Wanapaswa kujiuliza ikiwa kama mchakato mzima wa safari ya maisha yao, ilikuwa ni hija ya kumwendea Kristo Yesu, au wamekuwa wakijitafuta wenyewe na hatimaye, kujizunguka wenyewe? Je, ni watu wanaojitafuta wao wenyewe, ili kujijengea jina na umaarufu; kwa kulinda tu dhamana waliyokabidhiwa na Mama Kanisa, nafasi na muda wao, au wanajitaabisha kumwendea Kristo Mfufuka? Waamini wakumbuke kwamba, kuna hatari ikiwa kama hawatajitaabisha kumwendea Kristo Mfufuka wakajikuta wakiwa wametupwa nje, huku wakilia na kusaga meno. Kwa wale wafuasi wanaojishikamanisha na kuambatana na Kristo Mfufuka watambue kwamba, maisha ya mwanadamu tangu anapozaliwa kutoka tumboni mwa mama yake, kuwa ni safari ya kutoka kuelekea katika maisha ya ujana na hatimaye utu uzima.

Mama Kanisa anaposali na kuwakumbuka Makardinali na Maaskofu waliotoka katika maisha ya hapa duniani, ili kwenda kukutana na Kristo Mfufuka, wawakumbushe umuhimu wa kutoka katika ubinafsi, ili kufungua mlango unaoelekea kwa Kristo Mfufuka. Viongozi wa Kanisa wawe na ujasiri wa kuomba neema ya kumwendea Kristo Mfufuka kwa njia pamoja na wandani wa safari wanaotembea nao kila kukicha, ili kukutana na Kristo Mfufuka, “chemchemi ya maisha mapya”. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwa kusema kwamba, Kitabu cha Pili cha Wamakabayo kinaelezea kwamba, Yuda  kiongozi wa Wayahudi alichangisha fedha akazipeleka Yerusalemu kutoa sadaka ya dhambi. Kwa kufanya hivi alitenda vema na kwa haki kwa kuwa alikuwa na imani, aliukumbuka ufufuo wa wafu na aliona umuhimu wa kuonesha huruma kwa wale wanaosinzia katika kifo (Rej. 2Wak. 12:45). Huruma kwa wengine inafungua malango ya maisha na uzima wa milele kama ilivyo hata katika huduma inayotolewa kwa unyenyekevu kwa maskini ni ufunguo wa maisha na uzima wa milele kwa sababu upendo hauna ukomo!

Upendo ni daraja kati ya mbingu na dunia, changamoto na mwaliko wa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na wahitaji zaidi. Waamini wajifunze kuhuzunika na wale wanaohuzunika; kuwaombea wasio na waombezi na hatimaye, kutoa kwa ukarimu bila kungojea malipo! Huu ni msingi wa Ufufuko na maisha ya uzima wa milele. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele ndiyo inayopaswa kuwa ni hatima ya maisha ya mwanadamu. Kumbe, kila uamuzi unapaswa kufanywa na kutekelezwa kwa kuzingatia hatima ya maisha ya mwanadamu, kwani ufufuko wa wafu ndich kiini na maana ya maisha ya mwanadamu. Mtakatifu Inyasi wa Loyola anawaalika waaamini kutafakari jinsi itakavyokuwa ile Siku ya Hukumu kwa kuzingatia matendo yote waliyotenda wakiwa hapa ulimwenguni, kwani kila mtu atavuna kile alichopanda. Safari ya hapa duniani, iwasaidie waamini kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya Siku ya Hukumu.

Tafakari hii anasema Baba Mtakatifu, iwasaidie kuona ukweli wa mambo kwa kutumia macho ya Kristo Mfufuka; kwa kuangalia ya mbeleni kwa imani na matumaini ili hatimaye, kufanya maamuzi kadiri ya maisha na uzima wa milele; maisha yanayopambwa kwa fadhila ya upendo! Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Makardinali, Maaskofu wakuu pamoja na Maaskofu kwa kuwauliza watu wa Mungu, ikiwa kama wako tayari kutoka katika ubinafsi wao na kuanza safari siku kwa siku ya kumwendea Kristo Mfufuka? Je, ndani mwao wanayo huruma kwa maskini na wahitaji zaidi? Katika utekelezaji wa dhamana na utume wao kwa Kanisa, Je, wanajitahidi kutanguliza mapenzi ya Mungu? Mambo haya yawasaidie kutafakari kuhusu hatima ya maisha na ufufuko wa wafu, ili siku moja waweze kuungana na Kristo Mfufuka na wala asiwepo hata mmoja kati yao, atakayekuwa ameachwa nje ya maisha na uzima wa milele. Wajitahidi kumtafuta na kumwambata Kristo Yesu: Mfufuka na kwa kufanya hivyo, kwa hakika watakuwa wanaanza kuishi mapambazuko ya Ufufuko wa wafu!

Papa: Misa Wafu
04 November 2019, 15:14