Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika viongozi wa Kanisa kuwasikiliza na kuwasindikiza vijana katika hija ya maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika viongozi wa Kanisa kuwasikiliza na kuwasindikiza vijana katika hija ya maisha yao. 

Papa: Viongozi wa Kanisa wasikilizeni na kuwasindikiza vijana!

Kanisa halina budi kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, linasikiliza na kujibu matamanio halali ya vijana. Waguswe na maoni ya vijana wanapowaonesha mafanikio katika maisha na utume wa Kanisa; wayafanyie kazi mapungufu ya viongozi wa Kanisa yanayonyooshewa kidole na vijana. Kanisa liwe tayari kusoma alama za nyakati, kwa kuwasaidia vijana kukomaa zaidi katika maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Viongozi wa utume wa vijana ndani ya Kanisa wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Kanisa halina budi kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, linasikiliza na kujibu matamanio halali ya vijana. Waguswe na maoni ya vijana wanapowaonesha mafanikio katika maisha na utume wa Kanisa; wayafanyie kazi mapungufu ya viongozi wa Kanisa yanayonyooshewa kidole na vijana. Kanisa liwe tayari kusoma alama za nyakati, kwa kuwasaidia vijana kukua na kukomaa katika maisha yao, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Vijana ni ardhi takatifu, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Jumuiya ya Kikristo.

Viongozi wa utume wa vijana wanahimizwa kuwasindikiza vijana hawa katika hija ya maisha yao, kwa heshima na upole, ili waweze kukua na kukomaa katika imani kwa njia ya neema inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili hatimaye, waweze kuzaa matunda ya upendo na matumaini kwa kutambua kwamba, Amerika ya Kusini ni Bara lenye matumaini, kama ilivyo leo ya Mungu kwa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kristo Yesu, ameonesha ule utashi, wema na huruma yake kwa kutaka kuambatana na kuendelea kubaki akiwa ameshikamana na vijana wa kizazi kipya katika lugha ya upendo. Vijana wajengewe uwezo wa kusimama tena baada ya kuanguka; wawe na ari na moyo wa kutumia kila fursa mpya kuweza kujipatanisha na yaliyopita, ili kujenga ya mbeleni kwa matumaini zaidi.

Hii ni sehemu ya ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko aliowaandikia viongozi wa utume wa vijana, wanaokutana mjini Lima, nchini Perù kuanzia tarehe 18-23 Novemba 2019 ili kuhudhuria mkutano wa XX wa Amerika ya Kusini unaoongozwa na kauli mbiu “Sisi vijana ni ardhi takatifu na leo ya Mungu”. Baba Mtakatifu anawataka viongozi hawa wawasaidie vijana kumfahamu Kristo Yesu, ili waweze kujenga mahusiano na mafungamano ya ndani na hatimaye, wageuke na kuwa ni wafuasi wamisionari na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Vijana wawe na jeuri ya kumkaribia Kristo Yesu, ambaye daima ni kijana, ili waonje furaha ya urafiki wao inayokita mizizi yake katika udugu wa kibinadamu na mshikamano wa Kikristo.

Akiwa na mawazo haya, Baba Mtakatifu Francisko anawaombea washiriki wote na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Guadalupe, Msimamizi wa Amerika ya Kusini, ili aweze kuwaombea viongozi wa utume wa vijana pamoja na vijana wenyewe kutoka Amerika ya Kusini, ili waweze kuimarika katika upendo, kwa kuwasindikiza katika safari ya maisha yao ya kila siku. Mkutano huu unahudhuriwa na wajumbe kutoka Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean, CELAM. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”, matunda ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa Mwaka 2018, yaliyoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Mang’amuzi na Miito” anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Kumbe, wajumbe wanaendelea kutafakari kuhusu Wosia huu wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”.[ Audio Embed Vijana: CELAM]

 

20 November 2019, 15:32