Tafuta

Vatican News
Kumbu kumbu ya Miaka 40 ya Caritas Romana: Ushuhuda wa Injili ya Upendo kwa maskini na wahitaji zaidi. Kumbu kumbu ya Miaka 40 ya Caritas Romana: Ushuhuda wa Injili ya Upendo kwa maskini na wahitaji zaidi.  (ANSA)

Kumbu kumbu Miaka 40 Caritas Romana: Injili ya Upendo kwa maskini

Baba Mtakatifu amepata fursa ya kusikiliza shuhuda mbali mbali na kuitaka kwa namna ya pekee Caritas Romana kutambua udhaifu wa wale wanaowahudumia, kama chanzo cha huduma ya upendo na uponyaji wa ndani unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu amewaonjesha wanadamu huruma, upendo na mshikamano wake wa dhati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jimbo kuu la Roma linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 40 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Msaada la Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Roma, Caritas Romana na Don Luigi di Liegro kunako mwaka 1979 na baada ya huduma kwa maskini, akafariki dunia tarehe 12 Oktoba 1997. Katika maisha yake, ni kiongozi aliyethubutu kusimama kidete kuomba nafasi na haki kwa maskini waliokuwa wananyanyaswa utu na heshima yao mjini Roma. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 29 Novemba 2019 majira ya jioni, ametembelea: Kituo cha Tiba kwa Magonjwa ya Kinywa “Centro Odontoiatrico”, ambamo kuna madaktari 40 wanatoa huduma kwa wagonjwa wa meno zaidi ya 350 na wengi wao ni watoto wagonjwa wanaotoka kwenye familia zenye kipato cha chini kiasi cha kutoweza kumudu gharama za tiba ya meno. Nyumba ya Maskini ya “Santa Giacinta”, inatoa hifadhi na malazi kwa watu 82 ambao wana matatizo ya afya na hali ngumu ya uchumi.

Kituo cha Mshikamano “Emporio della Solidarietà” hii “Supermarket iliyoanzishwa kunako mwaka 2008 kwa ajili ya kutoa huduma ya mahitaji msingi kwa maskini na wenye shida kutoka Roma. Hiki ni kituo kinachowahudumia: wakimbizi na wahamiaji; watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Mwishoni Baba Mtakatifu atatembelea Bwalo la Chakula kwa ajili ya maskini wa mji wa Roma. Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Caritas, maskini wa Roma pamoja na watu wa kujitolea, wanao endelea kujisadaka kila kukicha kwa ajili ya kuwaonjesha maskini ushuhuda wa Injili ya upendo na mshikamano. Hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Makao makuu ya Caritas Romana ni sehemu ya maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 40 ya Caritas Romana ambayo imekuwa kweli ni “Sakramenti ya huduma” kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Watu wengi wanaohudumiwa na Caritas Romana ni watu ambao utu, heshima na haki zao msingi zinasiginwa na umaskini, magonjwa, ubaguzi, upweke hasi pamoja na nyanyaso mbali mbali.

Hawa ni watu ambao wamejeruhiwa katika utu na heshima yao kama binadamu. Caritas Romana katika kipindi cha miaka 40 imekuwa ni kielelezo cha mshikamano wa upendo; shule ya Injili na chachu ya umoja na mshikamano wa watu wa Mungu katika maeneo ya familia, kazi na shule. Huduma hii ya upendo na mshikamano inachota nguvu kutoka katika Injili na maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa anasema Padre Benoni Ambarus, Mkurugenzi mkuu wa Caritas Romana. Caritas katika kipindi cha miaka 40 ya uwepo na utume wake, imejenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini. Imejenga utamaduni na madaraja yanayowakutanisha maskini na watu wa kujitolea; wakimbizi na wahamiaji; wahanga wa mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo pamoja na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi pamoja na kundi kubwa la watu wasiokuwa na fursa za ajira.

Watu wa kujitolea wamejifunza mengi kutoka kwenye shule ya maskini! Wale wanaohudumiwa na Caritas Romana wameshudia nguvu na huruma ya Mungu inayoganga, inayoponya na kuokoa maisha ya mwanadamu: kiroho na kimwili; mambo ambayo yamewaletea mageuzi makubwa katika hija ya maisha yao, kwa kuwajengea imani, matumaini na mapendo. Kwa hakika, Caritas Romana imekuwa ni chemchemi ya upendo na urafiki na maskini wa Roma. Baba Mtakatifu katika salam zake alipowasili katika eneo la tukio amewatakia wote heri na matashi mema, akatawaka kushikamana na kutembea bega kwa bega, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ameitaka Caritas Romana kujenga na kudumisha urafiki na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu amepata fursa ya kusikiliza shuhuda mbali mbali na kuitaka kwa namna ya pekee Caritas Romana kutambua udhaifu wa wale wanaowahudumia, kama chanzo cha huduma ya upendo na uponyaji wa ndani unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu.

Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu amewaonjesha wanadamu huruma, upendo na mshikamano wake wa dhati. Kristo Yesu aliteswa, akafa na siku ya tatu akafufuka kwa wafu. Hii ndiyo hali wanayokumbana nayo maskini, wakimbizi na wahamiaji. Hata hawa Mwenyezi Mungu anataka kuwaonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Mshikamano huu wa upendo, unawapatia jeuri, waamini kumwendea Kristo Yesu ili kumshirikisha yale yanayowasibu kutoka katika undani wa maisha yao! Mwishoni, Baba Mtakatifu anaitaka Caritas Romana kutambua kwamba, hata wao ni dhaifu, watu wanaopendwa na kuokolewa na Mungu. Changamoto na mwaliko wa kugusa Madonda Matakatifu ya Yesu, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, ili kujenga na kudumisha urafiki na udugu wa kibinadamu, tayari kuambatana na Kristo Yesu katika hija ya maisha. Historia ya ukombozi inaonesha jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu alivyoamua kutembea na waja wake katika historia ya maisha yao.

Caritas Romana inapaswa kuendelea kujikita katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama alivyofanya Msamaria mwema. Waoneshe huruma na wawe tayari kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia maskini. Baba Mtakatifu anawaalika na kuwahimiza wakleri, watawa na waamini walei kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini!

Papa: Caritas Romana
30 November 2019, 16:19