Papa Francisko anakazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo kwa kutoa kipaumbele kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Papa Francisko anakazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo kwa kutoa kipaumbele kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. 

Hija ya Papa Francisko Thailand: Hotuba kwa viongozi wa Thailand

Baba Mtakatifu amekazia: umoja na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa; changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; Kumbu kumbu ya Miaka 30 ya Tamko la Haki ya Mtoto Duniani; Ukarimu kama kichocheo cha maendeleo fungamani ya binadamu. Papa amewashukuru wale wote waliochakarika ili kufanikisha hija yake ya kitume nchini Thailand ili kukuza kifungo cha urafiki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 19-23 Novemba 2019 anafanya hija ya 32 ya kitume nchini Thailand inayoongozwa na kauli mbiu: “Mitume wa Kristo, Wamisionari Mitume”. Hija hii ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 tangu kuanzishwa kwa utume wa Vikarieti ya Siam kunako mwaka 1669. Alhamisi, tarehe 21 Novemba 2019, Baba amekutana na kuzungumza na Jenerali Prayuth Chan Ocha, Waziri mkuu wa Thailand, baadaye ametoa hotuba kwa viongozi wa Serikali na kisiasa; wanadiplomasia, viongozi wa kidini pamoja na viongozi wa vyama vya kiraia nchini Thailand. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia: umoja na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa; changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; Kumbu kumbu ya Miaka 30 ya Tamko la Haki ya Mtoto Duniani; Ukarimu kama kichocheo cha maendeleo fungamani ya binadamu.

Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wale wote waliochakarika usiku na mchana ili kufanikisha hija yake ya kitume nchini Thailand ili kukuza kifungo cha urafiki kati ya watu wa Mataifa. Amewapongeza viongozi waliochaguliwa nchini Thailand kuwa ni mwendelezo wa mchakato wa demokrasia. Changamoto mamboleo zinazoendelea kuikumba familia ya binadamu zinahitaji kujibikiwa kwa kudumisha haki ya kimataifa na mshikamano kati ya watu. Baba Mtakatifu ameipongeza Thailand inapokaribia kumaliza kipindi chake cha uenyekiti wa ASEAN “Association of Southeast Asian Nations” yaani “Shirikisho la Nchi Zilizoko Kusini Mashariki mwa Asia” kielelezo kwamba, Thailand imekuwa ikijishughulisha na  masuala mapana sanjari na changamoto zinazowakumba wananchi waliko Kusini Mashariki mwa Bara la Asia, ili kujenga na kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni.

Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa ujenzi wa umoja, mshikamano wa kitaifa, amani na utulivu nchini Thailand; kwa kutambua tofauti zao msingi na hivyo kuheshimiana. Mwelekeo wa utandawazi katika ulimwengu mamboleo ni kutaka kufutilia mbali tofauti za watu kwa misingi ya faida ya kiuchumi; lakini umoja katika tofauti ni muhimu katika ujenzi wa matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, urithi mkubwa kwa siku za mbeleni. Baba Mtakatifu amepongeza jitihada za Thailand za kuunda Tume ya Maadili Kitaifa inayowashirikisha pia viongozi wa dini mbali mbali, ili kuweza kuchangia amana na urithi wa maisha ya kiroho. Kumbe, kuna haja ya kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga jamii jumuishi. Kanisa Katoliki litaendelea kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Thailand kwa kukuza amani na upendo bila woga wowote ule.

Kanisa litaendelea kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema katika mchakato unaopania kuwakomboa watu kutoka katika umaskini, vita na ukosefu wa haki, kwa kutambua kwamba, uhuru wa kweli unawajibisha ili hatimaye kuweza kujenga misingi ya usawa; kwa kuhakikisha kwamba, watu wengi zaidi wanapata huduma ya elimu na afya, fursa za ajira zitakazowezesha kujipatia kipato kwa ajili ya maendeleo fungamani ya binadamu. Wimbi kubwa la wakimbizi ni changamoto kubwa ya kimaadili katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu anaipongeza Thailand kwa kutoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka katika nchi jirani. Kanisa linakazia umuhimu wa: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha wakimbizi na wahamiaji kama kielelezo cha umoja na mshikamano wa kidugu na huduma ya upendo kwa maskini. Utu, heshima na haki zao msingi zikizingatiwa sanjari na kupatiwa maisha yenye hadhi ya kibinadamu, utambulisho makini wa jamii inayowajibika

Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya Kimataifa kwa Mwaka 2019 inaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 30 ya Tamko la Haki ya Mtoto Duniani, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza haki msingi za watoto; utu na heshima yao kama binadamu. Watoto wajengewe mazingira mazuri ya maisha, kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao kiroho, kimwili, kisaikolojia na kiakili. Matumaini ya kesho iliyo bora zaidi yanafumbatwa kwa namna ya pekee katika huduma kwa watoto. Baba Mtakatifu anaipongeza Serikali ya Thailand inayoendelea kupambana na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo inayodhalilisha na kunyanyasa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, leo hii jamii inawahitaji wajenzi wa ukarimu, watu wanaoweza kujisadaka kwa ajili ya kukoleza mchakato wa maendeleo fungamani katika familia ya binadamu kwa kuzama zaidi katika misingi ya haki, mshikamano, udugu wa kibinadamu na utulivu. Kila mmoja anapaswa kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu amewatakia viongozi na wananchi wote wa Thailand hekima, haki na amani!

Papa: Diplomasia
21 November 2019, 16:47