Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana nchini Vietnam kuwa ni mashuhuda wa uaminifu, uwajibikaji na watu wenye matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana nchini Vietnam kuwa ni mashuhuda wa uaminifu, uwajibikaji na watu wenye matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. 

Papa Francisko: Ujumbe kwa Siku ya Vijana Kitaifa Vietnam 2019

Vijana nchini Vietnam wametakiwa kuendeleza urithi walioachiwa na mashuhuda wa imani, waliyoyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu. Huu ni ushuhuda unaofumbatwa katika: uaminifu, uwajibikaji pamoja na matumaini. Kanisa linawakumbuka na kuwaombea wahamiaji na wakimbizi 39 kutoka Vietnam waliokufa kwa njaa na kiu baada ya kufungiwa kwenye Container.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Vietnam, Jumatano tarehe 20 Novemba 2019 linaadhimisha Siku ya Vijana kwa Majimbo ya Kaskazini mwa Vietnam kwa kuongozwa na kauli mbiu “Enenda zako nyumbani kwako, kwa watu wa kwenu” Mk. 5:19. Hii ni changamoto kwa vijana wa kizazi kipya nchini Vietnam kuendeleza urithi, amana na utajiri walioachiwa na mashuhuda wa imani, waliyoyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu. Huu ni ushuhuda unaofumbatwa katika: uaminifu, uwajibikaji pamoja na matumaini. Kanisa linawakumbuka na kuwaombea wahamiaji na wakimbizi 39 kutoka Vietnam waliokufa kwa njaa na kiu nchini Uingereza baada ya kufungiwa kwenye Container na kusafirishwa kama mizigo, ukatili unaoshuhudiwa kwenye biashara haramu ya binadamu na viungo vyake.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa video kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Vijana kwa Majimbo ya Kaskazini mwa Vietnam. Kadiri ya tamaduni na mapokeo ya Vietnam, nyumba inapewa umuhimu wa pekee, kwani hapa ni kitovu cha maisha ya mtu yaani familia, mahali alipozaliwa na nchi ambayo inampatia hifadhi. Ni mahali pa kukuza na kujenga upendo kwa majirani; heshima na utii kwa wazazi na watu wazima pamoja na kuwatunza wazee. Kauli mbiu ya maadhimisho haya inawataka vijana kurejea tena katika asili na chimbuko la maisha yao; ili kugundua tena amana, utajiri na tamaduni za watu wao; mambo yanayopaswa kuhifadhiwa kama mboni ya jicho! Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wamepata nyumba kubwa zaidi ambayo ni Kanisa, wametungwa mimba na kuzaliwa kwenye Kanisa lenye utajiri mkubwa wa shuhuda angavu kutoka kwa mashahidi, wafiadini, wazazi na walei wao.

Nyumbani ni mahali ambapo wanaweza kurejea na kujichotea tena misingi ya imani, kwa kuunda dhamiri nyofu na utu wema na kwa njia hii, wataweza kugundua ndani mwao wito wao wa pili kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anawakumbuka wamisionari waliojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu nchini Vietnam, changamoto na mwaliko wa kukoleza upendo kwa Mungu na jirani, ili kukuza ari na mwamko wa kimisionari. Baba Mtakatifu anawataka vijana warejee nyumbani kwao na kwa watu wao ili kuwatangazia matendo makuu ambayo Mwenyezi Mungu amewatendea katika maisha, tayari kushiriki katika ujenzi wa Kanisa, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko bila kufanya wongofu wa shuruti. Baba Mtakatifu anawaonya kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu, wawe na uwezo wa kufanya mang’amuzi; kwa kuwa ni waaminifu na wawajibikaji; mambo yanayohitaji sadaka, kwani kuna watu wametopea katika rushwa na ufisadi wa mali ya umma.

Baba Mtakatifu anawataka vijana wa Vietnam kung’ara kama "nyota ya asubuhi", ili kushuhudia tunu msingi na utambulisho wa Kikatoliki. Vijana wawe wazalendo na waipende nchi yao; wajitahidi kukabiliana na changamoto mamboleo kwa njia ya kipaji cha ugunduzi. Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, Mtumishi wa Mungu Kardinali Van Thuan ni shuhuda amini wa matumaini. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, maadhimisho haya yatakuwa ni changamoto ya kuwawezesha kuzamisha mizizi yao katika tamaduni na maisha ya kiroho, ili kuimarisha imani, ari na mwamko mpya wa kimisionari; kwa kuzipenda familia pamoja na nchi yao.

Papa: Vietnam

 

20 November 2019, 16:01