Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko akutana na kuzungumza na Patriaki Mkuu Somdej Phra Maha Muneewong wa Dini ya Wabudha nchini Thailand. Baba Mtakatifu Francisko akutana na kuzungumza na Patriaki Mkuu Somdej Phra Maha Muneewong wa Dini ya Wabudha nchini Thailand. 

Hija ya Papa Francisko Thailand: Majadiliano ya kidini na Wabudha!

Baba Mtakatifu amemzawadia Patriaki mkuu Somdej Phra Maha Muneewong “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu”. Anasema kuna haja kwa waamini wa dini hizi mbili kushirikiana kwa ajili ya kudumisha udugu wa kibinadamu. Papa anaendelea kusali ili amana na utajiri wa unaofumbatwa katika Mapokeo ya dini hizi mbili, uwasaidie kudumisha haki na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 21 Novemba 2019 amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na Patriaki mkuu Somdej Phra Maha Muneewong wa dini wa Wabudha nchini Thailand kwenye Hekalu la Wat Ratchabophit Sathit Maha Simaram. Viongozi hawa wawili wamezungumzia kuhusu umuhimu wa kudumisha udugu wa kibinadamu ili kukuza amani duniani. Waamini wa dini mbali mbali wakiwa wameungana wanaweza kuwahudumia maskini, watu wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa jamii kwa sababu huduma kwa maskini daima ni kielelezo cha baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Elimu makini, umuhimu wa wamisionari katika kutangaza na kushuhudia imani yao ni muhimu kwa watu wa kizazi hiki. Viongozi wote wawili wamepinga wongofu wa shuruti na kwamba, kuna haja kwa dini hizi mbili kushirikiana kwa karibu zaidi.

Baba Mtakatifu amemzawadia Patriaki mkuu Somdej Phra Maha Muneewong “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu”. Baba Mtakatifu anasema kuna haja ya waamini wa dini hizi mbili kushirikiana kwa ajili ya kudumisha udugu wa kibinadamu. Katika kitabu cha wageni mashuhuri, Baba Mtakatifu ameandika kwamba, anaendelea kusali ili amana na utajiri wa unaofumbatwa katika Mapokeo ya dini hizi mbili, uwasaidie kufahamiana, kukua na hatimaye, waweze kuzaa matunda ya amani kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Thailand. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, amewapongeza waamini wa dini ya Kibudha kwa mchango wao mkubwa kwa ajili ya familia ya Mungu nchini Thailand, kiasi kwamba, wamechota utajiri mkubwa ambao umewawezesha kusimama kidete kulinda maisha dhidi ya utamaduni wa kifo; nidhamu na tafakuri ya kina na bidii ya kazi mambo yanayowafanya kuwa ni watu wa “kawaida.”.

Miaka 50 imekwisha kuyoyoma tangu Mtakatifu Paulo VI alipokutana kwa mara ya kwanza ya kikundi cha waamini wa dini ya Kibudha, majadiliano ambayo yaliendelezwa pia na Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea nchini Thailand kunako mwaka 1984. Tarehe 16 Mei 2018, Baba Mtakatifu Francisko alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wajumbe wa dini ya Kibudha kutoka Thailand. Zote hizi ni juhudi za ujenzi wa jamii jumuishi, kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu, ili kweli dini sehemu mbali mbali za dunia ziweze kuwa ni nguzo ya matumaini na kikolezo cha mchakato wa ujenzi wa udugu. Baba Mtakatifu anaipongeza Thailand kwa kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini; kwa kuheshimiana na kuthaminiana na ndugu zao waamini wa dini ya Kibudha.

Waamini wa dini hizi mbili ni watu ambao wana aminiana na wanajisikia kuwa ni ndugu wamoja licha ya tofauti zao msingi. Kanisa Katoliki litaendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini kwa ajili ya huduma ya amani, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu nchini Thailand. Kanisa linapania kuanzisha miradi ya pamoja kwa ajili ya huduma kwa maskini ili kukuza udugu wa kibinadamu pamoja na kusaidia ujenzi wa utamaduni wa huruma, udugu na watu kukutana, ili kwa njia ya ushirikiano huu waweze kuzaa matunda mengi.

Papa: Wabudha
21 November 2019, 15:44