Papa Francisko amewashukuru na kuwapongeza wale wote waliojisadaka kwa ajili ya kudhuria Ibada ya Misa Takatifu ya kuwatangaza watakatifu wapya Oktoba 2019. Papa Francisko amewashukuru na kuwapongeza wale wote waliojisadaka kwa ajili ya kudhuria Ibada ya Misa Takatifu ya kuwatangaza watakatifu wapya Oktoba 2019. 

Watakatifu Wapya 2019: Shukrani za Baba Mtakatifu Francisko!

Papa amewashukuru wageni kutoka ndani na nje ya Italia, hasa zaidi wageni kutoka Uingereza kwa ushuhuda wao wa Kiinjili, kwa Watakatifu wapya ambao wamechangia ukuaji wa maisha ya kiroho na kijamii katika nchi zao asilia. Baba Mtakatifu amechukua fursa hii kumkaribisha Askofu Ian Ernest ambaye ameteuliwa hivi karibuni kuwa Mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Kanisa Anglikani, Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu na kuwatangaza watakatifu wapya watano, ameyaelekeza mawazo yake katika shukrani, mahangaiko na mateso ya watu wa Mungu Mashariki ya Kati pamoja na hali tete ya kisiasa nchini Equador. Watakatifu wapya ni: Kardinali John Newman, muasisi wa Kituo cha Michezo cha Mtakatifu Filippo Neri kilichoko nchini Uingereza. Sr. Giuseppina Vannini, Muasisi wa Shirika la Mabinti wa Mtakatifu Camillus; Maria Theresa Chiramel Mankidiyan, Muasisi wa Shirika la Watawa wa Familia Takatifu; Sr. Dulce Lopes Pontes wa Shirika la Watawa Wamisionari wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili na Mama wa Mungu pamoja na Margarita Bays, Bikira na mtawa wa Utawa wa tatu wa Mtakatifu Francisko wa Assisi.

Baba Mtakatifu kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 13 Oktoba 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewashukuru watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliofika mjini Vatican kushuhudia Kanisa likiwatangaza watakatifu wapya watano. Amewashukuru wageni maalum kutoka ndani na nje ya Italia, lakini kwa namna ya pekee, wageni kutoka Uingereza kwa ushuhuda wao wa Kiinjili, kwa Watakatifu hawa wapya ambao wamechangia ukuaji wa maisha ya kiroho na kijamii katika nchi zao asilia. Baba Mtakatifu amechukua fursa hii kumkaribisha Askofu Ian Ernest ambaye ameteuliwa hivi karibuni kuwa Mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Kanisa Anglikani, Roma.

Baba Mtakatifu ametambua na kushukuru uwepo wa waamini wa Kanisa Anglikani bila kuwasahau wale wote waliofuatilia Ibada hii ya Misa Takatifu kwa njia ya vyombo mbali mbali vya mawasiliano ya jamii. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza waamini wa Kanisa Katoliki nchini Poland ambao, Jumapili tarehe 13 Oktoba 2019 wameadhimisha Siku ya Ukarimu wa Papa. Anawashukuru kwa sala na mchango wao wa hali na mali katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Papa: Shukrani
13 October 2019, 15:16