Vatican News
Papa Francisko anawataka Wakristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa utamadunisho unaokita mizizi yake katika ushuhuda wa imani tendaji! Papa Francisko anawataka Wakristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa utamadunisho unaokita mizizi yake katika ushuhuda wa imani tendaji!  (Vatican Media)

Katekesi ya Safari ya Injili Duniani: Utamadunisho wa Injili

Mtume Paulo akasimama katikati ya Areopago na kuwaambia kwamba katika pitapita yake kuhusu Ibada zao, ameona madhabahu iliyoandikwa kwa maneno haya “Kwa Mungu Asiyejulikana”. Mtume Paulo akawahubiria habari zake yeye ambaye wanamwabudu bila kumjua. Huu ni mfano bora katika mchakato wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili mjini Athene. (Mdo. 17:23).

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mzunguko wa Katekesi kuhusu Safari ya Injili Ulimwenguni mintarafu Kitabu cha Matendo ya Mitume ni fursa ya kupembua: mchango wa Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa la Mwanzo na uwepo wa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, uliozindua mchakato mzima wa uinjilishaji. Jumatano tarehe 6 Novemba 2019 safari ya Injili inamkutanisha Mtakatifu Paulo mtume na wanafalasafa wa Athene, nchini Ugiriki waliokuwa wamebobea katika fani zao. Mtume Paulo akasimama katikati ya Areopago na kuwaambia kwamba katika pitapita yake kuhusu Ibada zao, ameona madhabahu iliyoandikwa kwa maneno haya “Kwa Mungu Asiyejulikana”. Mtume Paulo akawaambia sasa anawahubiria habari zake yeye ambaye wanamwabudu bila kumjua. Huu ni mfano bora katika mchakato wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili mjini Athene. (Mdo. 17:23). Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi yake anafafanua kwamba, huu ni mji uliokuwa na umaarufu mkubwa licha na wanasiasa wake kukengeuka, lakini ulikuwa unahifadhi utamaduni wa wananchi wa Ugiriki.

Mtume Paulo aliona jinsi ambavyo mji wa Athene ulivyojaa kwa sanamu, roho yake ikachukizwa sana ndani mwake, badala ya kukimbia, akaamua kusimama kidete ili kuanzisha mchakato wa majadiliano ya kitamaduni, kwa kukutana na kuzungumza na wanafalsafa pamoja na watu mashuhuri mjini humo. Alitembelelea viunga mbali mbali akakutana na watu katika uhalisia wa maisha yao na hatimaye, akaenda Areopago, kiini cha maisha ya kisiasa na kitamaduni, kwani hapa ni mahali ambapo walikutanisha wanafalsafa na wanasiasa. Katika tafakari yake ya kina, Mtume Paulo  akamwona Mwenyezi Mungu akiishi kwenye nyumba, mitaa na viwanja vya mji huo. Anauangalia mji wa Athene kwa jicho la imani, changamoto kwa waamini kuiangalia miji yao kwa jicho la imani, bila kuigeuzia kisogo wala kuitweza ili kutambua uwepo wa Mungu kati ya umati wa watu. Jicho la Mtume Paulo likamwezesha kupenyeza Injili katika moyo wa taasisi muhimu sana kisiasa na kitamaduni yaani Areopago, kielelezo makini cha mchakato wa uinjilishaji wa tamaduni na utamadunisho wa Injili.

Mtume Paulo akamtangaza Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka, kwa kujenga na kudumisha madaraja yanayowakutanisha watu. Mtume Paulo akaanza mahubiri yake kuhusiana na altare ambayo imewekwa wakfu “Kwa Mungu Asiyejulikana”. Akawakumbusha kwamba, Mwenyezi Mungu amefanya maskani na anaishi kati ya watu wake. Mwenyezi Mungu hajifichi kwa wale wanaomtafuta kwa moyo mnyofu, japokuwa wanafanya kwa wasi wasi na kwa namna ambayo haina uhakika wala utaratibu kamili. Huyu ndiye yule Mungu ambaye wanamwabudu bila kumjua. Mtume Paulo anafafanua kuhusu uwepo wa Mungu kwa kukita imani yake katika Biblia inayoonesha ufunuo wa Mungu katika kazi ya uumbaji na ukombozi. Huyu ndiye yule Mwenyezi Mungu ambaye watu wanamfahamu au wameamua kumbeza. Huu ni mwaliko wa kuondokana na ujinga ili kuanza mchakato wa toba na wongofu wa ndani, kwa maana siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki iko mbele yao.

Mtume Paulo anamtangaza Kristo Yesu bila kumtaja kwa jina, kwa kumtambulisha kuwa ni mtu yule aliyechaguliwa na Mungu, naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu. Ufufuo wa wafu ni ufunuo mpya ambao uliwaacha wasikilizaji wake wakiwa wamepigwa butwaa kwa mshangao mkubwa! Mtume Paulo kwa ujasiri mkubwa anamtangaza Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu anayeonekana kuwa ni “upuuzi” kwa watu wengine. Mtume Paulo anafunga vilago na kuondoka kwani juhudi zake zote zinaonekana kana kwamba, zimegonga mwamba. Lakini baadhi ya watu wakashikamana naye, wakaamini; kati yao alikuwamo Dionisio, Mwareopago na mwanamke mmoja jina lake Damari, na watu wengine pamoja nao! Injili inatangazwa na kushuhudiwa mjini Athene na sauti ya mwanaume na mwanamke. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwafundisha jinsi ya kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu kwa njia ya utamadunisho, bila kutumia nguvu. Waamini wawe na ujasiri wa kutamadunisha Injili kwa chachu ya imani, kwa kuwasaidia wale wasiomfahamu Kristo Yesu, ili waweze kumfahamu, kwa kuwafunulia upendo unaolainisha nyoyo ngumu!

Papa: Utamadunisho
06 November 2019, 15:02