Tafuta

Vatican News
Maadhimisho ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni kwa mwaka 2019: Kauli mbiu "Mmebatizwa na kutumwa kutangaza Injili: Kanisa la Kristo katika umisionari duniani". Maadhimisho ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni kwa mwaka 2019: Kauli mbiu "Mmebatizwa na kutumwa kutangaza Injili: Kanisa la Kristo katika umisionari duniani". 

Ujumbe wa Papa kwa Siku ya Kimisionari Ulimwenguni 2019

Maadhimisho ya Mwezi wa Kimisionari yasaidie: Kutambua upya mwingiliano wa Umisionari wa Imani yetu kwa Yesu Kristo, Imani tunayomiminiwa kwa huruma katika Sakramenti ya Ubatizo. Uhusiano wetu na Mungu daima huhusika na Kanisa. Kwa muungano wetu na Fumbo la Utatu Mtakatifu sisi pamoja na waamini wenzetu tunazaliwa upya! Ushuhuda wa imani katika matendo.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, - Dar es Salaam.

Wapendwa Kaka na Dada, kwa Mwezi Oktoba 2019, nimeomba kwamba Kanisa zima lihuishe mtazamo na wajibu wake wa Umisionari na majitoleo tukiwa tunafanya kumbukumbu ya karne moja ya Barua ya Kichungaji - MAXIMUM ILLUD ya Papa Benedikto XV (30 Novemba 1919). Kwa taswira yake ya kinabii na mtazamo wa mbali kwa utume huu, imenihimiza nione kwa mara nyingine tena umuhimu wa kupyaisha wajibu wa Kanisa katika Umisionari na kuchochea msukumo mpya wa kiinjili kwa kazi yake ya utangazaji na kuleta duniani wokovu wa Yesu Kristo ambaye alikufa na kufufuka tena. Ama hakika, barua hiyo ililenga masafa marefu yenye taswira ya Kinabii ya Kitume ambayo imenichochea kwa mara nyingine tena kuutambua umuhimu wa kuhuisha wajibu wa Kanisa na kuupatia msukumo mpya wa Uinjilishaji kwa kazi yake ya kichungaji ya kufundisha na kuifikishia dunia wokovu wa Yesu Kristo, ambaye alikufa na kufufuka tena. Kauli mbiu ya ujumbe huu wa sasa ni sawasawa na kauli mbiu ya Oktoba, Mwezi wa Umisionari: Kubatizwa na Kutumwa Kutangaza Injili: Kanisa la Kristo katika Umisionari Duniani.

Kwa kuadhimisha mwezi huu, kutatusaidia kwanza kutambua upya mwingiliano wa Umisionari wa Imani yetu kwa Yesu Kristo, Imani tunayomiminiwa kwa huruma katika Sakramenti ya Ubatizo. Uhusiano wetu wa dhati na Mungu siyo suala jepesi la mtu mmoja binafsi, bali daima huhusika na Kanisa. Kwa muungano wetu na Mungu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, sisi pamoja na waamini wenzetu wengi, kaka na dada, tunazaliwa upya. Maisha haya matakatifu siyo bidhaa kwa ajili ya kuuzwa kamwe hatuzalishi lugha ya ujazo, kumbe ni hazina ya kukabidhiwa, kushirikishwa na kutangazwa: hiyo ndiyo maana ya Umisionari. Tunaipokea zawadi hii bure na tunashirikishana bure (Rej. Mt. 10: 8), bila ya kumbagua mtu ye yote. Mungu anataka watu wote waokolewe kwa kuja kuutambua ukweli na kuonja huruma yake kwa njia ya Utume wa Kanisa, Sakramenti ya kiulimwengu ya wokovu (Rej. 1Tim 2:4, Lumen Gentium, 48). Kanisa liko katika Umisionari duniani. 

Imani kwa Yesu Kristo hutuwezesha kuona mambo yote katika uhalisia wake, tunapoutafakari ulimwengu kwa macho na moyo wake Mungu. Matumaini hutufungulia upeo wa umilele wa maisha ya Kimungu tunayoshirikishana. Upendo ambao tayari tunauonja kwa njia ya Sakramenti na katika maisha ya kidugu, hutusukuma kusonga mbele hadi miisho ya dunia. Kanisa linalopania kusonga mbele hadi miisho ya upeo wa dunia huhitaji daima upyaisho endelevu wa umisionari (Rej. Mik. 5:4; Mt. 28: 19; Mdo 1: 8; Rom 10: 18). Kanisa linalowania kusonga mbele hadi kwenye mipaka   ya mbali ya upeo wa macho, huhitaji daima kuboreshwa na miundombinu mipya ya Kimisionari. Watakatifu wangapi, wanaume kwa wanawake wenye imani wanaoshuhudia ukweli huu kwamba huu uwazi usio na  mipaka, huku kuenenda kwa huruma, ni jambo linalowezekana na la uhalisia, kwani husukumwa na upendo na ni maana halisi ya zawadi inayokita katika kina kirefu, sadaka na shukrani (Rej. 2Kor 5: 14 – 21). Mtu anayefundisha juu ya Mungu hana budi kuwa mtu wa Mungu (Rej. MAXIMUM ILLUD).

Huu udhamini wa kimisionari hutugusa sote, kila mmoja binafsi; mimi ni mmisionari daima, wewe ni mmisionari daima na kila mbatizwa, mwanaume kwa mwanamke ni mmisionari daima. Wapendanao hawaduwai; hujikatalia, huvutwa na pia kuwavutia wengine sawia. Wanajitoa kwa wengine na kujenga uhusiano ambao huleta uhai. Kwa kadiri ya upendo wa Mungu ulivyo, hakuna mtu ambaye hafai au kutokuwa na umuhimu. Kila mmoja wetu ni mmisionari kwa dunia kwani, kila mmoja wetu ni tunda la Upendo wa Mungu. Hata kama wazazi wanaweza kuusaliti upendo wao kwa uwongo, chuki na kukosa uaminifu, kamwe Mungu haiondoi zawadi yake ya uhai. Tangu milele amemkirimia kila mtoto wake zawadi ya kushiriki Utakatifu wake wa umilele (Rej. Eph.1:3 – 6). Uhai huu umetiwa ndani yetu kwa njia ya Ubatizo, ambao unatupatia zawadi ya imani kwa Yesu Kristo, mshindi wa dhambi na mauti. Ubatizo hutufanya upya kwa sura na mfano wa Mungu na kutufanya washiriki wa Fumbo la mwili wa Kristo, ambao ndio Kanisa lenyewe.

Kwa mantiki hiyo, ubatizo ni muhimu kweli kwa wokovu kwani huhakikisha kwamba daima na po pote sisi ni watoto wa Mungu, yaani wana na mabinti nyumbani kwa Baba, na siyo yatima, wageni au watumwa. Kile ambacho kwa Mkristo ni uhalisia wa Sakramenti inayokamilishwa na Ekaristi takatifu kinabaki kuwa wito na ukomo wa kila mwanamme na mwanamke katika kuwania mabadiliko na wokovu. Kwa jinsi hiyo, Ubatizo hukamilisha ahadi ya zawadi ya Mungu ambayo humfanya kila mmoja kuwa mwana au binti katika Mwana (Kristo). Sisi tu watoto wa wazazi wetu wa asili, lakini kwa Ubatizo, tunapokea uasili wote wa Ubaba na Umama halisi: hakuna mtu awezaye kuwa na Mungu kama Baba endapo hana Kanisa kama Mama (Rej. St. Cyprian De Cath. Eccl; 6). Kwa hiyo, Umisionari wetu umejikita katika Ubaba wa Mungu na Umama wa Kanisa. Yaliyotolewa na Yesu Kristo Mfufuka wakati wa Pasaka yanajidhihirisha katika Ubatizo: Kama Baba alivyonituma mimi, vivyo hivyo nawatuma ninyi, mkijazwa na Roho Mtakatifu, kwa upatanisho wa dunia (Rej. Yoh. 20:19 – 23; Mt. 28:16 – 20).

Utume huu ni sehemu ya utambulisho wetu kama Wakristo; hutufanya tuwajibike kwa kuwawezesha wanaume na wanawake wote kutambua wito wao wa kuwa watoto wa Baba, kutambua utu wao binafsi na kuthamini utu wa kila binadamu kuanzia inapotunga mimba hadi kifo cha kawaida. Katika utandawazi mamboleo uliozingirwa na malimwengu lukuki, unapogeuka kuwa tamaduni katili na kukataa ubaba hai wa Mungu katika historia ya maisha yetu, unakuwa kero dhidi ya upendo wa kidugu wa utu wa binadamu. Bila ya Umungu wa Yesu Kristo, kila tofauti hudhalilika na kuwa sumu ya hatari ilioje, na hivyo kusababisha ugumu katika maisha ya udugu na umoja wenye heri miongoni mwa binadamu. Wokovu wa watu ulimwenguni aliotujalia Mungu kwa njia ya Yesu Kristo ulimfanya Papa Benedikto XV kutoa wito wa kukomesha aina yo yote ya kusisitiza utaifa na ukabila, udhalilishaji na udhalimu, au upotoshaji wa ufundishaji Injili wenye maslahi ya kimabavu, kiuchumi na ya kijeshi ya utawala wa kikoloni.

Katika barua yake ya Kitume, MAXIMUM ILLUD, Papa Benedikto XV alisisitiza kwamba Ujumbe wa Kanisa la kiulimwengu unatakiwa uache kabisa mitazamo anuwai ya vikundi vya dini zinazolenga kuchochea vurugu ya chuki, na fitina miongoni mwa jamii ya kimataifa na Makanisa. Leo pia Kanisa linahitaji wanaume na wanawake ambao kwa vipawa vyao vya Ubatizo wataitikia wito huu kwa ukarimu katika kulitetea Kanisa lao, na kuwa tayari kuyaacha mazoea yao na makazi yao na hata taifa lao, nchi na lugha yao na hata Makanisa mahalia na kuwa tayari kutumwa kwenda kwa mataifa mengine, kwenye ulimwengu ambao haujapata mabadiliko yaletwayo na Sakramenti za Yesu Kristo na Kanisa lake takatifu. Kwa  kulitangaza Neno la Mungu, kwa kutoa ushuhuda wa Injili na kuadhimisha maisha ya Roho, wanaashiria mabadiliko, wanabatiza na kuleta wokovu wa Kikristo, wakiheshimu uhuru wa kila mtu, na katika majadiliano na tamaduni na dini za wale waliotumwa kwao.

Ujumbe wa “Missio ad gentes”, ambao daima ni muhimu kwa Kanisa, huchangia kwa namna mahsusi mambo ya msingi katika mchakato wa mabadiliko endelevu kwa Wakristo wote. Imani katika Fumbo la Pasaka ya Yesu; Ujumbe wa Kanisa uliopokelewa katika Ubatizo, kujibandua kijiografia na kiutamaduni kwa mtu binafsi na makazi yake mwenyewe, hitaji la wokovu kutoka dhambi na kufunguliwa kutoka maovu binafsi na ya kijamii: hayo yote yanahitaji Umisionari unaofika hadi miisho ya ulimwengu. Bahati njema iliyo sanjari na mwaka huu wa Jubilei na Maadhimisho ya Sinodi Maalumu ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, inanipa fursa kusisitiza jinsi Umisionari ulivyodhaminiwa kwetu na Yesu; na zawadi ya Roho wake nayo imekuja kwa wakati muafaka kwa nchi hizo na watu wake. Pentekoste mpya inafungua wazi milango ya Kanisa hivyo kwamba hakuna tamaduni zitakazobaki zimefungiwa na wala watu kutengwa nje ya umoja wa kiulimwengu wa imani. Hatakiwi mtu ye yote kujitenga kwa kujizamisha katika mambo yake binafsi akijikita katika mila na dini yake binafsi.

Fumbo la Pasaka ya Yesu, huvunjilia mbali vikwazo vya aina yo yote ile vya dunia, dini na tamaduni, na kuwaita ili wakue kwa heshima ya utu wa binadamu, wanaume kwa wanawake, ili kuweza kujikita kwenye kina kirefu cha mabadiliko kwa ukweli wa Bwana Mfufuka anayeleta uhai halisi kwa wote. Hapa nakumbushwa maneno ya Papa Mstaafu Benedikto XVI alivyotamka mwanzoni mwa mkutano wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean huko mjini Aparecida, nchini Brazili kunako mwaka 2007. Ningependa kuyanukuu maneno hayo na kuyafanya yawe yangu: “Hata hivyo, kupokea imani ya Kikristo kulimaanisha nini kwa mataifa ya Amerika ya Kusini na Caribbean? Kwao kulimaanisha kumjua na kumkaribisha Kristo, Mungu asiyejulikana ambaye mababu zao walimtafuta, bila kumtambua, licha ya utajiri wao mkubwa ulioshamiri katika dini zao   za jadi. Kristo ni mwokozi ambaye walikuwa wakimtamani kimya kimya. Pia ilimaanisha kuwa walipokea kutoka maji ya Ubatizo, Uhai Mtakatifu uliowafanya kuwa watoto wa Mungu kwa kuridhia; zaidi ya hayo, walimpokea Roho Mtakatifu aliyefika kuzifanya tamaduni zao zizae matunda, kuzitakasa na kuziendeleza mbegu anuwai ambazo ni Neno  Takatifu  lilizipanda; papo hapo kuliziongoza kwenye njia sahihi za Injili... Neno wa Mungu alipojimwilisha katika Yesu Kristo, pia ikawa historia na utamaduni. Wazo la kurejea nyuma na kuzihuisha dini za kale za Kolumbani, kuwatenga na Kristo na kutoka katika Kanisa la kiulimwengu kusingekuwa kusonga mbele kamwe bali kurudi nyuma. Kwa yamkini, kungekuwa ni kurudi nyuma katika kipindi cha historia iliyotia nanga huko zamani” (Hotuba ya ufunguzi wa Mkutano 13 Mei 2017 , Insegnamenti III, 1 (2007), 855 – 856).

Tunadhaminisha Umisionari wa Kanisa kwa Mama yetu Maria kwa kuungana na Mwanae. Kwa kuanzia pale alipojimwilisha ndani yake, Bikira Maria aliondoka kuanza hija yake. Alijihusisha kikamilifu katika Umisionari wa Yesu, utume ambayo pia ilikuwa wake mwenyewe akiwa chini ya Msalaba: Ni utume wa kushiriki, kama Mama wa Kanisa, akileta wana wa mabinti wapya wa Mungu wazaliwe katika Roho na katika Imani. Ningependa kuhitimisha kwa kutoa maneno machache juu ya Mashirika  ya Kipapa ya Kimisionari, ambayo tayari yametajwa katika MAXIMUM ILLUD kama rasilimali ya Umisionari. Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari yanatoa huduma kwa Kanisa kiulimwengu kama mtandao wa dunia nzima wa kumuunga mkono Papa katika majukumu yake ya Kimisionari: kwa sala, roho ya kimisionari, na ukarimu kutoka kwa wakristo duniani kote. Michango hiyo humsamdia Khalifa wa Mtakatifu Petro katika juhudi zake za Uinjilishaji kwa baadhi  ya Makanisa yenye uhitaji maalum (Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu”, katika kuwaandaa mapadri wazalendo (Shirika la Kipapa la Mtakatifu Petro Mtume), katika kuhamasisha mtazamo wa Kimisionari kwa watoto (Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu) na kuhamasisha na kutia moyo ukuzaji wa Imani ya Kikristo (Shirika la Kipapa la Umoja wa Wamisionari).

Kwa kuupa msukumo mpya mchango wangu kwa Mashirika ya Kipapa, naamini kuwa maadhimisho ya Mwezi adhimu wa Kimisionari, Oktoba 2019, utazaa matunda maridhawa katika kupyaisha huduma zao za Kimisionari kwa kazi yangu ya Kitume. Natoa Baraka zangu za dhati kwa Wamisionari wanaume kwa wanawake na kwa wale wote ambao kwa minajili ya Ubatizo wao, wanajumuika kwa namna fulani kwa utume wa Umisionari wa Kanisa.

Papa: Siku ya Kimisionari 2019

 

 

 

17 October 2019, 10:52