Tafuta

Papa Francisko tarehe 4 Novemba 2019 anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Makardinali na Maaskofu waliofariki dunia kati ya mwaka 2018-2019 Papa Francisko tarehe 4 Novemba 2019 anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Makardinali na Maaskofu waliofariki dunia kati ya mwaka 2018-2019 

Kumbu kumbu ya Waamini Marehemu: Kifo, imani na matumaini!

Tarehe 2 Novemba, ni Kumbu kumbu ya Waamini Marehemu wote! Fumbo la kifo ni changamoto kwa ajili ya tafakari, kukesha na kutekeleza nyajibu mbali mbali kwa uaminifu na ukamilifu kwa kutambua kwamba, wameteuliwa ili kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Fumbo la kifo ni fursa ya kufakari kwa kina na mapana maana ya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini kwamba, tarehe 2 Novemba, kila mwaka ni siku maalum iliyotolewa na Mama Kanisa kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliotangulia mbele ya haki wakiwa na alama ya imani sasa wanapumzika kwenye usingizi wa amani wakiwa na tumaini la maisha na uzima wa milele. Baba Mtakatifu Jumamosi jioni, tarehe 2 Novemba 2019 anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Waamini Marehemu wote kwenye “Makatakombe ya Priscilla” moja ya Makaburi yaliyotumiwa na Wakristo wa mwanzo mjini Roma. Baba Mtakatifu ameonya kuhusu tabia ya baadhi ya watu kufanya dhihaka kuhusu kifo! Kipindi hiki kiwe ni fursa ya kusali na kutembelea makaburi, ili kuwasalimia na kuwaombea wale waliolala katika usingi wa amani.

Jumatatu, tarehe 4 Novemba 2019, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea: Makardinali, Maaskofu wakuu na Maaskofu waliofariki dunia katika kipindi cha Mwaka 2018-2019. Hawa ni viongozi waliojisadaka kwa ajili ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Sasa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo amewaita kwenye makao ya uzima wa milele kwani yote yamekamilika, “Consummatum est”. Fumbo la kifo, liwe ni changamoto kwa ajili ya tafakari, kukesha na kutekeleza dhamana na nyajibu mbali mbali kwa uaminifu na ukamilifu kwa kutambua kwamba, wameteuliwa ili kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Fumbo la kifo ni fursa ya kufakari kwa kina na mapana Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Sakramenti zote, na hasa zile za kuingizwa kwa mwamini katika Ukristo, zina kama lengo, Pasaka ya mwisho ya mtoto wa Mungu, ile ambayo kwa kifo inamwingiza katika uzima wa Ufalme wa Mungu. Sasa kinatimilizika kile alichokisadiki katika imani na matumaini: “Nangojea ufufuko wa wafu na uzima wa ulimwengu ujao”. Maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, ambaye ndani mwake, waamini wanachota tumaini lao moja, yaani: kwa kutoka katika maisha ya hapa duniani ili kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kanisa linafundisha kwamba, kwa Mkristo siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo kwa kufanana kamili na “sura ya Mwana” kulikotolewa kwa mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme wa Mungu, uliotangulizwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, hata kama analazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi!

Mababa wa Kanisa wanakumbusha kwamba, kifo ni mshahara wa dhambi.  Kwa wale wanaokufa katika neema ya Kristo Yesu, kifo ni ushirika katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Kifo ni hitimisho la maisha ya hapa duniani na ndiye adui wa mwisho wa mwanadamu atakayeshikishwa adabu. Yesu Mwana wa Mungu alistahimili kifo kwa ajili ya binadamu kwa kutii na uhuru kamili kwa mapenzi ya Baba yake wa mbinguni. Utii wa Kristo Yesu umegeuza laana ya kifo kuwa baraka. Upya huu unapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo yaani, kufa na kufufuka pamoja na Kristo. Liturujia ya Kanisa inafafanua kwa kina kuhusu Fumbo la Kifo. Yaani kwa njia ya kifo, uzima wa waamini hauondolewi ila unageuzwa tu. Nayo makao ya hapa duniani yakishabomolewa, waamini wanapata makao ya milele mbinguni.

Kifo ni mwisho wa safari ya mwanadamu hapa duniani, mwanzo wa kukumbatia na kuambata neema na huruma ya Mungu. Waamini wakumbuke daima kujiandaa kwa ajili ya kupokea kifo chema, kwa kujenga na kudumisha dhamiri nyoofu, isiyokuwa na hofu ya kifo. Kanisa linasadiki na kufundisha kuhusu Kanisa la mbinguni na Kanisa linalosafiri. Wale walio mbinguni kwa kuwa wameunganika na Kristo Yesu kwa undani zaidi wanaliimarisha Kanisa lote katika utakatifu, wanakuza Ibada na kusaidia kulijenga na kuliimarisha zaidi.

Fumbo la Kifo

 

01 November 2019, 14:28