Tafuta

Papa Francisko anawaalika vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo! Papa Francisko anawaalika vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo! 

Hija ya Papa Francisko nchini Thailand: Ujumbe kwa vijana wa kizazi kipya!

Vijana wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya furaha kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu amewafikiria, akawatafuta, akawapata na kuwapenda pasi na upeo. Urafiki waliojenga na Kristo ni mafuta yanayohitajika kuwasha moto wa matumaini kwa ajili yao na wale wanaowazunguka. Vijana wasiogope ya mbeleni wala kuzamishwa katika lindi la hofu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 19-23 Novemba 2019 anafanya hija ya kitume nchini Thailand inayoongozwa na kauli mbiu: “Mitume wa Kristo, Wamisionari Mitume”. Hija hii ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 tangu kuanzishwa kwa utume wa Vikarieti ya Siam kunako mwaka 1669. Baba Mtakatifu, Ijumaa tarehe 22 Novemba 2019 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Jimbo kuu la Bangkok, nchini Thailand kwa kuwaalika vijana kuwa tayari kwenda kumlaki Kristo Yesu anayewajia katika maisha yao, huku akiwa amesheheni furaha na upendo, tayari kuwasaidia vijana kupyaisha ulimwengu, kwa kutambua kwamba, ya mbeleni yako mikononi mwao, kwa sababu Mwenyezi Mungu ana mpango mkakati thabiti kwa ajili yao kama ilivyokuwa kwa Taifa teule kwenye Agano la Kale.

Mwenyezi Mungu anawakaribisha kwenye karamu ya maisha na uzima wa milele na kwamba wote wanakaribishwa. Baba Mtakatifu amefanya rejea katika sehemu ya Injili Mt. 25:1-13 kuhusu wale wanawali kumi, kati yao, watano hawakuwa wamejiandaa kikamilifu ili kumpokea Bwana arusi, kwa kukosa mafuta ya akiba, wakaanza kuchoka na kukata tamaa kwa sababu Bwana arusi akikawia kuja! Huu ni mfano wa maisha ya Kikristo, kwani waamini wote wanaitwa kushiriki katika karamu ya maisha na uzima wa milele, huku wakiwa wanashirikiana na kushikamana na wengine. Lakini kuna wakati ambapo, wanakumbwa na matatizo na changamoto za maisha, kiasi cha kujikatia tamaa ya maisha; kiasi kwamba, imani na matumaini vinatoweka kama ndoto ya mchana na hivyo kukosa ile furaha na bashasha ya kumngojea Bwana arusi.

Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana wa Thailand kwamba, wao ni warithi wa historia ya uinjilishaji unaobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu na kwamba, Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ni  kilelezo makini cha urithi wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kutoka kwa Mababu zao waliojisadaka kulijenga ili kuwashirikisha jirani zao huruma na upendo wa Mungu katika maisha na wakatambua kwamba, Kanisa hili ni kielelezo cha uwepo endelevu wa Mungu kati ya waja wake. Baba Mtakatifu anawaka vijana kuzamisha imani yao katika mapokeo ya wazazi na walezi wao pia wawe na ujasiri wa kukabiliana na changamoto mamboleo; wadumifu katika imani nyakati za majaribu, mateso na mahangaiko ya maisha. Hata wazazi na walezi wao, walivumilia shida na mahangaiko mbali mbali, lakini wakawa na furaha, amani na usalama kwa kujiaminisha katika maisha, maneno, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu.

Vijana wanapaswa kuwa na matumaini na imani thabiti kwa kuzamisha matumaini yao kwa Kristo Yesu! Inasikitisha kuwaona vijana wakiwa wametindikiwa matumaini katika maisha na matokeo yake, wanakengeuka, wanatopea na hatimaye kumezwa na malimwengu. Na matokeo yake, wanazimisha maisha kutoka kwa Kristo Yesu, kama “kibatari kilichoishiwa na mafuta”. Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba wao ni kizazi kipya; watu wenye matumaini, ndoto na maswali dekedeke; hofu na mashaka, lakini wanapaswa kusimika maisha yao katika msingi wa Kristo Yesu. Vijana wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya furaha kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu amewafikiria, akawatafuta, akawapata na kuwapenda pasi na upeo. Urafiki waliojenga na Kristo Yesu ni mafuta yanayohitajika kuwasha moto wa matumaini kwa ajili yao na wale wanaowazunguka. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kwenda kumlaki Kristo Yesu kwani anakuja na kamwe wasiogope ya mbeleni wala kukubali kuzamishwa katika lindi la hofu na mashaka! Jambo la msingi ni kutambua kwamba, Kristo Yesu anawasubiri kwa mikono miwili!

Wakati huo huo, Kardinali Francis Xavier Kriengsak Kovithavanij, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Thailand amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kushiriki kikamilifu katika hija ya imani miongoni mwa vijana, ili waweze kutambua kwamba, wao kweli ni leo ya Mungu wanayopaswa kuchangia katika utekelezaji wake. Anamshukuru Baba Mtakatifu kwa Wosia wake wa Kitume Wosia wa kitume kutoka kwa Baba Francisko: “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”, vijana wanakumbushwa kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Anawahimiza vijana kumwilisha ndani mwao Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani kama ushuhuda wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Mara baada ya Misa takatifu, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru wale wote waliojisadaka na kuchangia hata kufanikisha hija yake ya kitume nchini Thailand. Amewashukuru kwa namna ya pekee viongozi wa Serikali, Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wao, lakini zaidi, vijana ambao kweli wameipamba ziara hii kwa uwepo na ushiriki wao mkamilifu. Baba Mtakatifu anawashukuru wale wote waliomsindikiza kwa sala na sadaka zao wakati wote wa hija yake ya kitume nchini Thailand, kwa namna ya pekee, amewakumbuka wafungwa, wagonjwa na wazee. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, awafariji katika mateso na mahangaiko yao, awajalie amani na utulivu. Dhamana kwa vijana kutoka Thailand, ni kuendelea kumkumbuka na kumsindikiza kwa njia ya sala na sadaka zao!

Papa. Vijana
22 November 2019, 17:26