Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 27 Novemba 2019 ametoa muhtasari wa hija yake ya kitume nchini Thailand na Japan, Novemba 2019. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 27 Novemba 2019 ametoa muhtasari wa hija yake ya kitume nchini Thailand na Japan, Novemba 2019.  (Vatican Media)

Muhtasari wa Hija ya Kitume ya Papa Francisko: Thailand na Japan

Baba Mtakatifu wakati wa katekesi yake, Jumatano tarehe 27 Novemba 2019 ametumia fursa hii kuwashukuru viongozi wa Serikali na Kanisa pamoja na watu wote wa Mungu kutoka Thailand na Japan kwa wema na ukarimu waliomwonesha wakati wa hija yake ya kitume nchini mwao. Amegusia umuhimu wa kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini kama nyenzo ya kuenzi amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Yesu Mfufuka alipokuwa na wanafunzi wake kumi na mmoja pale Mlimani Galilaya, akawaambia kwamba, amepewa mamlaka yote mbinguni na duniani na hatimaye, akawatuma kwenda kuwafanya mataifa yote kuwa ni wanafunzi wake, wakiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na Roho Mtakatifu pamoja na kuwafundisha kuyashika yote aliyowaamuru wao. Na tazama Yesu yuko pamoja nao siku zote, hata ukamilifu wa Dahari. (Rej. Mt. 28: 16-20). Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 19-23 Novemba 2019 amefanya hija ya 32 ya kitume nchini Thailand iliyoongozwa na kauli mbiu: “Mitume wa Kristo, Wamisionari Mitume”. Hija hii ilikuwa ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 tangu kuanzishwa kwa utume wa Vikarieti ya Siam kunako mwaka 1669. Kuanzia tarehe 23 hadi 26 Novemba 2019,  Baba Mtakatifu amekuwa nchini Japan na hija hii imeongozwa na kauli mbiu “Linda Maisha Yote”. Pamoja na mambo mengine, Baba Mtakatifu alipenda kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini, haki na amani.

Baba Mtakatifu alipata nafasi ya kutembelea Hiroshima na Nagasaki kama alivyofanya Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1981. Baba Mtakatifu wakati wa katekesi yake, Jumatano tarehe 27 Novemba 2019 ametumia fursa hii kuwashukuru viongozi wa Serikali na Kanisa pamoja na watu wote wa Mungu kutoka Thailand na Japan kwa wema na ukarimu waliomwonesha wakati wa hija yake ya kitume nchini mwao. Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kuweza kushuhudia amana na utajiri wa maisha ya kiroho na kitamaduni kutoka kwa wananchi wa Thailand. Amewatia shime kusonga mbele katika mchakato wa kuimarisha mafungamano ya kijamii, ili kudumisha amani na maridhiano kati ya wananchi wake. Maendeleo ya uchumi yawe ni kwa ajili ya mafao ya wengi na hasa zaidi katika mchakato wa kuganga na kuponya majeraha ya biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na kuwasaidia waathirika wa mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo.

Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na viongozi wa dini ya Kibudha, huku akifuata nyayo za watangulizi wake, ili kukuza na kudumisha upendo na udugu wa kibinadamu. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anasema, ameguswa na mkutano wa majadiliano ya kidini na kiekumene, uliowajumuisha wanafunzi kutoka vyuo vikuu nchini Thailand. Maisha na utume wa Kanisa nchini Thailand unapambwa na huduma kwa wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anasema, alipata bahati ya kutembelea na kuzungumza na wafanyakazi wa huduma ya afya pamoja na kusalimiana na baadhi ya wagonjwa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, alibahatika kukutana na kuzungumza na wakleri, watawa na makatekista pamoja na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Thailand na huko akaona na kuguswa na sura na sauti ya watu wa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anaendelea kusimulia hija yake nchini Japan kwa kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Japan ambako waliweza kushirikishana changamoto mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa, lakini zaidi umuhimu wa kuwa ni chachu ya Injili ya Kristo Yesu!

Hija hii imeongozwa na kauli mbiu “Linda Maisha yote”. Japan ni nchi ambayo imeathirika kutokana na milipuko ya mabomu ya atomiki na hivyo ni sauti ya watu wanaotafuta haki ya maisha na amani. Akiwa mjini Nagasaki na Hiroshima amepata nafasi ya kukaa kimya na kusali na hatimaye kutoa msimamo wa Kanisa kuhusu utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha za nyuklia. Kuna unafiki mkubwa wa nchi na makampuni mbali mbali kuzungumzia  amani, wakati huo huo yanauza silaha za maangamizi. Baba Mtakatifu anasema amekutana na kuzungumza na wahanga wa tetemeko la ardhi, Tsunami pamoja athari zilizosababishwa na kuvuja kwa mtambo wa nyuklia wa Fukushima. Ili kulinda maisha, kuna haja ya kusimama kidete kuyapenda na kuyatetea na kuyalinda. Ameguswa na ushuhuda wa watakatifu na wafiadini nchini Japan. Amekutana na kuzungumza na vijana. Amesikiliza na kujibu maswali yao msingi na kuwataka kuondokana na ukatili na nyanyaso za kimtandao, daima wakijitahidi kushuhudia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Baba Mtakatifu amewataka vijana wawe ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao; kwa kujenga na kudumisha mahusiano mema kwa njia ya sala na huduma kwa jirani zao. Amekipongeza Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sophia nchini Japan ka huduma na mchango wake kwa watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anasema, amekutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali ya Japan pamoja na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao. Ametumia fursa hii kuwahimiza kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana, sanjari na kuendeleza tunu msingi za maisha ya kiroho na kimaadili, daima wakiwa tayari kupokea ujumbe wa Injili, ili Japan iweze kuwa kweli ni nchi ambayo inasimikwa katika misingi ya haki, amani, maridhiano pamoja na  utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Papa: Barani Asia
27 November 2019, 17:44