Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 23 Novemba 2019 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Japan: Umuhimu wa kulinda Injili ya uhai na ushuhuda wa imani. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 23 Novemba 2019 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Japan: Umuhimu wa kulinda Injili ya uhai na ushuhuda wa imani. 

Hija ya Papa Francisko nchini Japan: Hotuba kwa Maaskofu Katoliki Japan

Katika hotuba yake, Papa amepembua kwa ufupi, historia ya uinjilishaji nchini Japan; umuhimu wa ushuhuda wa imani; Kanisa katika mchakato wa kulinda maisha; dhamana ya uinjilishaji unaokita mizizi yake katika misingi ya haki na amani na mwishoni ni changamoto changamani za watu wanaoishi mjini. Papa ametumia fursa hii kuwashukuru watu wa Mungu nchini Japan kwa ukarimu wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Japan kuanzia tarehe 23 hadi 26 Novemba 2019 inaongozwa na kauli mbiu “Linda Maisha Yote”. Huu ni ujumbe unaowataka watu wa Mungu nchini Japan kusimama kidete kulinda: utu, haki na heshima ya binadamu dhidi ya vitisho vinavyohatarisha misingi ya amani na utulivu na hasa zaidi mapambano ya silaha. Japan inatambua fika madhara ya vita na matumizi ya silaha za atomiki; maafa makubwa ya tetemeko kubwa la ardhi na tsunami iliofuatia vilisababisha vifo vya watu zaidi ya 20,000 nchini Japan. Uharibifu uliosababishwa kwenye mtambo wa nyuklia wa Fukushima Daichi ukapelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao. Haya ni mambo ambayo bado yameacha kumbu kumbu hai katika maisha ya wananchi wa Japan. Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linasema kuna haja ya kujizatiti zaidi “Kulinda maisha yote”.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 23 Novemba 2019 ameanza rasmi hija yake ya kichungaji nchini Japan. Alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Tokyo, amelakiwa na  viongozi wa Serikali na Kanisa, akakagua gwaride la heshima na hatimaye, akaelekea kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Japan ambako amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Japan, CBCJ. Katika hotuba yake, amepembua kwa ufupi, historia ya uinjilishaji nchini Japan; umuhimu wa ushuhuda wa imani; Kanisa katika mchakato wa kulinda maisha; dhamana ya uinjilishaji unaokita mizizi yake katika misingi ya haki na amani na mwishoni ni changamoto changamani za watu wanaoishi mijini.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru watu wa Mungu nchini Japan kwa ukarimu wao na kwamba, tangu akiwa kijana mbichi alitamani sana kutembelea nchini Japan na leo hii Mwenyezi Mungu amemkirimia fursa ya kutembelea Japan kama hujaji wa imani, akifuata nyayo za wamisionari kama Mtakatifu Francisko Xavier, muasisi wa uinjilishaji wa awali nchini Japan. Baba Mtakatifu anawashukuru wale wote waliojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili nchini Japan; wakajitahidi kuwahudumia watu wa Mungu kwa huruma na upendo, kiasi hata cha kubahatika kuwa na wafiadini kama Mtakatifu Paulo Mikki na wenzake na Mwenyeheri Justo Takayama Ukon, baada ya majaribu makubwa hatimaye, wakayamimina maisha yao kama ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Sadaka ya maisha ilisaidia kupyaisha imani miongoni mwa Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo nchini Japan, zikakua na kukomaa na hatimaye, kuzaa matunda.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza Wakristo waliofichika kwenye Mkoa wa Nagasaki ambao kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Maisha ya Sala na Katekesi makini, wakafanikiwa kuwarithisha watoto wao amana na utajiri wa imani. Familia zao zikageuka kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani, taswira kama ile ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Zote hizi ni juhudi za Kristo Yesu, ili kuhakikisha kwamba, waja wake wanaendeleza imani kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Ushuhuda wa imani ni sehemu ya vinasaba vya Kanisa dhidi ya tabia ya watu kukata tamaa na hivyo kuendelea kulipyaisha Kanisa licha ya nyanyaso na madhulumu waliyokumbana nayo Wakristo nchini Japan. Matokeo yake ni imani kuendelea kukita mizizi yake kwenye utamaduni wa watu wa Mungu nchini Japan, kiasi hata cha kuthubutu kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ni hatua muhimu sana katika historia ya Kanisa Katoliki nchini Japan na ulimwenguni kwa ujumla. Kuna baadhi ya Makanisa na vijiji ambavyo vinatambuliwa na Jumuiya ya Kimataifa kama urithi wa kimataifa.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, Kanisa lina wajibu na dhamana ya kulinda maisha, kukuza na kuendeleza mchakato wa kutamadunisha Injili, ili kuinjilisha tamaduni pamoja na kukoleza moyo wa majadiliano. Japan imechangia sana katika ukuaji wa tamaduni mbali mbali Barani Ulaya. Kulinda maisha yote maana yake ni kupenda na kuthamini maisha ya wale wote ambao wamewekwa chini ya ulinzi na usimamizi wao kama Maaskofu. Watambue kwamba, maisha ni zawadi. Kumbe, wanapaswa kutangaza na kushuhudia Injili sanjari na kulinda maisha kwa ajili ya mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu mintarafu mwanga wa Injili ya Kristo Yesu. Kanisa Katoliki nchini Japan halina budi kujizatiti katika mchakato wa uinjilishaji, kwa njia ya ushuhuda wa maisha na majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali.

Kanisa liwe ni shuhuda wa ukarimu kwa wageni kama kielelezo cha utambulisho na mafungamano ya dhati na Kristo Yesu. Kanisa linaweza kushuhudia kwa uhuru zaidi masuala tete ya haki na amani duniani. Mashambulizi ya mabomu ya atomiki kwenye miji ya Nagasaki na Hiroshima yameacha madhara makubwa katika maisha ya watu, changamoto na mwaliko kwa Kanisa kuwa ni sauti ya kinabii dhidi ya utengenezaji, usambazaji, matumizi na ulimbikizaji wa silaha za kinyuklia. Mahangaiko ya waathirika wa mashambulizi ya mabomu ya atomiki kiroho na kimwili ni mwaliko kwa Kanisa kuwatangazia Injili ya matumaini, uponyaji na upatanisho. Hii inatokana na ukweli kwamba, nguvu ya Ibilisi inalenga kubomoa bila hata ya kuzingatia asili na utambulisho wa watu. Baba Mtakatifu ameyakumbuka pia majanga asilia ambayo yanaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Amewaombea wote walioathirika kwa majanga haya na kwamba, iwe ni nafasi ya kuendelea kujizatiti zaidi katika kulinda maisha kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahimiza Wakatoliki nchini Japan kuwa kweli ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili katika jamii. Taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vya Kikatoliki ni mtaji tosha katika mchakato wa uinjilishaji pamoja na mchango wa kuwafunda wasomi na kwamba, ubora wa elimu inayotolewa kwenye taasisi za Kanisa lazima zijielekeze zaidi katika kutoa utambulisho na utume wa Kanisa Katoliki. Baba Mtakatifu anasema, anatambua fika changamoto changamani wanazokabiliana nazo watu wa Mungu wanaoishi kwenye miji mikubwa duniani. Hawa ni watu wanaokumbwa na upweke hasi, hali ya kukata tamaa pamoja na kutengwa. Yote haya yamepelekea kuongezeka kwa idadi ya watu wanaojinyonga, kuchanganyikiwa katika maisha pamoja na kukosa mwelekeo sahihi wa maisha ya kiroho. Waathirika wakuu ni vijana wa kizazi kipya.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu nchini Japan kuhakikisha kwamba, wanajielekeza katika huduma kwa vijana, kwa kusikiliza na kujibu kwa dhati kabisa matamanio yao halali. Kanisa lijitahidi kuwajengea vijana wa Japan mwelekeo mpya wa utamaduni dhidi ya ufanisi, juhudi na mafanikio na kuanza kujikita katika utamaduni wa ukarimu, upendo wa dhati na kuwajali watu wote bila ubaguzi na wala si wale tu waliofanikiwa na kufurahia maisha. Ari, mawazo na nguvu ya vijana wa kizazi kipya zikitumika barabara ni chemchemi ya matumaini kwa vijana wenzao na ushuhuda wa upendo wa Kikristo. Huku ndiko Maaskofu wanapaswa kujielekeza zaidi kwa kuweka sera na mikakati ya shughuli za kichungaji maeneo ya vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu pamoja na mahali pa kazi, ili kuwasindikiza waamini kwa Injili ya huruma na mapendo.

Papa: Maaskofu Katoliki Japan

 

23 November 2019, 17:11