Tafuta

Vatican News
Papa Francisko amewatumia watu wa Mungu nchini Japan ujumbe wa imani, matumaini na mapendo, wakati huu anapojiandaa kwa hija yake ya kitume nchini humo! Papa Francisko amewatumia watu wa Mungu nchini Japan ujumbe wa imani, matumaini na mapendo, wakati huu anapojiandaa kwa hija yake ya kitume nchini humo!  (ANSA)

Hija ya Papa Francisko Japan: Ujumbe kwa watu wa Mungu

Kauli mbiu iliyochaguliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Japan kwa ajili ya hija ya Baba Mtakatifu nchini Japan ni “Linda Maisha Yote”. Huu ni ujumbe unaowataka watu wa Mungu nchini Japan kusimama kidete kulinda: utu na heshima ya binadamu dhidi ya vitisho vinavyohatarisha misingi ya amani na utulivu na hasa zaidi mapambano ya silaha. Japan inatambua fika madhara ya vita.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 23 hadi 26 Novemba 2019 anafanya hija ya kitume nchini Japan inayoongozwa na kauli mbiu “Linda Maisha Yote”. Nembo ya hija hii ni mwali wa moto unaohimiza upendo unaopaswa kumwilishwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kulinda maisha. Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linasema, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa. Maandiko Matakatifu yanabainisha kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba dunia na kuifanya, ndiye aliyeifanya imara, hakuimba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu. Ili kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu kuna haja wanasema Maaskofu kusimama kidete kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa watu wa Mungu nchini Japan kwa njia ya video anasema, kwa sasa yuko njiani kwenda Japan ili kuwatembelea na kwamba, anapenda kuwatumia ujumbe wa urafiki.

Kauli mbiu iliyochaguliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Japan kwa ajili ya hija ya 32 ya Baba Mtakatifu nchini Japan ni “Linda Maisha Yote”. Huu ni ujumbe mzito unaotikisa “sakafu ya nyoyo za watu” ili kusimama kidete kulinda tunu msingi, utu na heshima ya binadamu dhidi ya vitisho vinavyohatarisha misingi ya amani na utulivu na hasa zaidi mapambano ya silaha. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Japan inatambua fika madhara ya vita. Anapenda kuchukua nafasi hii kuungana na Japan ili nguvu ya uharibifu kutoka kwenye silaha za kinyuklia, isirejee tena na kusababisha madhara makubwa katika historia ya maisha ya binadamu. Matumizi ya silaha za kinyuklia ni kinyume kabisa cha kanuni maadili. Familia ya Mungu nchini Japan inatambua fika umuhimu wa utamaduni wa majadiliano na udugu miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali; ili kujenga umoja na mshikamano sanjari na kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu, tayari kujielekeza zaidi katika mchakato wa maendeleo fungamani ya watu wote.

Baba Mtakatifu anatumaini kwamba, hija yake ya kitume nchini Japan itasaidia kuimarisha mafungamano na utamaduni wa watu kukutana ili kupata amani ya kudumu; amani ambayo kamwe haiwezi kurejea tena nyuma. Uzuri wa amani ya kweli ni kwamba, inapaswa kulindwa kwa nguvu zote. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, katika hija hii, atapata nafasi ya kujionea uzuri asilia ambao kimsingi ni utambulisho wa taifa lao pamoja na kuonesha nia ya kushirikiana kuongeza nguvu ya kulinda maisha ya binadamu na ardhi kama nyumba ya wote, inayoelezewa kwa kutumia maua ya matunda ya “Prunus”. Baba Mtakatifu anatambua fika kwamba, wakati huu, kuna watu wanaoendelea kuchakarika mchana na usiku ili kuhakikisha kwamba, wanafanikisha hija yake ya kitume nchini Japan. Anapenda tangu wakati huu, kuwashukuru kwa moyo wote, huku akitumainia kwamba, wakati wa hija yake, atapata nafasi ya kuwa pamoja nao na kwamba, hizi ni siku ambazo zitapambwa kwa neema na furaha. Anapenda kuwahakikishia sala za mshikamano kwa ajili ya watu wote wa Mungu nchini Japana. Anawaalika wao pia kumkumbuka na kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Papa: Japan 2019
18 November 2019, 09:54