Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Thailand, amewashukuru na kuwapongeza: mapadre, watawa na makatekista wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Thailand, amewashukuru na kuwapongeza: mapadre, watawa na makatekista wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu.  (Vatican Media)

Hija ya Papa Francisko Nchini Thailand: Ujumbe kwa:Mapadre, Watawa na Makatekista

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wakleri, watawa na makatekista kuwa ni watu wa shukrani kwa uzoefu na mang’amuzi ambayo wameshirikishwa jirani zao kuhusu huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Kwa namna ya pekee, wakaguswa na ukarimu, wakajenga mshikamano wa upendo pamoja na kuaminiana. Wakaonja: uvumilivu, huruma na msamaha. Ushuhuda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 19-23 Novemba 2019 anafanya hija ya kitume nchini Thailand inayoongozwa na kauli mbiu: “Mitume wa Kristo, Wamisionari Mitume”. Hija hii ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 tangu kuanzishwa kwa utume wa Vikarieti ya Siam kunako mwaka 1669. Ijumaa, tarehe 22 Novemba 2019, Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na wakleri, watawa, waseminari na makatekista kwenye Parokia ya St. Peter, Jimbo kuu la Bangkok nchini Thailand. Hawa ni watu wanaojivunia utajiri wa maisha na utume wao unaojikita  katika: ukimya, tafakari, unyenyekevu, amani na utulivu; kazi na uwepo wao katika medani mbali mbali za maisha kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu. Askofu Joseph Pradhan Sridarunsil katika salam zake kwa Baba Mtakatifu amesema, watawa ni watu wenye kiu ya ujuzi, elimu na maarifa kwa ajili ya maboresho ya maisha na utume wao kwa watu wa Mungu. Kuna mashirika 35 ya watawa wanawake yenye idadi ya watawa 1,378.

Kuna mashirika ya 22 ya kitawa kwa upande wa wanaume yenye watawa 456. Mashirika ya Kazi za Kitume ni 7 yakiwa na watawa 41, bila kusahau kwamba, kuna mashirika 3 ya watawa wa ndani yenye watawa 164. Mchakato wa uinjilishaji nchini Thailand ulianza kutimua vumbi kunako mwaka 1669 na tangu wakati huo, Kanisa mahalia limeendelea kusoma alama za nyakati, ili kujibu changamoto za uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili. Kanisa limekuwa mstari wa mbele nchini Thailand katika huduma ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya jamii. Watawa wanaendelea kujizatiti katika mapambano dhidi ya biashara ya binadamu na viungo vyake, mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Kanisa Katoliki nchini Thailand limewekeza sana katika maisha na utume wa wanawake, kwa kutambua na kuheshimu mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko amepata bahati ya kusikiliza shuhuda mbali mbali mbali za watawa, walioguswa na Ibada kwa Bikira Maria, wakaamua kujiunga na mashirika ya kitawa ili kuwahudumia jirani zao: wagonjwa, maskini, yatima na wajane.

Wanaomba neema ya kudumu katika wongofu wa ndani, ili kweli waweze kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani zao. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amewashukuru mashuhuda wa maisha na utume wa kitawa nchini Thailand, wanaoendelea kujisadaka kutokana na uaminifu wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Udumifu wao unaendelea kuzaa matunda ya imani, matumaini na mapendo. Amewashukuru na kuwapongeza makatekista na watawa wazee, ambao wamewasaidia watu wa Mungu kujenga urafiki na Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anawataka wakleri, watawa na makatekista kuwa ni watu wa shukrani kwa uzoefu na mang’amuzi ambayo wameshirikishwa na jirani zao kuhusu huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Kwa namna ya pekee, wakaguswa na ukarimu, wakajenga mshikamano wa upendo pamoja na kuaminiana. Wakaonja: uvumilivu, huruma na msamaha. Kwa njia ya shukrani, wanampatia nafasi Roho Mtakatifu kuweza kupyaisha tena maisha na utume wao.

Baba Mtakatifu anawatia shime kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, daima wakijitahidi kuungana na Kristo Yesu katika maisha na utume wao, ili hatimaye, waweze kujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani. Baba Mtakatifu anawataka mapadre, watawa na makatekista kujiweka wazi mbele ya Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaonesha maajabu katika maisha. Kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu ni jambo sahihi na la kweli linaloyajaza maisha kwa mwanga mpya na furaha kuu hata katikati ya matatizo. Hakuna sababu msingi ya kuogopa kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili kwa watu wa Mungu nchini Thailand, ili waweze kumfahamu Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Baba Mtakatifu anasikitika kusikia kwamba, Ukristo kwa watu wengi nchini Thailand ni “eti ni dini ya wageni”, changamoto na mwaliko kwa Wakristo nchini Thailand kuwa kweli ni mashuhuda wa Kristo Yesu na Kanisa lake; kwa kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria; sanjari na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Maombezi ya Bikira Maria, yawasaidie waamini kuguswa na kweli za Kiinjili. Watambue na kukiri uzuri uliomo katika maisha ya kila mwanadamu, tayari kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani. Katika maisha na utume wa Kristo Yesu ndani ya watoza ushuru, wadhambi na wale waliosukumizwa pembezoni mwa jamii aliweza kugundua uzuri wao na kuwasaidia kuwaonesha wengine. Baba Mtakatifu anawahimiza mapadre, watawa na makatekista kuendelea kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa maskini, watu waliokata tamaa na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wawahudumie wote hawa kama ndugu waliokombolewa kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu na kwamba, wao ni ufunuo wa Uso wa Yesu, mwingi wa huruma na mapendo. Mapadre, watawa na makatekista wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huruma inayotenda kazi nchini Thailand.

Baba Mtakatifu anawataka mapadre, watawa na makatekista kuwa ni watu waaminifu kwa maisha ya sala; wawe na Ibada kwa Bikira Maria kwa njia ya Sala ya Rozari Takatifu, lakini zaidi, maisha yao yawe ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa njia ya maneno na matendo yao. Bila maisha ya sala, maisha na utume wao ni bure kabisa kwani utakosa: maana, nguvu na ladha, kikwazo kikubwa cha uinjilishaji. Wajenge utamaduni wa kukutana na Kristo Yesu mara kwa mara katika maisha na utume wao. Watenge muda wa kurejea tena kwenye “Kisima cha maji ya wokovu” ili kupyaisha tena maisha na utume wao. Wajitahidi kutenga muda kwa ajili ya sala, tafakari na maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru wote kwa ushuhuda wa maisha na utume wao kama mapadre, watawa na makatekista.

Papa: Mapadre

 

22 November 2019, 15:46