Tafuta

Papa Francisko atuma salam za rambi rambi nchini Albania kutoka na maafa makubwa yaliyosababishwa na tetemeko la rdhi na hivyo kupelekea watu wengi kupoteza maisha na miundo mbinu kuharibika. Papa Francisko atuma salam za rambi rambi nchini Albania kutoka na maafa makubwa yaliyosababishwa na tetemeko la rdhi na hivyo kupelekea watu wengi kupoteza maisha na miundo mbinu kuharibika. 

Papa Francisko asikitikishwa na maafa yaliyotokea nchini Albania

Papa Francisko amewakumbuka na kuwaombea watu wa Mungu nchini Albania ambao wameathirika kutokana na tetemeko la ardhi ambalo limeukumba mji wa Durazzo na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Itakumbukwa kuwa Albania ni nchi ya kwanza kuitembelea Barani Ulaya baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi yake kwa mahujaji na wageni waliofika mjini Vatican, Jumatano tarehe 27 Novemba 2019, amewakumbuka na kuwaombea watu wa Mungu nchini Albania ambao wameathirika vibaya sana kutokana na tetemeko la ardhi ambalo limeukumba mji wa Durazzo na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Albania ni nchi ya kwanza kuitembelea Barani Ulaya baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia watu wa Mungu nchini Albania, uwepo wake wa karibu, hasa kwa wale walioguswa na kutikiswa na janga hili asilia.

Papa Francisko anawaombea wale waliofariki dunia, waweze kupata pumziko la milele na majeruhi kupona na kurejea tena kwenye shughuli zao za kawaida! Baba Mtakatifu katika salam za rambi rambi zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Rais Ilir Meta wa Albania, anasema, amesikitishwa na kuguswa sana na maafa makubwa yaliyowakumba watu wa Mungu nchini Albania. Anapenda kumhakikishia uwepo wake wa karibu kwa wananchi wa Albania kwa njia ya sala. Anapenda kutumia fursa hii kuwatia shime wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu ambao bado wamefukiwa na vifusi. Wote hawa, amewapatia baraka zake za kitume!

Papa: Albania
27 November 2019, 17:07