Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume "Gaudete et exsultate", Sura ya Pili anabainisha vikwazo vya mchakato wa utakatifu wa maisha. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume "Gaudete et exsultate", Sura ya Pili anabainisha vikwazo vya mchakato wa utakatifu wa maisha. 

Papa Francisko: Vikwazo vya mchakato wa utakatifu wa maisha!

Maadui wa imani: Mitindo potofu ya utakatifu wa maisha unaoelea katika ombwe; akili bila ya kumtegemea Mungu. Hawa ni watu wanaomtafuta Mungu bila ya Yesu; wanaomtaka Kristo bila Kanisa, au kulipenda Kanisa bila watoto wake! Haya ni mawazo yanayoendelea kusumbua vichwa vya watu wa nyakati hizi. Ni watu wanaotaka mafundisho ambayo kamwe hayana Fumbo ndani mwake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12)anasema, Kristo Yesu anawaalika wote wanaoteseka au kudhulumiwa kwa ajili yake, kufurahi na kushangilia, kwani yeye ni chemchemi ya maisha na furaha ya kweli. Anataka waja wake kuwa kweli ni wakamilifu na watakatifu, mwaliko na changamoto inayojionesha katika sehemu mbali mbali za Maandiko Matakatifu. Wosia huu wa kitume umegawanyika katika sura kuu tano: Sura ya kwanza ni Wito wa utakatifu; Sura ya Pili ni Adui wa utakatifu; Sura ya tatu: Mwanga katika maisha ya Mwalimu, Sura ya nne: Alama za Utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo na Sura ya tano: Mapambano ya maisha ya kiroho; kukesha na kufanya mang’amuzi! Kama sehemu ya mapambano kuelekea utakatifu wa maisha, leo Radio Vatican inapenda kukushirikisha kuhusu maadui wa utakatifu wa maisha.

Baba Mtakatifu Francisko katika sura ya pili anagusia: Maadui wa imani:  Mitindo potofu ya utakatifu wa maisha unaoelea katika ombwe; akili bila ya kumtegemea Mungu wala kumwilishwa katika uhalisia wa maisha. Hawa ndio wale watu wanaomtafuta Mungu bila ya Kristo Yesu; wanaomtaka Kristo Yesu bila Kanisa, au kulipenda Kanisa bila watoto wake! Haya ni mawazo yanayoendelea kusumbua vichwa vya watu wa nyakati hizi. Ni watu wanaotaka mafundisho ambayo kamwe hayana Fumbo ndani mwake, kwani wanayo majibu ya maswali yote yanayomtatiza mwanadamu! Hawa ni watu wanaodhani kwamba, wanaweza kumweka Mwenyezi Mungu “mfukoni mwao” na kumtumia kama wanavyotaka! Waamini wanapaswa kutambua kwamba, uwezo wa mwanadamu kufikiri una ukomo wake! Hawawezi kuhalalisha kweli za Kiinjili ili kukidhi matakwa yao binafsi na kwamba, Mafundisho tanzu ya Kanisa yanaendelea kufafanuliwa daima katika maisha na kwamba, taalimungu na utakatifu wa maisha ni mambo yasiyopingana wala kusigana!

Hekima na busara ya Kikristo inafumbatwa pia katika huruma na upendo kwa jirani! Waamini waendelee kupambana na maadui wa utakatifu wa maisha kwa kwa kujikita katika Ibada ya kweli inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Baba Mtakatifu anasema, hata leo hii bado kuna wazushi na wakanimungu kwani wanadhani kwamba, kila jambo linategemea utashi wa binadamu na kusahau huruma na upendo wa Mungu, ambaye aliwapenda binadamu kwanza! Hawa ni watu wanaoshindwa kutambua karama, mchango na nafasi ya kila mwamini katika maisha na utume wa Kanisa. Hakuna mtu aliyebarikiwa kufanya yote kwa ukamilifu, bali watu wanategemeana na kukamilishana katika unyenyekevu! Watu wakiri na kutambua: karama, uwezo na mapungufu yao katika maisha kwani neema inajikita katika asili ya binadamu! Mama Kanisa anaendelea kufundisha kwamba, watu wanahesabiwa haki si kwa matendo yao bali kwa njia ya neema inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu!

Lakini ikiwa ni kwa neema, haiwi kwa matendo tena, au hapo neema isingekuwa neema. (Rej. Rum. 11:6). Wito huu wa uzima wa milele ni wa Kimungu. Wote kabisa twategemea kazi ya Mungu, kwani Yeye peke yake anajifunua na anajitoa mwenyewe; Wapita maweza ya akili na nguvu za utashi wa kibinadamu! (Rej. KKK. Namba 1999). Watakatifu walijitahidi kutenda haki mbele ya Mungu na jirani zao, wakamwilisha upendo huo katika uhalisia  na vipaumbele vya maisha yao! Wazushi mamboleo na wakanimungu wanaendelea kujionesha kwa kujikita katika Sheria kanuni za Kanisa, Liturujia na Mafundisho Tanzu ya Kanisa, kwa ajili ya kutaka kujikweza, “kujimwambafai” pamoja na kujitafutia umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko! Badala ya kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu katika unyenyekevu na upendo, ili hatimaye, kuwa ni vyombo na mashuhuda wa uzuri na furaha ya Injili, ili kuzima kiu na matamanio halali ya watu wa Mataifa! Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna itifaki ya karama na tunu msingi zinazowaunganisha waamini ili kuambata mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa. Tunu hizi ni: imani na upendo. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuzitafakari tunu hizi na kufanya mang’amuzi mbele ya Mwenyezi Mungu.

Vikwazo vya Utakatifu

 

31 October 2019, 11:39