Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anazitaka Familia za Kikristo ziwe ni Kanisa dogo la nyumbani, mahali pa katekesi, sala, tafakari na maadhimisho ya mafumbo ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anazitaka Familia za Kikristo ziwe ni Kanisa dogo la nyumbani, mahali pa katekesi, sala, tafakari na maadhimisho ya mafumbo ya Kanisa. 

Katekesi ya Safari ya Injili Duniani: Familia Kanisa dogo la nyumbani

Papa Francisko: Familia ya Akila na mkewe ilikuwa ni mahali ambapo ndugu katika Kristo waliweza kukutanika kwa sala na tafakari ya Neno la Mungu, kiasi kwamba, familia hii ikageuka kuwa ni “Domus ecclesiae” yaani “Kanisa dogo la nyumbani” mahali pa kusoma na kutafakari Neno la Mungu; kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Mfufuka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mzunguko wa Katekesi kuhusu Safari ya Injili Ulimwenguni mintarafu Kitabu cha Matendo ya Mitume ni fursa ya kupembua: mchango wa Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa la Mwanzo na uwepo wa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, uliozindua mchakato mzima wa uinjilishaji unaopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji! Jumatano tarehe 13 Novemba 2019 safari ya Injili inaonesha jinsi ambavyo Mtakatifu Paulo, Mtume alivyoanzisha Kanisa huko Korintho kwa msaada wa Akila pamoja na mkewe Prisila, waliomkaribisha nyumbani kwao, akakaa kwao wakafanya kazi kwa pamoja na kuendelea kuwahubiria Wayahudi na Wayunani kuhusu Habari Njema ya Wokovu. Kutokana na hali mbaya ya hewa iliyokuwa imetanda mjini Roma, Baba Mtakatifu alianza sehemu ya kwanza ya Katekesi yake kwa kuwatembelea na kuwasalimia wagonjwa na wazee waliokuwa wanafuatilia katekesi hii kwa njia ya luninga kutoka kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Paulo VI mjini Vatican.

Baba Mtakatifu amewapongeza wagonjwa na wazee wanaojihimu kufika mjini Vatican hata katika shida na mahangaiko yao na kwamba, hiki ni kielelezo cha upendo wao kwa Kanisa, jambo linatoa faraja kwa wengi. Amewapatia baraka zake za kitume na hatimaye, kuelekea kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kuendelea na Katekesi yake. Kitabu cha Matendo ya Mitume kinamwonesha Mtakatifu Paulo, Mtume baada ya majadiliano katika ukweli na uwazi kuhusu mchakato wa uinjilishaji wa tamaduni na utamadunisho wa Injili, leo yuko Korintho, mji maarufu sana wa biashara kutokana na uwepo wa bandari, uliorahisisha shughuli za biashara na usafiri wa majini. Baba Mtakatifu, kwa muhtasari amegusia historia ya Wayahudi ambao wameteseka sana katika historia ya maisha yao, wakatengwa na kunyanyaswa; wakadhulumiwa na kuuuwawa kikatili, mambo ambayo bado yanaendelea hata katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu anasikitika kusema, tabia hii ni kinyume kabisa cha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wayahudi ni ndugu ya watu wote hakuna sababu ya  kuwatesa na kuwadhulumu.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Akila pamoja na mkewe Prisila au Priska walikuwa ni watu wenye imani kwa Mwenyezi Mungu na wakarimu kwa jirani zao, kiasi hata cha kuweza kumkaribisha Mtakatifu Paulo, Mtume nyumbani kwao. Upendo na ukarimu ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa sanaa ya Kikristo. Kwa kutenda hivi, wanabarikiwa kwa kuinjilishwa na kulipokea Neno la Mungu ambalo ni uweza wa Mungu unaoleta wokovu kwa kila mwamini kwanza kwa Myahudi na kwa Myunani pia. Tangu wakati huo nyumba na familia yao ikapambwa kwa Neno la Mungu ambalo li hai na tena lina nguvu na lina uwezo wa kujenga na kuimarisha nyoyo za watu. Wakashirikiana hata katika kazi yao ya ufundi wa kushona mahema, kazi ambayo Mtakatifu Paulo aliisifia sana kama kielelezo cha ushuhuda wa Kikristo unaojikita katika kazi kama utimilifu wa utu na heshima ya binadamu, bila ya kuwa ni mzigo kwa wengine au kwa jumuiya.

Nyumba hii, ikawa ni mahali ambapo ndugu katika Kristo waliweza kukutanika kwa sala na tafakari ya Neno la Mungu, kiasi kwamba, familia hii ikageuka kuwa ni “Domus ecclesiae” yaani “Kanisa dogo la nyumbani” mahali pa kusoma na kutafakari Neno la Mungu; kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Mfufuka. Kwa nchi zile ambazo hazina uhuru wa kuabudu na uhuru wa kiimani, familia kama hizi zimegeuzwa kuwa ni Makanisa madogo ya nyumbani, mahali ambapo wanaweza kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu. Kwa muda wa mwaka mmoja, nyumba hii ikawa ni ukumbi wa katekesi na hata waliporejea mjini Roma, Paulo Mtume akawakumbuka kwa moyo wa shukrani akiwasalimia mmoja mmoja yaani akina Akila na mkewe Prisila; watenda kazi walioshirikiana naye katika Kristo Yesu, wakawa tayari hata kukatwa kichwa kwa ajili ya maisha ya Mtakatifu Paulo, wote hawa anawashukuru kwa dhati kabisa.

Baba Mtakatifu anasema, hata leo hii kuna familia ambazo ziko hatarini kudhulumiwa, kuteswa na hata kuuwawa kutokana na Injili. Familia ya Akila na Prisila ni mfano bora wa kuigwa kwa ushuhuda wa ukarimu hata katika zile nyakati tete za maisha na utume wa Kanisa. Familia hii inatajwa na Mtakatifu Paulo kuwa ni mfano wa kuigwa katika sadaka na huduma kwa jumuiya ya waamini, kielelezo cha imani tendaji na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo kama kikolezo cha uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Huu ni mwendelezo wa dhamana na utume unaotekelezwa na waamini walei hadi nyakati hizi. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini walei wanashiriki pia; Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo, kiasi kwamba, wanachangia katika maboresho na ukuaji wa imani. Baba Mtakatifu amewakumbusha wanandoa wapya kuhakikisha kwamba, nyumba na familia zao zinakuwa kweli ni Kanisa dogo la nyumbani; kwa kuwa tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa njia ya ukarimu kwa jirani; kwa kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano, ili imani iweze kukua na hatimaye, kukomaa!

Papa: Familia Kanisa Dogo
13 November 2019, 16:04