Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amewasili mjini Bangkok nchini Thailand kwa ajili ya hija yake ya kitume: 19-23 Novemba 2019. Baba Mtakatifu Francisko amewasili mjini Bangkok nchini Thailand kwa ajili ya hija yake ya kitume: 19-23 Novemba 2019. 

Hija ya Papa Francisko nchini Thailand: Salam na matashi mema!

Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 20 Novemba 2019 amewasili mjini Bangkok nchini Thailand kuanza hija yake ya kitume. Alipowasili uwanjani hapo, amelakiwa na viongozi wa Serikali na Kanisa na kusalimiana nao na baadaye akakagua gwaride la heshima kwa ajili yake, lililoandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama nchini Thailand. Lengo ni kupyaisha mwamko wa kimisionari!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Habari Njema ya Wokovu haina budi kutangazwa na kushuhudiwa kwa ari na moyo mkuu, kwa njia ya tunu msingi za maisha ya Kikristo kama kielelezo cha imani tendaji! Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 19-23 Novemba 2019 anafanya hija ya kitume nchini Thailand inayoongozwa na kauli mbiu: “Mitume wa Kristo, Wamisionari Mitume”. Hija hii ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 tangu kuanzishwa kwa utume wa Vikarieti ya Siam kunako mwaka 1669. Baba Mtakatifu anawataka Wakristo nchini Thailand kuwa kweli ni wafuasi amini wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Wakristo wawe ni wamisionari mitume, vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, watu ambao wako tayari kujisadaka kwa ajili ya uinjilishaji unaopania kuleta upyaisho katika maisha ya watu na kama njia ya kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili.

Baba Mtakatifu Jumatano tarehe 20 Novemba 2019 amewasili mjini Bangkok nchini Thailand kuanza hija yake ya kitume. Alipowasili uwanjani hapo, amelakiwa na viongozi wa Serikali na Kanisa na kusalimiana nao na baadaye akakagua gwaride la heshima kwa ajili yake, lililoandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama nchini Thailand. Baadaye, Baba Mtakatifu alikwenda moja kwa moja hadi kwenye ubalozi wa Vatican kwa mapumziko mafupi. Alipowasili ubalozini hapo, amekutana na kikundi cha waseminari, wanovisi na vijana kutoka katika parokia za jirani, wakamtumbuiza kwa ngoma asilia! Baadaye ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Ubalozi wa Vatican na hatimaye, akapata chakula cha usiku ubalozini hapo. Kwa ufupi, Jumatano hakukuwa na ratiba yenye matukio ya hadhara.

Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Alhamisi, tarehe 21 Novemba 2019, Baba atakutana na kuzungumza na Jenerali Prayuth Chan Ocha, Waziri mkuu wa Thailand, baadaye atakutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, viongozi wa kisiasa, wanadiplomasia, viongozi wa kidini pamoja na viongozi wa vyama vya kiraia nchini Thailand. Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Patriaki mkuu Somdej Phra Maha Muneewong wa dini wa Wabudha nchini Thailand. Kama kielelezo cha mshikamano na wagonjwa pamoja na wale wote wanaoteseka kiroho na kimwili, Baba Mtakatifu atatembelea Hospitali ya St. Louis iliyoanzishwa kunako mwaka 1898 kama kielelezo cha huruma na uwepo wa Mungu kati ua waja wake. Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kuzungumza na Jumuiya ya Hospitali ya St. Louis, baadaye atawatembelea wagonjwa na walemavu ili kuwafariji. Baba Mtakatifu atapata pia fursa ya kumtembelea Mfalme Maha Vajiralongkorn “Rama X”.

Baadaye jioni, Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Uwanja wa Taifa wa Bangkok nchini Thailand, Mama Kanisa anapoadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria kutolewa Hekaluni, sanjari na Maadhimisho ya Siku ya Watawa wa Ndani. Waamini wanakumbushwa kwamba, Kanisa ni nyumba ya Sala na Ibada, mahali ambapo Mafumbo matakatifu yanaadhimishwa, ili kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa. Na kwa Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu Francisko atakuwa anahitimisha rasmi siku ya Alhamisi. Baba Mtakatifu Francisko Francisko kabla ya kuondoka mjini Vatican, alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na kikundi cha wazee wanaotunzwa na Shirika la Masista Wadogo kwa ajili ya Maskini. Akiwa njiani amezungumza na waandishi wa habari ambao wako kwenye msafara wake.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amewashukuru wadau wa tasnia ya mawasiliano kwa kazi yao kubwa wanayoitekeleza kwa ajili ya jamii. Kwa sababu watu wana haki ya kuhabarishwa yale mambo msingi yanayojiri sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa namna ya pekee wakati huu wa hija yake nchini Thailand na Japan. Watu wafahamishwe utajiri wa tamaduni za watu wa Bara la Asia. Baba Mtakatifu akiwa njiani, amewatumia salam za matashi mema marais wa: Italia, Croatia, Bosnia Herzegovina, Serbia, Montenegro, Bulgaria, Uturuki, Iran, Afghanistan, India pamoja na Myanmar. Baba Mtakatifu katika salam zake kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia amemwelezea kwamba,  anafanya hija ya kitume nchini Thailand na Japan, ili aweze kukutana na ndugu zake katika imani. Anawatakia watu wote wa Mungu nchini Italia, heri na baraka, amani, utulivu na ushirikiano. Alipofika kwenye anga la Bulgaria, Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa Rais Rumen Radev wa Bulgaria, amemkumbusha kuhusu hija yake ya kitume aliyoifanya hivi karibuni nchini Bulgaria, mwishoni amewatakia matashi mema, amani, ustawi na maendeleo.

Papa: Thailand

 

20 November 2019, 14:33