Watakatifu wapya ni mashuhuda waliojitahidi kumwilisha ndani mwao huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa Mataifa, ushuhuda maisha na utume wa Kanisa. Watakatifu wapya ni mashuhuda waliojitahidi kumwilisha ndani mwao huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa Mataifa, ushuhuda maisha na utume wa Kanisa. 

Wasifu wa Watakatifu wapya kwa Mwaka 2019: Umisionari wa Kanisa

Watakatifu wapya: Kardinali John Newman: Umuhimu wa kutafuta ukweli na kuuambata! Sr. Giuseppina Vannini, sadaka na huduma kwa wagonjwa wa Roma. Maria Theresa Chiramel Mankidiyan alibahatika kupata mwilini mwake Madonda Matakatifu ya Yesu. Sr. Dulce Lopes Pontes: Sala katika huduma kwa wagonjwa. Margarita Bays: Ibada kwa B. M. Mkingiwa Dhambi ya Asili. Utakatifu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jumapili ya 28 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa, anatarajia kuwatangaza Wenyeheri watano kuwa watakatifu. Ibada hii ya Misa itaadhimishwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili  tarehe 13 Oktoba 2019 kuanzia majira ya saa 4:00 za asubuhi kwa saa za Ulaya. Watakatifu watarajiwa ni pamoja na Kardinali John Newman, muasisi wa Kituo cha Michezo cha Mtakatifu Filippo Neri, nchini Uingereza. Maisha ya Kardinali John Newman yalikuwa ni hija kuelekea kwenye ukweli mkamilifu. Alizaliwa kunako mwaka 1801, akawekwa wakfu kuwa Shemasi, Kanisa Anglikani. Baada ya tafakari ya kina na ya muda mrefu, akaongokea kwenye Kanisa Katoliki na Mwaka 1847 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre, akateuliwa kuwa Kardinali na Papa Leo XIII na kufariki dunia kunako mwaka 1890. Hii ni changamoto kwa waamini kuutafuta na kuuambata ukweli unaowaweka huru, ingawa una gharama zake. Ni kiongozi aliyejibidiisha kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo kwa wagonjwa, maskini pamoja na wafungwa gerezani. Maisha na wito wa kila Mkristo ni kuambata utakatifu wa maisha. 

Sr. Giuseppina Vannini, Muasisi wa Shirika la Mabinti wa Mtakatifu Camillus aliyezaliwa kunako mwaka 1859 mjini Roma, akapata malezi makini kutoka katika familia ya Kikristo. Akiwa na umri wa miaka 32, kunako mwaka 1891 akajiunga na maisha ya kitawa, baada ya safari ndefu ya maisha ya kiroho, mwaka 1892 akaanzisha Shirika na kukubaliwa na Kanisa kunako mwaka 1909, baada ya changamoto nyingi. Katika maisha na utume wake, akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa wa Roma. Tarehe 23 Februari 1911 akafariki dunia na kuacha Shirika lake likiwa na watawa 156. Tarehe 16 Oktoba 1994, akatangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa ni Mwenyeheri.

Maria Theresa Chiramel Mankidiyan, Muasisi wa Shirika la Watawa wa Familia Takatifu aliyezaliwa kunako mwaka 1876. Alipata malezi makini kutoka kwa Mama yake na katika ujana wake, akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini, wagonjwa pamoja na kutoa hifadhi kwa watu ambao hawa kuwa na makazi maalum. Akajaliwa neema ya kuwa na maono, akapata mang’amuzi ya Madonda Matakatifu mwilini wake, na hatimaye, akabahatika kuanzisha Shirika la Watawa wa Familia takatifu kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa waliokuwa kufani pamoja na elimu na majiundo makini kwa wasichana wa kizazi kipya. Akafanikiwa kuliongoza Shirika kwa kipindi cha miaka 12. Akafariki dunia kunako mwaka 1926 na kutangazwa Mwenyeheri na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2000.

Sr. Dulce Lopes Pontes wa Shirika la Watawa Wamisionari wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili na Mama wa Mungu, alizaliwa kunako mwaka 1914, akiwa na umri wa miaka 18 alijiunga na Shirika la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili na Mama wa Mungu. Alivutiwa sana na maisha na wito wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu. Akasaidia sana kuunda umoja wa wafanyakazi wa Mtakatifu Francisko, ili kuwasaidia wafanyakazi waliokuwa wanakabiliwa na matatizo pamoja na changamoto mbali mbali za maisha. Kunako mwaka 1959 akaanzisha Hospitali kama kielelezo cha huduma ya upendo. Akafariki dunia kunako mwaka 1992. Ni mtawa ambaye alikita maisha yake katika sala iliyomwilishwa kwenye huduma ya upendo kwa wagonjwa, kiasi kwamba, upendo wake, ukavunjilia mbali kuta zilizokuwa zinawatenganisha watu! Leo hii amekuwa ni mfano bora wa kuigwa katika uchaji na utakatifu wa maisha!

Margarita Bays, Bikira na mtawa wa Utawa wa tatu wa Mtakatifu Francisko wa Assisi, alizaliwa kunako mwaka 1815. Katika maisha yake alikuwa ni mshonaji, dada wa nyumbani na katekista, akabahatika kupata Madonda Matakatifu mwilini wake. Kwa muujiza, akaponeshwa saratani ya tumbo tarehe 8 Desemba 1854 wakati Papa Pio IX alipokuwa anatangaza kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mungu Mwenyezi, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Akafariki dunia katika hali ya neema kunako mwaka 1879. Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza kuwa Mwenyeheri kunako mwaka 1995.

Watakatifu wanatarajiwa wanatangazwa wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kwa kuongozwa na kauli mbiu "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani". Hati ya maandalizi ya Sinodi ya Amazonia inakazia umuhimu wa: kuona, kung'amua na kutenda! Ni Sinodi itakayopembua tema mbali mbali:kuhusu: haki jamii, malezi awali na endelevu, katekesi, liturujia na utambulisho wa Kanisa katika Ukanda wa Amazonia. Watakatifu wapya, wanawekwa mbele ya macho ya watu wa Mungu kama mfano na kielelezo cha kufuatwa katika maisha na utume wa Kanisa.

Watakatifu wateule wanatangazwa wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa. Kanisa la Kristo katika utume”. Kanisa linaendeleza wito na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, agizo kutoka kwa Kristo mwenyewe kwa wafuasi wake. Hiki ni kipindi maalum sana kwa maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni muda wa kutangaza furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa; Kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa ari na ushiriki mkamilifu na hatimaye, Kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Watakatifu wa Kanisa
11 October 2019, 17:28