Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana nchini Japan kuwa ni mashuhuda wa imani, matumaini na wajenzi wa urafiki wa kijamii. Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana nchini Japan kuwa ni mashuhuda wa imani, matumaini na wajenzi wa urafiki wa kijamii. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Japan: Utume wa vijana!

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa vijana wa kizazi kipya nchini japan amegusia kuhusu: Ubaguzi na “Cyberbullying” yaani unyanyasaji na uonevu wa kimtandao; Ubora wa elimu; nafasi ya Mungu katika maisha ya vijana pamoja na mapambano ya umaskini wa maisha ya kiroho. Vijana wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa urafiki wa kijamii. Wawe ni vyombo vya matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anapenda kujielekeza zaidi katika utume kwa vijana, ili kujenga sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwaongoza vijana kufanya maamuzi mazito katika maisha kwa kuwa na msimamo thabiti unaojikita katika imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! Vijana wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa uinjilishaji mpya kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Japan kuanzia tarehe 23 hadi 26 Novemba 2019 inaongozwa na kauli mbiu “Linda Maisha Yote”. Jumatatu, tarehe 25 Novemba 2019 amekutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya kutoka Japan, waliokusanyika kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Jimbo Kuu la Tokyo. Amesikiliza shuhuda za vijana, ametambua pia uwepo wa vijana kutoka mataifa mbali mbali wanaotafuta hifadhi ya maisha kama wakimbizi na kwamba, wote kwa pamoja wanapaswa kujifunza kujenga jamii wanayoitaka kwa siku za mbeleni.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amegusia kuhusu: Ubaguzi na “Cyberbullying” yaani unyanyasaji na uonevu wa kimtandao;   Ubora wa elimu; nafasi ya Mungu katika maisha ya vijana pamoja na mapambano ya umaskini wa maisha ya kiroho. Vijana wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa urafiki wa kijamii. “Cyberbullying” ni uonevu na unyanyasaji unaotendeka kupitia vifaa vya mawasiliano vya kidigitali, mfano simu, kompyuta, “tablets”, uonevu huu unaweza kutokea kupitishia jumbe fupi za maneno, maandishi ya blogs, program za kwenye simu ama kupitia mitandao ya kijamii, majukwaa nk mahali ambapo watu wanaweza kuhusika kwa kuona, kuandika ama kushirikishana. Uonevu huu unahusisha kutuma, kuandika ama kushirikishana taarifa hasi, za uzushi, uongo au za kuumiza na kudhalilisha utu na heshima yaw engine ambao wanageuka kuwa ni wahanga. Inaweza kuhusisha kushirikishana taarifa za mtu binafsi bila hiari yake, na kusababisha aibu, udhalilishaji. Na matendo haya yanapelekea kwenye uvunjifu mkubwa wa makosa ya jinai. Baba Mtakatifu anasema, leo hii vijana wengi wanaendelea kupata ujasiri wa kuzungumzia kuhusu uonevu na unyanyasaji wa kimtandao.

Vijana wanapaswa kujenga tabia ya kujiamini na kukabiliana na changamoto za maisha kwa ujasiri na busara, watambue nguvu na uzuri uliomo ndani mwao; udhaifu na mapungufu katika maisha na kwamba, kwa wale wanaotaka “kujimwambafai kwa kutumia mitandao ya kijamii wanadhani kwamba, kwa kufanya hivi wanakuwa ni watu muhimu sana katika jamii. Baba Mtakatifu anasema hiki ni kinyume chake kabisa kwani hawa ni watu waoga lakini wanataka kujitutumua kwa kutumia mitandao ya kijamii. Jukumu la kudhibiti unyanyasaji, uonevu na ubaguzi wa kimtandao ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na vijana wenyewe kwa kuunganisha nguvu zao huku wakisaidiwa na taasisi za elimu pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kusema “HAPANA” ili kuwaonesha kwamba, haya wanayotenda si mambo mazuri kwa jamii. Woga na wasi wasi ni adui mkubwa wa wema kwa sababu woga ni adui mkubwa wa upendo na amani. Dini mbali mbali zinafundisha: maridhiano, utulivu, huruma na upendo na kamwe si woga, wasi wasi wala mipasuko.

Watu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na wala hakuna sababu ya kuwanyanyasa, kuwatenga na kuwabagua wengine. Ulimwengu unahitaji ushiriki na mchango wa kila mmoja na kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda na kuwathamini vijana, anawataka washirikiane na kushikamana ili waweze kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuanzia sasa kujifunza kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa vijana wenzao, kwa kuwasikiliza, kuwasaidia na kushirikiana nao, ili kujenga upendo wa dhati unaoweza kuleta mabadiliko makubwa katika ulimwengu mamboleo. Vijana wawe wakarimu kwa kutumia vyema rasilimali muda kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya vijana wenzao, bila kusahau kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala, tafakari na ushiriki mkamilifu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Sala ina changamoto zake, lakini sala maana yake ni kutoa nafasi ili aweze kuwaangalia na kuwajazia kile kinachopunguka.

Hata katika nchi zilizoendelea kwa kiwango kikubwa kama Japan, lakini bado kuna maskini wa maisha ya kiroho; watu ambao hawana hata chembe ya furaha; wamepoteza kipaji cha kushangaa kwani kwao kila kitu ni kawaida tu! Wanaweza kuwa na utajiri wa fedha na mali, lakini ni maskini wakutupwa katika maisha ya kiroho, kwani wanashindwa kusherehekea maisha na jirani zao. Ni watu wanaoendelea kuzama na kutopea katika upweke hasi na matokeo yake, wakati wowote ule “wanaweza kuchungulia kaburi”. Hakuna umaskini mkubwa katika maisha anasema Mama Theresa wa Calcutta kama upweke hasi! Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kujizatiti kupambana kufa na kupona na umaskini wa maisha ya kiroho kwa kutoa kipaumbele kwa watu kuliko vitu; kwa kujenga na kudumisha urafiki wa dhati na Mwenyezi Mungu, tayari kushirikishana na wengine karama na mapaji yao. Vijana wawe ni mashuhuda na wajenzi wa urafiki wa kijamii, kwa kuwekeza zaidi katika Injili ya matumaini.

Vijana wajenge utamaduni wa wa kukutana na watu, kuwakubali na kuwapokea jinsi walivyo; kujenga na kuimarisha udugu wa kibinadamu; kwa kuheshimu utu wao na hasa zaidi wale wanaohitaji huruma, upendo na kufahamika katika maisha. Hakuna sababu ya kumnyanyasa, kumshambulia au kumtenga mtu awaye yote! Vijana wajifunze kuona na kuthamini karama za jirani zao. Baba Mtakatifu anawataka vijana kukuza na kudumisha moyo wa sala na tafakari, ili kukua na hatimaye kupata ukomavu wa ndani kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda upeo. Vijana wanaweza kugundua yote haya kwa kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya vijana wenzao. Kama wanafunzi, wanapaswa kujenga na kuimarisha uhusiano na mafungamano mema kati yao na walimu pamoja na walezi wao ili kuwafunda na kuwapatia utambulisho katika maisha.

Baba Mtakatifu anawataka vijana wa Japan kujenga na kuimarisha urafiki na vijana wenzao ambao ni wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi, ili waweze kujisikia kwamba wako na ndugu zao katika Kristo Yesu. Wajitahidi kutafuta majibu makini kwa maswali na changamoto wanazokabiliana nazo katika hija ya maisha yao hapa duniani. Watambue maana ya maisha na kwamba, Japan na ulimwengu mzima unawahitaji vijana wa kizazi kipya; watu ambao ni wakarimu, wenye furaha na wanao wajali ndugu zao katika shida. Mwishoni, anawataka vijana kukua na kukomaa katika hekima na busara ili kugundua furaha ya kweli katika maisha.

Papa: Vijana Japan

 

25 November 2019, 14:56