Papa Francisko: Utume wa Bahari: Ujumbe: Kukuza na kudumisha utakatifu wa maisha na mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Papa Francisko: Utume wa Bahari: Ujumbe: Kukuza na kudumisha utakatifu wa maisha na mchakato wa majadiliano ya kiekumene. 

Papa Francisko: Utume wa Bahari: Utakatifu wa maisha na Uekumene

Chama cha Mabaharia Wakristo Kimataifa, ICMA, kuanzia tarehe 21 hadi tarehe 25 Oktoba 2019 huko Kaohsiung, nchini Taiwan, kinaadhimisha mkutano wa kumi na moja wa kimataifa kama sehemu ya Jubilei ya Miaka 50 ya kufanya kazi bega kwa bega na Mabaharia na Wavuvi pamoja na familia zao. baba Mtakatifu Francisko anawataka wajumbe kukuza: utakatifu na majadiliano ya kiekumene.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chama cha Mabaharia Wakristo Kimataifa, “The International Christian Maritime Association, ICMA”, kilianzishwa kunako mwaka 1969. Kina jumla ya vituo 450 kwa ajili ya huduma kwa Mabaharia na viongozi wa maisha ya kiroho 900 wanaotekeleza dhamana na utume wao katika nchi 120. Chama hiki pamoja na mambo mengine, kinapania kuhakikisha kwamba, kinahamasisha umoja, amani na maridhiano kati ya watu, kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene. Ni chama kinacho thamini na kuheshimu tofauti msingi za kiimani na kinapania kushirikiana wadau mbali mbali katika kulinda na kutetea ustawi, maendeleo na mafao ya Mabaharia pamoja na familia zao. Chama cha Mabaharia Wakristo Kimataifa, ICMA, kuanzia tarehe 21 hadi tarehe 25 Oktoba 2019 huko Kaohsiung, nchini Taiwan,  kinaadhimisha mkutano wa kumi na moja wa kimataifa kama sehemu ya Jubilei ya Miaka 50 ya kufanya kazi bega kwa bega na Mabaharia na Wavuvi pamoja na familia zao.

Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amewatumia wajumbe wa mkutano huu, ujumbe kwa njia ya video anawatakia heri na baraka katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya uwepo na utume wao miongoni mwa Mabaharia, Wavuvi pamoja na familia zao. Anawataka wanachama kuendelea kujikita katika mchakato na upyaisho wa majadiliano ya kiekumene kama sehemu ya huduma kwa Mabaria, Wavuvi pamoja na familia zao. Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 31 Januari 1997 aliandika Waraka wa Kitume katika mfumo wa Barua Binafsi yaani “MOTU PROPRIO STELLA MARIS” yaani “Kuhusu Utume wa Bahari”. Katika Barua hii alikazia kuhusu umuhimu wa Kanisa kutoa huduma ya maisha ya kiroho na kimwili kwa Mabaharia, Wavuvi pamoja na familia zao. Mtakatifu Yohane Paulo II alibainisha pia dhamana na utume wa wahudumu wa maisha ya kiroho katika Utume wa Bahari pamoja na kuyahamasisha Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kuwa na Idara ya Utume wa Bahari katika ngazi ya kitaifa na kikanda na kijimbo.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ujumbe huu bado ni hai hata katika mazingira ya sasa. Huduma hii pia inapaswa kutolewa kwa wasafiri na wale wote wanaotumia vyombo vya usafiri majini, ili kuhakikisha kwamba, wadau wote wanaofumbatwa katika Utume wa Bahari wanapata huduma msingi za maisha ya kiroho, zitakazowasaidia kuchochea utakatifu wa maisha. Ni matumaini na matamanio makubwa ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Utume wa Bahari utakoleza ari na moyo wa majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika utakatifu wa maisha; kwa kumtambua, kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu na hatimaye, kumwilisha mafundisho yake katika maisha yao; kwa kuheshimiana, kuthaminiana sanjari na kukuza fadhila ya ukarimu kwa watu wote bila ubaguzi. Anakitaka Chama cha Mabaharia Wakristo Kimataifa, “The International Christian Maritime Association, ICMA” kuwa na ujasiri wa kuweza kuvuka kinzani na vikwazo wanavyoweza kupambana navyo katika utume wao; daima wakijitahidi kujenga na kukuza  ari na mwamko wa majadiliano ya kiekumene. Mwishoni, anawapatia washiriki wote baraka zake za kitume na kuwaomba hata wao kumkumbuka na kumsindikiza katika maisha na utume wake!

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni, amewataka Mapadri washauri wa kiroho pamoja na watu wa kujitolea kuendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa mabaharia pamoja na wavuvi sehemu mbali mbali za dunia, wakijaribu kuiga na kufuata mifano ya watangulizi wao. Mama Kanisa anajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Pio XI alipoanzisha Utume wa Bahari, “Stella Maris” sanjari na Kongamano la 25 la Utume wa Bahari litakaloadhimishwa huko mjini Glasgow, nchini Scotland. Huu ni utume ulioasisiwa na waamini walei ndani ya Kanisa kama sehemu ya mchango wao wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaobubujika kutoka katika tunu msingi za Kiinjili!

Wanaokumbukwa zaidi ni Peter F. Hanson aliyeongokea Kanisa Katoliki, Arthur Gannon pamoja na Daniel Shields. Kongamano la 25 la Utume wa Bahari linatarajiwa kuadhimishwa kuanzia tarehe 29 Septemba 2020 hadi tarehe 4 Oktoba 2020 huko mjini Glasgow, nchini Scotland. Na kuanzia tarehe 4 Oktoba 2019 hadi tarehe 4 Oktoba 2020 ni maandalizi ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 Papa Pio XI alipoanzisha Utume wa Bahari, “Stella Maris”. Katika kipindi cha miaka 100 kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika Utume wa Bahari kwa Mama Kanisa kusoma alama za nyakati na kuendelea kujibu kilio cha mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na utume wao baharini! Pamoja na mambo mengine, Utume wa Bahari umeendelea kujizatiti ili kuhakikisha kwamba, mabaharia na wavuvi ambao wanajisadaka usiku na mchana ili kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi wanapata pia fursa ya kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao. Takwimu zinaonesha kwamba, Utume wa Bahari unatekeleza dhamana na wajibu wake katika bandari 261 katika nchi 55 na wanahudumiwa na Mapadre zaidi ya 200 bila kuwasahau watu wa kujitolea.

Wakati huo huo, Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu anapenda kuchukua fursa hii kuwaalika wadau wa huduma ya kiekumene kutoka Makanisa mbali mbali duniani; mashirika ya mabaharia kimataifa, wawakilishi wa Serikali, wawakilishi wa sekta ya uvuvi kuhakikisha kwamba, kuanzia sasa wanajipanga ili kuweza kuhudhuria tukio hili muhimu katika maisha na utume wa Kanisa kwa mabaharia pamoja na wavuvi. Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waratibu wa kanda na mapadre wakurugenzi wa Utume wa Bahari, kuhakikisha kwamba, Jubilei ya Miaka 100 ya Utume wa Bahari inaadhimishwa pia hata katika ngazi ya Kitaifa, Kijimbo na Kiparokia. Huu utakuwa ni muda muafaka wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, waliosadaka maisha yao bila ya kujibakiza kwa ajili Utume wa Bahari.

Ni muda wa kuwashukuru hata mabaharia na wavuvi wanaoendelea kuchakarika usiku na mchana pamoja na familia zao kwa sadaka kubwa na mchango wao katika ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu duniani! Kwa upande wake, Padre Bruno Ciceri, Mkurugenzi wa Utume wa Bahari Kimataifa anasema, lengo ni kuweza kuwasaidia mabaharia na wavuvi kutua nanga ya: imani, matumaini na mapendo katika maisha yao. Utume wa Bahari umejiaminisha katika ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Nyota ya Bahari. Hii itakuwa ni fursa pia ya kukuza na kuendelea kudumisha Ibada kwa Bikira Maria Nyota ya Bahari, inayopata amana na utajiri wake kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Utume wa Bahari unataka kuendelea kuwa ni sauti ya watu wasiokuwa na sauti katika maisha na utume wao! Utume wa Bahari katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 unataka kuanzisha miradi maalum kama kumbu kumbu ya tukio hili, miradi itakayotekelezwa kitaifa na katika ngazi ya Kijimbo!

Baba Mtakatifu anakazia zaidi kwa kusema, Mama Kanisa anapenda kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini! Papa Pio XI alitamani sana kuona kwamba, Utume wa Bahari unaendelezwa kwenye Bahari na fukwe mbali mbali za dunia. Roho Mtakatifu, kwa maombezi ya Bikira Maria aendelee kupyaisha utume na huduma hii mintarafu mahitaji ya ulimwengu mamboleo! Kuna mabaharia ambao dhamiri zao zinahangaika sana na mara nyingi Mapadre wa maisha ya kiroho kwa mabaharia na wavuvi wamekuwa ni msaada mkubwa. Mabaharia ni watu wanaofanya kazi zao mara nyingi nje ya nchi, makazi na familia zao! Mapadre washauri wa kiroho katika muktadha kama huu, wanakuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya matumaini kwa mabaharia na wavuvi waliopondeka na kuvunjika moyo! Mapadre wanapaswa kuwa ni watu wenye huruma, wapole na wanyenyekevu!

Kwa kutambua magumu yanayowakabili mabaharia na wavuvi, Baba Mtakatifu Francisko kama ilivyokuwa kwa Wamisionari wa Huruma ya Mungu, amewapatia madaraka Mapadre wote washauri wa maisha ya kiroho kwa mabaharia na wavuvi ili kuwaondolea watu dhambi zote hata zile ambazo kimsingi, zilikuwa zimehifadhiwa kwa ajili ya Kiti Kitakatifu tu! Baba Mtakatifu anasema, lengo ni kuweza kuwapatia watu amani na utulivu wa maisha ya kiroho huko baharini! Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Jumapili ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2019 amekazia mambo yafuatayo: Umuhimu wa mabaharia na wavuvi katika ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya binadamu ulimwenguni. Hawa ni watu wanaofanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi na kwamba, kuna umuhimu wa kutekeleza kwa vitendo, itifaki na mikataba mbali mbali ya kimataifa kwa ajili ya mabaharia na wavuvi sehemu mbali mbali za dunia!

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson anafafanua kwa kusema kwamba, mabaharia na wavuvi ni watu muhimu sana wanaochangia ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu ulimwenguni. Ni kundi linalosafirisha bidhaa mbali mbali zinazowaletea watu faraja, huduma, starehe pamoja na mafao yao kama watu binafsi na jamii katika ujumla wake. Jumapili ya Utume wa Bahari ni fursa ya kutafakari kwa kina na mapana mchango na huduma inayotolewa na mabaharia pamoja na wavuvi. Waswahili wanasema “eti, ukiona vinaelea ujue vimeumbwa! Watu wengi wanaweza kudanganyika na kuvutwa na hali pamoja na maisha ya mabaharia wanaosafiri sana kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine! Lakini, watu wasisahau kwamba, ni kundi la watu ambalo linafanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi na daima linakabiliwa na changamoto pevu katika utume wale. Mabaharia ni watu wanaotekeleza shughuli zao kwa sehemu kubwa wakiwa nje ya nchi na familia zao. Ni watu ambao mishahara yao inawafikia kwa kuchelewa sana na hata wakati mwingine hawapewi mishahara hadi pale wanapomaliza mikataba yao.

Vitendo vya kigaidi na uharamia baharini vimekuwa ni tishio kubwa kwa usalama wa maisha ya mabaharia na wavuvi pamoja na vyombo vyao vya kazi. Wamekuwa wakitekwa nyara na hata wakati mwingine kufunguliwa mashtaka ya uhalifu, bila kupata msaada wa kisheria wala kufaidika na mikataba pamoja na itifaki mbali mbali ambazo zimetiwa mkwaju na Jumuiya ya Kimataifa! Mabaharia na wavuvi ni watu kutoka katika mataifa, tamaduni na dini mbali mbali duniani, kiasi kwamba, ule mwingiliano na mafungamano ya kijamii yanaendelea kupungua kila kukicha. Matokeo yake ni mabaharia na wavuvi kutumbukia katika upweke hasi unaoweza kuwasababishia kushindwa kuona umuhimu wa kazi na maisha katika ujumla wake na huu ni mwanzo wa ugonjwa wa sonona, kuteteleka kwa afya ya akili pamoja na kuvunjika moyo na hivyo kubomoa uhusiano mwema na familia zao, mabaharia na wamiliki wa vyombo vya kazi. Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson anakiri kwamba, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na maboresho makubwa ya mazingira ya kazi na hali ya maisha katika ujumla wake.

Lakini, bado kuna sehemu mbali mbali za dunia, ambako wamiliki wa vyombo hivi bado wanaendelea kusua sua kutekeleza sheria, mikataba na itifaki zilizokubaliwa na Jumuiya ya Kimataifa, hali inayowaathiri mabaharia na wavuvi pamoja na familia zao. Kwa mara nyingine tena, Mama Kanisa anapenda kuchukua fursa hii ya maadhimisho ya Jumapili ya Utume wa Bahari kuyahamasisha Mashirika ya Kimataifa pamoja viongozi wa Serikali mbali mbali duniani bila kuwasahau wadau wa shughuli mbali mbali baharini kuhakikisha kwamba, wanajizatiti kikamilifu kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za wafanyakazi baharini. Mapadri washauri wa kiroho pamoja na watu wa kujitolea waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa mabaharia pamoja na wavuvi sehemu mbali mbali za dunia, wakijaribu kuiga na kufuata mifano ya watangulizi wao takribani miaka 100 iliyopita, yaani tarehe 4 Oktoba 1920.

Waamini walei wakajitosa kimasomaso kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya huduma makini kwa mabaharia na wavuvi sehemu mbali mbali za dunia. Wahudumu hawa wawe na ujasiri wa kutambua Uso wa Kristo Yesu kati ya mabaharia na wavuvi wanaokutana nao katika hija ya maisha na utume wao Baharini. Wasimame kidete: kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za mabaharia na wavuvi baharini kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko. Wawe ni mashuhuda na vyombo vya upendo wa Kristo kwa waja wake. Waendelee kushirikiana na kushikamana na wale wote wanaosimama usiku na mchana kuboresha mazingira ya kazi, kwa kuheshimu na kuthamini: utu, heshima na haki msingi za binadamu; mambo yanayoleta mafao kwa wafanyakazi wenyewe, wamiliki wa makampuni na watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu anahitimisha ujumbe wake kwa Jumapili ya Utume wa Bahari kwa kuwaweka mabaharia, wavuvi na wadau wengine wote, chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Nyota ya Bahari, ili aendelee kuwatia shime na nguvu katika utume wao!

Papa: Utume wa Bahari
21 October 2019, 14:19