Tafuta

Vatican News
Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia mambo makuu ya kuzingatia: Wongofu wa kichungaji, kiekolojia, kimisionari kwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia mambo makuu ya kuzingatia: Wongofu wa kichungaji, kiekolojia, kimisionari kwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa.  (Vatican Media)

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Vipaumbele vya Kanisa!

Ili kuweza kuadhimisha vyema Sinodi hii, mambo makuu manne yanatakiwa kuelekezwa: Mabadiliko ya mwelekeo wa maisha ya mtu binafsi na jumuiya; wongofu katika mambo msingi; kinzani ndani ya Ukanda wa Amazonia na kwamba, Sinodi ni mchakato muhimu katika maisha na kwamba, kuna haja ya kujipatanisha na Mungu, Mazingira nyumba ya wote pamoja na majirani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anapania kumtangaza na kumshuhudia Kristo kuwa ni kiini cha maisha na wokovu wa walimwengu sanjari na kukabiliana na changamoto ya ekolojia fungamani. Lengo ni kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya maendeleo fungamani ya binadamu. Hiki ndicho kiini cha maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6-27 Oktoba, 2019. Kauli mbiu ni: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Baba Mtakatifu Francisko amependa kuyakabidhi maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Francisko wa Assisi aliyejisadaka katika maisha na utume wake kwa ajili ya kuwahudumia maskini, akasimama kidete kulinda mazingira nyumba ya wote pamoja na kujitahidi kutafuta amani na utulivu.

Maadhimisho ya Sinodi ya Amazonia ni muda wa toba na wongofu wa ndani; ili kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani, umoja na udugu wa kibinadamu; upendo na mshikamano wa dhati, ili wote waweze kupata utimilifu wa maisha. Ni muda wa sala na tafakari ili hatimaye, kufanya mang’amuzi yatakayolisaidia Kanisa kwenye Ukanda wa Amazonia kupata njia mpya kwa ajili ekolojia fungamani. Ili kuweza kuadhimisha vyema Sinodi hii, mambo makuu manne yanatakiwa kuelekezwa katika maisha na utume wa Kanisa: Mabadiliko ya mwelekeo wa maisha ya mtu binafsi na jumuiya; wongofu katika mambo msingi; kinzani ndani ya Ukanda wa Amazonia na kwamba, Sinodi ni mchakato muhimu katika maisha na utume wa Kanisa. Hapa kuna haja ya watu wa Mungu kujipatanisha na Mungu, Mazingira nyumba ya wote pamoja na majirani, ambao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Hii ni safari kuelekea katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu, changamoto inayohitaji ujasiri, kama unavyoshuhudiwa na watakatifu, wafiadini na waungama imani. Kanisa linataka kuwa ni sauti ya kinabii inayojikita katika wongofu wa kichungaji, wongofu wa kiekolojia na wongofu wa kimisionari, ili kuweza kutoka kifua mbele kwenda kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa, kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu ndiye nguzo kuu ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Maendeleo fungamani ya binadamu yanagusa kimsingi: masuala ya kisiasa, kijamii, kitamaduni na kimazingira. Ni mwaliko wa kujizatiti katika misingi ya haki sanjari na kujenga tasaufi ya utunzaji bora wa mazingira.

Kimsingi, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapaswa kuwa ni dira na mwongozo katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu wa Ukanda wa Amazonia. Lengo liwe ni kukabiliana na changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi katika umoja na mshikamano wa watu wa Mungu, kwa kuendelea kusoma alama za nyakati. Ukanda wa Amazonia unaonekana kwa sasa kukabiliwa na mvutano wa Kikanda na Kiulimwengu, kutokana na mvutano huu, Kanisa halina budi kutumia msingi wa Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ili hatimaye, liweze kutoa majibu muafaka kwa changamoto changamani zinazoendelea kwenye Ukanda wa Amazonia. Hapa kuna umuhimu wa kujizatiti katika wongofu wa kichungaji kwa kuondokana na mipasuko kati ya Hierakia na dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inayopania kutoa fursa zaidi kwa watu wa Mungu kushiriki kikamilifu katika kupanga, kuamua na kutekeleza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Hapa umoja na mshikamano ni mambo msingi sana.

Sinodi ni kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu, Ukanda wa Amazonia ni mwendelezo wa safari ambayo imefanywa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean CELAM, tangu mwaka 1955 hadi mwaka 2007 kwa mkutano wa Aparecida ulioasisi “Mtandao wa Kanisa Amerika ya Kusini”, (Pan-Amazon Ecclesial Network of the Latin American Church, REPAM). Sinodi ni chombo maalum cha ushauri kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kabla ya maadhimisho ya Sinodi, kuna umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka Ukanda wa Amazonia ambao umeshiriki katika hatua mbali mbali za maadhimisho haya. Wajumbe walioteuliwa kuwawakilisha watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia ni fursa kwa Mama Kanisa kuangalia changamoto hizi mintarafu umoja wa Maaskofu, wakiwa wameungana na Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu. Ikumbukwe kwamba, Sinodi ni tukio maalum ambalo limetengwa na Baba Mtakatifu kwa ajili ya kujadili mustakabali wa maisha na utume wa Kanisa kwa kuendelea kusoma alama za nyakati.

Maadhimisho ya Sinodi yasaidie kutakasa misimamo mikali, kwa kusoma alama za nyakati, ili kujibu kilio cha maskini na Dunia Mama. Watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia wanayo matumaini katika kukabiliana na changamoto zinazowaandama katika maisha yao. Huu ni Ukanda wenye watu milioni 33 na kati yao kuna wazawa milioni 3 kutoka katika watu wa makabila na mataifa zaidi 390. Hapa kunahitajika: Ujasiri na busara ya kichungaji ili kuweza kupata njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani. Baada ya maadhimisho ya Sinodi, hatua muhimu ni utekelezaji wa maamuzi yatakayokuwa yamefikiwa na Mababa wa Sinodi na hatimaye, Wosia wa Kitume, utakaotolewa kama dira na mwongozo wa Kanisa katika maisha na utume wake, Ukanda wa Amazonia.

Sinodi Amazonia: mambo msingi
07 October 2019, 14:24