Vatican News
Mwenyeheri Bartolomeo Fernandes wa Mashahidi ametangazwa kuwa Mtakatifu kwa kufuata kanuni ya "Equipollente" Mwenyeheri Bartolomeo Fernandes wa Mashahidi ametangazwa kuwa Mtakatifu kwa kufuata kanuni ya "Equipollente"  (Vatican Media)

Mtakatifu Bartolomeo Fernandes wa Mashahidi: Kanuni Equipollente

Mtakatifu Bartolomeo Fernandes wa Mashahidi alizaliwa mwaka 1514 huko Ureno. Akaweka nadhiri zake mwaka 1528. Mwaka 1559 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Braga, Ureno. Kati ya Mwaka 1561 hadi mwaka 1563 alishiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mtaguso wa Trento. Akajitahidi kupyaisha maisha na utume wa Kanisa mintarafu Nyaraka za Mtaguso wa Trento.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake binafsi, “Motu Proprio” ijulikanayo kama “Maiorem hac dilectionem” yaani “Kuhusu sadaka ya maisha” anafafanua njia kuu nne ambazo Mama Kanisa anaweza kuzitumia kumtangaza mwamini kuwa Mwenyeheri na hatimaye Mtakatifu. Njia hizo ni: Kifo dini, kielelezo cha pekee katika kumfuasa Kristo, lakini, ikumbukwe kwamba, kielelezo cha juu kabisa cha ushuhuda kwa Kristo na Kanisa lake ni upendo kwa Mungu na jirani. Njia ya pili ambayo mwamini anaweza kutangazwa kuwa ni Mwenyeheri au Mtakatifu ni katika mchakato wa kumwilisha fadhila za kishujaa zinazotekelezwa kwa haraka, bila kusita na kwa moyo mkunjufu, kiasi cha kuonekana kuwa ni fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si tu nguvu za kibinadamu. Huu ni mwelekeo unaomwezesha mwamini kufikiri na kutenda mintarafu mwanga wa Injili. Njia ya tatu inayomwezesha mwamini kutangazwa kuwa Mwenyeheri au Mtakatifu ambayo waamini wengi hawaifahamu sana, lakini imefafanuliwa katika Sheria, Kanuni na Tararibu za Kanisa katika Sheria za Mwaka 1917 inayojulikana kama kutangazwa Mwenyeheri au Mtakatifu kwa kutumia kanuni ya “Equipollente”.

Kanuni hii kimsingi, inatumika kwa nadra sana katika Kanisa kwa ajili ya kesi maalum. Njia ya nne iliyotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko ni sadaka ya maisha ambayo pengine inafumbata baadhi ya mambo msingi yaliyokwisha kufafanuliwa katika hatua tatu zilizotangulia, inataka kutoa kipaumbele cha pekee kwa ushuhuda wa Kikristo unaofumbatwa katika upendo, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushuhuda kwa Kristo na Kanisa lake; ushuhuda unaopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya mwamini kama njia ya kutafuta ukamilifu wa maisha na hatimaye, utakatifu. Sadaka ya maisha inafumbwata kwa namna ya pekee katika fadhila ya: Imani, Matumaini, Busara pamoja na Nguvu. Hizi ni njia ambazo Mama Kanisa anazitumia kwa ajili ya kuwatangaza waamini wake kuwa wenyeheri na watakatifu, lakini kadiri ya historia inavyozidi kusonga mbele, njia hizi zinazonekana kana kwamba, zinawatenga baadhi ya waamini ambao wamekuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa kwa njia ya ushuhuda wa upendo wenye mvuto na mashiko! Yesu mwenyewe anasema, hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. (Rej. Yoh. 15:13).

Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 10 Novemba 2019 amemsifia Mtakatifu na Askofu mkuu Bartolomeo Fernandes wa Mashahidi, aliyetangazwa kuwa Mtakatifu, kwenye Jimbo kuu la Braga, nchini Ureno, Jumapili, tarehe 10 Novemba 2019 kwa kutumia kanuni ya “Equipollente”.  Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, jioni kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kulipatia Kanisa Askofu na mchungaji mwema aliyejisadaka kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni mtakatifu aliyekuwa na Ibada ya pekee ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Humo akajichotea nguvu na ukarimu uliomwezesha kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Ni mfano bora wa kuigwa kama Askofu na mchungaji mwema “Pastor bonus” aliyejisadaka kwa ajili ya uinjilishaji jimboni mwake. Ni kiongozi aliyetoa mchango mkubwa katika maadhimisho ya Mtaguso wa Trento uliofanya mabadiliko makubwa kuhusu dhamana na utume wa Askofu mahalia. Alifariki dunia tarehe 16 Julai 1590. Mara tu baada ya kifo chake, wengi wakamkumbuka kutokana na utakatifu wa maisha, hekima na busara, mtu wa kiasi, aliyejitahidi kusimama kidete kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Alikuwa ni mnyenyekevu na mtu aliyejitahidi kuboresha maisha yake kwa kupenda na kutafuta ukweli; kwa njia ya Neno la Mungu, Sala, Sakramenti pamoja na mafundisho tanzu ya Kanisa, ili aweze kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza vyema watu wa Mungu Jimbo kuu la Braga.

Hata katika madhulumu dhidi ya Kanisa nchini Ureno, Mtakatifu Bartolomeo Fernandes wa Mashahidi aliendelea kusimama kidete kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu, Jimbo kuu la Braga, kiasi hata cha kuhatarisha maisha maisha yake binafsi. Mtakatifu Paulo VI alitambua na kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na Mtakatifu Bartolomeo Fernandes wa Mashahidi katika maisha na utume wake, kiasi kwamba, baada ya kuhitimisha maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, akawakabidhi Mababa wa Mtaguso nakala ya maandiko ya Mtakatifu Bartolomeo Fernandes wa Mashahidi ijulikanayo kama “Stimulus Pastorum”. Alijikita katika mchakato wa uinjilishaji na upyaishaji wa Kanisa; kwa kuwalinda na kuwatetea waamini wake. Akashughulikia matatizo na changamoto za Kanisa kwa ujasiri, busara na hekima iliyokuwa inabubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu.

Kwa ufupi, Mtakatifu Bartolomeo Fernandes wa Mashahidi alizaliwa mwaka 1514 huko Lisbon, Ureno. Akaweka nadhiri zake za daima kwenye Shirika la Wadominican mwaka 1528. Mwaka 1559 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Braga, Ureno. Kati ya Mwaka 1561 hadi mwaka 1563 alishiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mtaguso wa Trento na akajipambanua kuwa ni kati ya wawezeshaji na wahamasishaji wakuu wa maadhimisho ya Mtaguso wa Trento. Akajitahidi kupyaisha maisha na utume wa Kanisa mintarafu Nyaraka za Mtaguso wa Trento. Akaitisha Sinodi ya Jimbo kuu la Braga. Kati ya mwaka 1571 na mwaka 1572 akaanza ujenzi wa Seminari kwa ajili ya kuwaandaa Mapadre:kiroho, kimwili, kiakili na katika shughuli za kitume. Alikazia katekesi kwa waamini walei Tarehe 23 Februari 1582 akang’atuka kutoka madarakani na kurejea kwenye Monasteri kuendelea na maisha yake kama mtawa wa kawaida. Akafariki dunia tarehe 16 Julai 1590. Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza kuwa Mwenyeheri tarehe 4 Novemba 2001. Kardinali Giovanni Angelo Becciu kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 10 Novemba 2019 akamtangaza kuwa ni Mtakatifu kwa kututumia kanuni ya “Equipollente”.

Papa: Mtakatifu
11 November 2019, 11:00