Hospitali ya Bambino Gesù inaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 tangu kuanzishwa kwake, kielelezo cha Injili ya huduma na matumaini kwa watoto wagonjwa! Hospitali ya Bambino Gesù inaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 tangu kuanzishwa kwake, kielelezo cha Injili ya huduma na matumaini kwa watoto wagonjwa! 

Jubilei Miaka 150 ya Hospitali ya Bambino Gesù: Huduma kwa wagonjwa!

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 16 Novemba 2019 anakutana na watu 6, 000 kutoka Jumuiya ya Hospitali ya Bambino Gesù. Kati yao kuna watoto 200 pamoja na wazazi wao. Kati yao kuna watoto kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaohudumiwa Hospitalini hapo, kama kielelezo cha mshikamano wa Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini kwa watoto.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican, ilianzishwa kunako mwaka 1869 kama Hospitali ya kwanza kwa ajili ya watoto wagonjwa nchini Italia. Kunako mwaka 1924, familia ya Jacqueline Arabela de Fitz-James Salviati wamiliki wa Hospitali hii, wakatoa zawadi kwa Vatican na kupokelewa na Papa Pio IX. Tangu wakati huo, ikaanza kufahamika kama Hospitali ya Bambino Gesù, Hospitali ya Papa kwa ajili ya watoto wagonjwa. Huduma kwa watoto wagonjwa na maskini anasema Papa Pio XI ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 16 Novemba 2019 anakutana na watu 6, 000 kutoka Jumuiya ya Hospitali ya Bambino Gesù. Kati yao kuna watoto 200 pamoja na wazazi wao. Kati yao kuna watoto kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaohudumiwa Hospitalini hapo, kama kielelezo cha mshikamano wa Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma. Katika kundi hili wamo madaktari, wauguzi, wanafunzi, watafiti, viongozi, wafanyakazi wa hospitali katika ujumla wao bila kuwasahau watu wa kujitolea!

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Hospitali ya Bambino Gesù ni kipindi muafaka cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini! Huu ni muda wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watoto wagonjwa. Ni muda wa kuimarisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati, kama utambulisho wa maisha na utume ya Hospitali ya Bambino Gesù. Ikumbukwe kwamba, utambulisho huu unapata chimbuko lake kutoka katika Injili ya huruma ya Mungu, “nilikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama”. Haya ni matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji. Hii ndiyo changamoto changamani ambayo imefanyiwa kazi na Mama Kanisa kwa kuanzisha vituo vya huduma kwa ajili ya wagonjwa na maskini, kama sehemu ya utekelezaji wake wa utume wa kinabii: kwa kusoma alama za nyakati, kusikiliza na hatimaye, kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii mintarafu mwanga wa Injili.

Uwepo na utume wa Hospitali ya Bambino Gesù ni ndoto ya upendo, kielelezo cha upendo unaowawezesha waamini kuona, ili kutambua na kung’amua tayari kujizatiti kutoa msaada, kama jibu makini kwa mahitaji ya watu kwa nyakati hizi na hata kwa siku za mbeleni! Ndoto ya upendo inawawajibisha waamini kutoa huduma makini, kujenga uwezo wa ujirani mwema na mshikamano na wale wote wanaoteseka, kielelezo makini cha udugu na mshikamano wa dhati! Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatatu, tarehe 19 Machi 2019, wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Hospitali ya Bambino Gesù. Tukio hili lilihudhuriwa pia na viongozi waandamizi kutoka Serikali ya Italia chini ya uongozi wa Rais Sergio Mattarella pamoja na viongozi wa Kanisa kutoka Italia. Kardinali Parolin anakaza kusema, historia ya Hospitali ya Bambino Gesù ni maono ya watu yanayomwilishwa katika mradi unaoishirikisha jamii na hatimaye, kuupatia utambulisho wake kama kielelezo cha upendo na mshikamano kwa ajili ya wagonjwa hata kwa siku za mbeleni!

Historia ya huduma ya afya imebadilika sana nchini Italia, ikilinganishwa na miaka 150 iliyopita wakati Hospitali hii ikianzishwa. Huduma za Afya Kitaifa zimeendelea kuimarishwa, kwa kujikita katika usawa unaofafanuliwa kwenye Katiba ya Italia, ili kulinda na kudumisha uhai! Ubora wa huduma inayotolewa unapaswa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu katika ukweli wake wote: katika: hisia, mahusiano, kisaikolojia na katika maisha ya kiroho. Hospitali hii, katika historia yake, kuanzia mwaka 1985 imeendelea kujipambanua kuwa ni Kituo cha Tafiti za Kimataifa, huduma ambayo inatambuliwa ulimwenguni kote! Hospitali hii ni Kituo Kikuu cha Tafiti za Magonjwa ya Watoto Barani Ulaya. Hatua hii imeweza kufikiwa kutokana na Kanisa kuendelea kuwekeza zaidi katika tafiti za kisayansi, miundo mbinu, teknolojia pamoja na katika rasilimali watu, kama njia ya kukabiliana na changamoto changamani kwa siku za usoni. Licha ya maboresho katika sekta ya afya, bado Kanisa litaendelea kuwekeza katika huduma kwa wagonjwa, kama sehemu ya utekelezaji wa dhamana na utume wake wa kinabii, kwa ajili ya maskini wapya wanaoendelea kujitokeza katika sekta ya afya!

Hawa ni wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa ya kudumu; wagonjwa wa magonjwa nasibu, wagonjwa wa afya ya akili, wazee na maskini wanaoteseka kupata huduma bora ya tiba. Wote hawa wanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee pamoja na kuzishirikisha familia husika, ili hatimaye, kujenga mtandao wa mshikamano katika huduma, ili kuimarisha imani, urafiki na udugu! Hii ni Hospitali inayotekeleza dhamana na wajibu wake, ndani na nje ya Italia kama kielelezo cha Ukatoliki wa Kanisa linaloangalia pia watoto maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Utume huu kama unavyojulikana “ubi amor ibi oculos” unaiwezesha Hospitali kushirikishana ujuzi na maarifa; majiundo ya kitaaluma pamoja na kusindikizana kama inavyojionesha katika ujenzi na hatimaye, ufunguzi wa Hospitali ya Watoto Wadogo, huko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Hospitali hii ni shuhuda wa umoja na upendo kati ya watu wa Mungu! Huu ndio upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake!

Huduma inayotolewa Hospitalini hapo inawalenga watoto wagonjwa pamoja na familia zao. Hii ni Hospitali ambayo imegawanyika katika maeneo makubwa manne: Makao makuu ya Hospitali, Kituo cha “San Paolo”, Kituo cha Palidoro pamoja na “Santa Marinella”. Jumla Hospitali ina vitanda 607 na ina uwezo wa kulaza wagonjwa 27, 000 kwa Mwaka. Hospitali ina uwezo wa kupandikiza viungo kwa wagonjwa 339. Wagonjwa 44, 000 wanahudumiwa katika “Day Hospital”. Familia 3700 zinapata huduma kwa gharama nafuu na kwamba, asilimia 13% ya watoto wagonjwa wanaohudumiwa hapa ni kutoka nje ya Italia. Hawa ni watoto wanaotoka katika maeneo ya vita, nchi maskini zaidi duniani; watoto ambao wanahitaji kupata huduma ya tiba kwa muda mrefu zaidi. Hospitali ya Bambino Gesù inashirikiana kwa karibu zaidi na Hospitali zinazoendeshwa na Makanisa, sehemu mbali mbali za dunia! Barani Afrika, inashirikiana pia na Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Manyoni, Singida nchini Tanzania pamoja na Hospitali ya Watoto Wadogo Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Wagonjwa Duniani 2019 anasema, Huduma kwa wagonjwa na wale wote wanaoteseka ni utekelezaji wa Injili ya upendo na huruma ya Mungu kwa watu wote. Hii ni sehemu ya mchakato wa kutangaza, kushuhudia na kujenga Ufalme wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kama alivyofanya Msamaria mwema. Kumbe, ni wajibu wa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa wagonjwa, maskini na wale wote wanaoteseka. Baba Mtakatifu anawataka watu wamwone Kristo Yesu anayeendelea kuteseka kati pamoja na wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Bambino Gesù 150 Yrs
15 November 2019, 12:06