Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini nchini Thailand kuwa mitume wamisionari, tayari kusoma alama za nyakati ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini nchini Thailand kuwa mitume wamisionari, tayari kusoma alama za nyakati ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! 

Hija ya Papa Francisko Thailand: Mahubiri Ibada ya Misa Takatifu

Utume huu ni chemchemi ya shukrani na furaha isiyokuwa na kikomo kwa kumruhusu Mwenyezi Mungu awapeleke mbali na upeo wao wenyewe, ili hatimaye, kuufikia ukweli mkamilifu wa asili ya binadamu, chanzo na kilele cha uinjilishaji ni kuwashirikisha wengine huruma na upendo wa Mungu. Imegota miaka 350 yaani tangu mwaka 1669-2019 tangu kuundwa kwa Vikarieti ya Siam.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 21 Novemba 2019 wakati wa hija yake ya kitume nchini Thailand ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Uwanja wa Taifa wa Bangkok nchini Thailand; Siku kuu ya Bikira Maria Kutolewa Hekaluni, sanjari na Maadhimisho ya Siku ya Watawa wa Ndani. Waamini wanakumbushwa kwamba, Kanisa ni nyumba ya Sala na Ibada, mahali ambapo Mafumbo matakatifu yanaadhimishwa, ili kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amekazia mawazo makuu matatu: ukweli, safari na maisha mambo yanayofafanua kwa kina lile swali msingi, Je, Mama yangu ni nani? Na ndugu zangi ni akina nani? Yesu anajibu akiwaambia wasikilizaji wake kwamba, Mama na ndugu zake ni wale wote wanaofanya mapenzi ya Baba yake wa mbinguni. Baba Mtakatifu anasema, Injili ni mwaliko na haki ya kusikiliza kile ambacho mwamini anataka kusikiliza, yaani ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu daima ni kijana na chanzo endelevu cha upya kinachopyaisha maisha na utume wa Kanisa; kwa kubomoa matabaka na kuendelea kuwastaajibisha watu wa Mungu kwa ubunifu wake wa kimungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema kila aina ya uinjilishaji halisi daima unakuwa mpya. Haya ndiyo yaliyowakumba wamisionari waliofika nchini Thailand kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kwa kusikiliza Neno la Mungu, kwa njia ya nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, wakajaliwa kupata mwamko mpya wa matumaini na kutoka kuanza safari ya kutafuta nyuso mpya! Kulikuwa na umuhimu wa kufungua kurasa mpya, ili kuwajalia watu kushiriki Neno la Mungu, ili kukua katika imani na kuyaelewa Maandiko Matakatifu. Bila ya wamisionari kufunga safari ya kukutana na watu wa Mataifa, Ukristo ungekosa sura, tamaduni na furaha ya watu wa Mungu kutoka Thailand. Wamisionari walisoma alama za nyakati, wakawa tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Wao ni wamisionari mitume wanaotambua mahitaji msingi ya watu wao, ili kuweza kuadhimisha upatanisho ambao Kristo Yesu anawakirimia waja wake, ili hatimaye, waweze kushiriki kwenye karamu yake ya milele.

Utume huu ni chemchemi ya shukrani na furaha isiyokuwa na kikomo kwa kumruhusu Mwenyezi Mungu awapeleke mbali na upeo wao wenyewe, ili hatimaye, kuufikia ukweli mkamilifu wa asili ya binadamu, chanzo na kilele cha uinjilishaji ni kuwashirikisha wengine huruma na upendo wa Mungu. Baba Mtakatifu anasema, imegota miaka 350 yaani tangu mwaka 1669-2019 tangu kuundwa kwa Vikarieti ya Siam. Hizi ni juhudi za wamisionari wawili waliokuwa na ujasiri wa ajabu kabisa, wakathubutu kupandikiza mbegu ya Ukristo na leo hii matunda yake yanaonekana kwa kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Thailand. Kumbu kumbu hii ni moto wa matumaini, nguvu na imani mpya, chemchemi ya furaha na shukrani, tayari kwa waamini kutoka kifua mbele ili kuwashirikisha watu wa Mataifa upya wa maisha unaobubujika kutoka katika Injili. Kila mwamini ni mtume mmisionari, ikiwa kama ataamua kuwa ni sehemu hai ya familia ya Mungu, kwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kristo Yesu, aliyeketi pamoja na wadhambi, akawagusa kutoka katika undani wa maisha yao; wakaonja ukaribu wa Mungu katika maisha yao na kutambua kwamba, kwa hakika walikuwa wamebarikiwa!

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amesikitishwa sana na watoto, wasichana na wanawake wanaotumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo; mambo yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni tabia inayofutilia mbali ndoto za watu; wakimbizi na wahamiaji wanalazimika kuzitelekeza familia zao. Kuna watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, wanajisikia kutelekezwa na jamii, kiasi hata cha kukosa nguvu, mwanga na faraja na urafiki kutoka kwa Kristo Yesu, wala Jumuiya ya waamini inayoweza kuwakaribisha na kuwakirimu, kwani wamekuwa ni watu wasioona tena maana ya maisha. Baba Mtakatifu anawakumbuka pia wavuvi wanaonyanyasika kutokana na kazi zao pamoja na wale wote wasioonekana. Lakini wote hawa ni sehemu ya familia ya Mungu, ambao wana madonda makubwa katika maisha na wanahitaji mafuta ya faraja na divai ya matumaini, huruma na upendo wa Mungu.

Mmisionari mtume anatambua kwamba, uinjilishaji dhamana na utume wake ni kuwakunjulia watu mikono ya Mungu yenye huruma na uponyaji, inayowafanya kuwa ni familia moja. Baba Mtakatifu anawaalika waamini nchini Thailand kufuata nyayo za wamisionari wa kwanza, ili kukutana na jirani zao ili hatimaye kung’amua na kugundua furaha ya maisha na karamu ya uzima wa milele!

Papa: Misa Thailand
21 November 2019, 17:36