Tafuta

Profesa Charles Tayor na Padre Paul Bèrè ndio washindi wa tuzo ya Mfuko wa Joseph Ratzinger-Benedikto XVI kwa Mwaka 2019. Profesa Charles Tayor na Padre Paul Bèrè ndio washindi wa tuzo ya Mfuko wa Joseph Ratzinger-Benedikto XVI kwa Mwaka 2019. 

Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI: Tuzo kwa Mwaka 2019

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Padre Paul Bèrè ni mwafrika wa kwanza kutunukiwa tuzo hii kwa kuwa amejipambanua barabara katika Sayansi ya Maandiko Matakatifu, changamoto na mwaliko kwa wale wote wanaoendelea kujisadaka katika mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho Barani Afrika, kuzama zaidi katika masomo na tafiti zao kama walivyokuwa Mababa wa Kanisa zama hizo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI, ulianzishwa rasmi tarehe 1 Machi 2010 na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Mfuko huu unapania pamoja na mambo mengine: kuibua na kukuza taalimungu ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwa njia ya tafiti makini za kisayansi, mikutano, warsha na makongamano ya kitaifa na kimataifa. Ni mfuko unaosaidia watafiti mbali mbali kuchapisha kazi zao pamoja na kutoa udhamini kwa wanafunzi wanaotaka kujizatiti zaidi katika taalimungu ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, ambaye katika maisha na utume wake wote ameendelea kujipambanua kuwa ni shuhuda wa imani, upendo na matumaini thabiti ya Kanisa Katoliki. Haya ni mambo yanayobubujika kutoka katika nyaraka zake za kitume. Kila mwaka, Mfuko huu unatoa tuzo kwa washindi katika nyanja mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa. Watafiti wanawasaidia watu kuzama na hatimaye, kufahamu utajiri na amana inayofumbatwa katika mawazo ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, katika uhalisia wa maisha ya watu.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 9 Novemba 2019 amewapongeza na kuwatunuku Profesa Charles Tayor pamoja na Padre Paul Bèrè washindi wa Tuzo ya Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI kwa mwaka 2019. Baba Mtakatifu amempongeza kwa namna ya pekee kabisa Papa Mstaafu Benedikto XVI kwa mafundisho yake makini; kwa kuwa mfano bora wa kuigwa katika huduma ya Kanisa mambo yanayoshuhudia kwamba, kwa hakika ni mtu mwenye mawazo mazito, anayependa kusoma; kusikiliza, kujadiliana na watu, lakini zaidi kusali. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwamba, imani ya Kanisa itaendelea kupyaishwa kwa kusoma alama za nyakati, ili hata katika mabadiliko ya nyakati, waamini wawe na jeuri ya kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Dhamana hii inaweza kutekelezwa kwa dhati kwa njia ya majadiliano, daima wakitafuta njia ya kweli ya kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu katika maisha ya nyakati hizi. Haya ndiyo matamanio makubwa ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI; mwanataalimungu mahiri na mchungaji wa kweli; aliyejisadaka katika maisha yake, ili kuwafundisha waamini kutafuta na kuambata ukweli pale ambapo imani na uwezo wa mwanadamu wa kufikiri; akili pamoja na tasaufi vinakumbatiana na kushibana kwa dhati kabisa. Masomo mbali mbali yanapaswa kumsaidia mwanadamu kukua, kukomaa na hatimaye, kufikia utimilifu wa maisha yake, kwa kukutana na Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, ufunuo wa Mungu ambaye ni upendo. Ni dhamana na wajibu wa taalimungu kuendeleza majadiliano na tamaduni mintarafu mabadiliko ya nyakati na wakati huo huo, Kanisa halina budi kujielekeza katika mchakato wa kupyaisha imani kama sehemu ya utume wake wa kuinjilisha.

Ni katika muktadha huu, washindi wa Tuzo ya Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI kwa mwaka 2019 wametoa mchango mkubwa unaogusa nyanja mbali mbali za maisha ya watu. Profesa Charles Tayor katika maisha na utume wake amepembua changamoto  zinazowakabili Wakristo na kwa namna ya pekee Wakatoliki bila kuwasahau na wale wote wanao mwamini Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro alidhamiria kumtangaza na kumshuhudia Mwenyezi Mungu aliyejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, ili aweze kupokelewa na kukubaliwa na wengi. Tatizo la waamini kumezwa na malimwengu limepembuliwa kwa kina na mapana mintarafu tamaduni za watu wa Magharibi, mikondo ya mawazo na fikra za watu mbali mbali; kwa kutambua upya katika mahusiano na mafungamano yao; mwanga na vivuli vinavyopaswa kufahamika. Yote haya yameliwezesha Kanisa kufahamu mambo msingi yanayowayumbisha watu katika maisha yao ya kiroho.

Huu ni mwaliko wa kukazia tunu msingi za maisha ya kiroho; kwa kujikita katika majadiliano na tamaduni mbali mbali, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda kama njia muafaka ya kutangaza imani kwa watu wa nyakati hizi. Padre Paul Bèrè ni mwafrika wa kwanza kutunukiwa tuzo hii kwa kuwa amejipambanua barabara katika Sayansi ya Maandiko Matakatifu, changamoto na mwaliko kwa wale wote wanaoendelea kujisadaka katika mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho Barani Afrika, kuzama zaidi katika masomo na tafiti zao kama walivyokuwa Mababa wa Kanisa kama vile Tertulian, Cyprian na Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa. Kuibuka na kuenea kwa dini ya Kiislam na baadaye ukoloni mkongwe ukazamia Barani Afrika, kulikwamisha mchakato wa utamadunisho wa Injili hadi kufikia nusu ya karne ya ishirini.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, taalimungu ya nyakati hizi kutoka Barani Afrika bado ni changa sana na inaendelea kuzaa matunda katika tamaduni nyingi za Kiafrika. Padre Paul Bèrè katika maisha na utume wake, ameendelea kujipambanua ili kuhakikisha kwamba Sinodi ya Afrika ambayo alishiriki kikamilifu, inafahamika na kupokelewa kwa mikono miwili mintarafu mazingira ya Bara la Afrika. Padre Paul Bèrè amesaidia kufasiri Agano la Kale mintarafu fasihi simulizi na hii ndiyo maana ya uinjilishaji unaopania kuleta upyaisho katika maisha ya watu na kama njia ya kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni ili kukidhi vionjo vya watu wakati wa furaha, machungu na matumaini. Washindi wa Tuzo ya Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI kwa mwaka 2019 ni watu wanaotoka katika Mabara mawili tofauti, lakini wanaonesha kwamba, mchakato wa utamadunisho unaweza kuwasaidia watu kukutana na Mwenyezi ambaye amejifunua kwa njia ya Kristo Yesu. Huu ndio utume na dhamana ya Mfuko wa Joseph Ratzinger, Benedikto XVI, ili wasomi wasaidie kuwa ni vyombo vya ukweli. Hii ndiyo changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na wote!

Papa: Mfuko Ratzinger
09 November 2019, 15:17