Papa Francisko asema inawezekana kabisa kwa dunia bila ya kuwa na silaha za kinyuklia na kwamba silaha za mangamizi haziwezi kutatua changamoto za ulinzi na usalama kitaifa na kimataifa. Papa Francisko asema inawezekana kabisa kwa dunia bila ya kuwa na silaha za kinyuklia na kwamba silaha za mangamizi haziwezi kutatua changamoto za ulinzi na usalama kitaifa na kimataifa. 

Hija ya Papa Francisko nchini Japan: Hatari ya Silaha za Nyuklia

Papa amezungumzia: Mateso na maafa makubwa yaliyosababishwa na mashambulizi ya mabomu ya atomiki; Umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kudumisha misingi ya: usalama, amani na utulivu kwa kuondokana na wasi wasi inayotawala akilini na mioyoni mwa watu kiasi cha kushindwa kuaminiana na hivyo, kudhohofisha mafungamano ya watu pamoja na mchakato wa majadiliano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa Katoliki nchini Japan, mwaka 2019 linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 470 tangu alipowasili nchini humo, Mtakatifu Francisko Xavier pamoja na wenzake na huo ukawa ni mwanzo wa kuenea kwa Ukristo nchini Japan. Kunako mwaka 1614 madhulumu dhidi ya Wakristo yakafumuka na kupamba moto kwa takribani miaka 260 na waamini wengi wakauwawa kikatili kwa ajili ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Katika kipindi cha madhulumu, Wakristo waliokuwa wanaishi kwenye Mkoa wa Nagasaki waliendelea kupyaisha imani yao na kufanikiwa kuwarithisha wengine amana na utajiri huu kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji, sala na katekesi ya kina. Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Japan kuanzia tarehe 23 hadi 26 Novemba 2019 inaongozwa na kauli mbiu “Linda Maisha Yote”. Huu ni ujumbe unaowataka watu wa Mungu nchini Japan kusimama kidete kulinda: utu, haki na heshima ya binadamu dhidi ya vitisho vinavyohatarisha misingi ya amani na utulivu na hasa zaidi mapambano ya silaha za maangamizi.

Baba Mtakatifu, Jumapili, tarehe 24 Novemba 2019 amezungumzia kuhusu mateso na maafa makubwa yaliyosababishwa na mashambulizi ya mabomu ya atomiki, changamoto na mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya: usalama, amani na utulivu kwa kuondokana na wasi wasi pamoja na hofu inayotawala akilini na mioyoni mwa watu kiasi cha kushindwa kuaminiana na hivyo kudhohofisha mafungamano ya watu pamoja na mchakato wa majadiliano. Amani na utulivu wa kimataifa vinaweza kujengeka katika msingi wa mshikamano na ushirikiano wa haki kwa ajili ya huduma kwa kutambua kwamba, watu wanategemeana na wanapaswa kuwajibika kama wamoja kwa ajili ya ustawi wa familia nzima ya binadamu. Baba Mtakatifu anasema, Nagasaki ni mji ambao umeshuhudia maafa makubwa kwa binadamu sanjari na uharibifu wa mazingira; kielelezo cha mashindano ya utengenezaji wa silaha za maangamizi; upotevu mkubwa wa rasilimali fedha ambayo ingeweza kutumika kuchochea maendeleo fungamani ya binadamu pamoja na utunzaji bora wa mazingira.

Rasilimali fedha inayotumika kwa ajili ya kutengeneza, kuboresha na kuhifadhi na hatimaye, kuuza silaha za maangamizi, nyuma yake kuna kilio cha watoto na familia nyingi duniani. Watu wanatamani amani ya kudumu ili kuondokana na vitisho vya silaha za maangamizi na kwamba, hii ni changamoto inayowahusisha watu wote; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kuaminiana na wala si katika tabia ya kupimana nguvu. Kuna haja ya kudhibiti biashara ya silaha kimataifa na maendeleo makubwa ya teknolojia kuhusu masuala ya kijeshi. Hii ni dharura inayohitaji kushughulikiwa na viongozi wote wa Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa Katoliki kwa upande wake, litaendelea kuhimiza umuhimu wa watu wa Mataifa kudumisha amani. Kanisa linaunga mkono Kanuni ya Sheria ya Kimataifa kuhusu Silaha za Nyuklia, ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa kupiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za kinyuklia duniani. Amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo!

Amani inatishiwa sana na mashindano ya silaha; utengenezaji na biashara ya silaha pamoja na mchakato wa ulimbikizaji wa silaha duniani! Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani ambalo ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu! Baraza la Maaskofu Katoliki Japan katika ujumbe wake wa Siku 10 za kuombea Amani Duniani, kwa mwaka 2019 linasema: amani ya kweli ni matunda ya maendeleo fungamani ya binadamu. Kunako mwaka 1981, Mtakatifu Yohane Paulo II aliwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema: kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani huko Hiroshima, nchini Japani. Tangu wakati huo, familia ya Mungu nchini Japan kuanzia tarehe 6 hadi 15 Agosti ya kila mwaka imekuwa ikisali kwa ajili ya kuombea amani duniani. Baba Mtakatifu anakaza kusema sala ni silaha nzito kwa ajili ya kusaidia mchakato wa majadiliano kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu ili aweze kusaidia kuenzi ujenzi wa dunia inayosimikwa katika haki na mshikamano kama kielelezo cha amani ya kudumu.

Baba Mtakatifu anasema, dunia bila kuwa na silaha za kinyuklia inawezekana kabisa na ni muhimu sana na kwamba, silaha hizi za maangamizi kamwe haziwezi kuwasaidia viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na uhakika wa usalama wa raia na mali zao kitaifa na kimataifa. Kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu madhara yake katika maisha ya watu sanjari na mazingira; kwa kuondoa hofu, mazingira ya kutoaminiana, chuki na uhasama vinavyozungumza “dhana ya silaha za nyuklia”. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujielekeza zaidi katika kubuni sera na mikakati itakayosaidia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Kunako mwaka 1964, Mtakatifu Paulo VI alishauri kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo kwa Nchi Maskini, ambao ungechangiwa kwa kuchukua sehemu ya bajeti ya serikali mbali mbali kwa ajili ya matumizi ya kijeshi. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutengeneza mazingira ya kuaminiana, kwa sababu hii ni changamoto pevu kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Umefika wakati wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kwa kujenga na kuimarisha utamaduni wa majadiliano; toba na wongofu wa ndani, ili utamaduni wa uhai, upatanisho na udugu viweze kutawala katika akili na nyoyo za watu. Baba Mtakatifu Francisko baada ya hotuba yake, amewaomba waamini wa dini mbali mbali kuungana pamoja naye kwa ajili ya kusali ile sala ya Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa ajili ya kuombea amani duniani: Ee Bwana unifanye kuwa chombo cha amani. Palipo chuki nieneze upendo. Palipo na mashaka pawe na imani. Palipo na tumaini pawe na matumaini. Palipo na giza pawe na mwanga. Palipo na huzuni pawe na furaha. Ee Bwana Mungu,unijalie; Nisitafute kufarijiwa bali kufariji Nisitafute kupendwa bali kupenda. Kwani ni katika kutoa ndipo tunapopokea Ni kwa kusamehe ndipo tunaposamehewa. Na ni kwa kufa ndipo tunazaliwa katika uzima wa milele, AMINA.  Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kuongoka na kujiaminisha mbele yake, ili aweze kuwageuza kuwa ni vyombo vya amani na hiyo kutorudia tena kwenye makosa ya zamani.

Papa: Nyuklia
24 November 2019, 14:04