Vatican News
Papa Francisko asikitishwa sana na mauaji ya kinyama yaliyotokea huko Halle nchini Ujerumani kwa sababu ya chuki za kidini! Papa Francisko asikitishwa sana na mauaji ya kinyama yaliyotokea huko Halle nchini Ujerumani kwa sababu ya chuki za kidini! 

Papa Francisko asikitikishwa na mauaji ya Halle, nchini Ujerumani

Papa Francisko amewaombea watu wawili waliouwawa kikatili na Stephan Balliet, huko mjini Halle, nchini Ujerumani kutokana na chuki za kidini. Watu hawa wameuwawa karibu na Sinagogi la waamini wa dini ya Kiyahudii Zaidi ya waamini 80 walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya sala kwenye Sinagogi hilo. Jeshi la Polisi nchini Ujerumani linaendelea kufanya uchunguzi wa mauaji haya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Kikao cha Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, Jumatano jioni, tarehe 9 Oktoba 2019 amewakumbuka na kuwaombea watu wawili waliouwawa kikatili na Stephan Balliet, mwenye umri wa miaka 27 huko mjini Halle, nchini Ujerumani kutokana na chuki za kidini. Watu hawa wameuwawa karibu na Sinagogi la waamini wa dini ya Kiyahudi. Taarifa zinabainisha kwamba, zaidi ya waamini 80 walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya sala kwenye Sinagogi hilo. Jeshi la Polisi nchini Ujerumani linaendelea kufanya uchunguzi kuhusu mauaji haya ya kinyama. Itakumbukwa kwamba, Waamini wa dini ya Kiyahudi kila mwaka husherehekea Siku kuu ya Rosh Ha-Shanah, yaani Mwanzo wa Mwaka Mpya wa Kiyahudi. Hizi ni sherehe zinazoambatana na Siku kuu ya Yom Kippur, yaani: Sherehe ya toba na utakaso wa dhambi na hatima ya sherehe zote hizi ni Siku kuu ya Sukkot, yaani Sherehe ya vibanda ambayo inafahamika zaidi kuwa ni Sherehe ya mavuno.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni amewatumia ujumbe wa matashi mema waamini wa dini ya Kiyahudi wanaoishi mjini Roma. Ujumbe huu umetumwa kwa Rabbi Riccardo Di Segni, Mkuu wa Jumuiya ya Wayahudi mjini Roma. Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini, anapenda kutuma salam na matashi mema katika maadhimisho haya, ili yaweze kuwafikia waamini wote wa dini ya Kiyahudi, sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa kusema kamba, Sherehe hizi ziwe ni chemchemi ya neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, anayependa kuwakirimia waja wake ile furaha na amani ya ndani. Mwenyezi Mungu anayewapenda wale wote wanaojiaminisha kwake, na kuwasindikiza katika hija ya maisha yao, awasaidie waamini wote kumshuhudia kwa njia ya huduma kwa jirani zao, kwa kuendelea kujikita katika kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani!

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia 2019 yanafuata kwa dhati kabisa Katiba ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko “Episcopalis Communio” yaani “kuhusu Sinodi za Maaskofu” inayobainisha kwamba: Sinodi ni chombo cha uinjilishaji kinachofumbatwa katika ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza, kuadhimisha na kutekeleza kwa kwa pamoja yale mambo msingi yaliyofikiwa. Baba Mtakatifu, Jumatano jioni, tarehe 9 Oktoba 2019 ametumia fursa ya uwepo na ushiriki wake kuchangia hatua mbali mbali ambazo zimefikiwa na Kanisa kama sehemu ya maadhimisho ya Sinodi hii. Hii ni changamoto kubwa katika maisha na utume wa Kanisa, kumbe, Kanisa linawajibika kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili; kwa kusimama kidete ili kukazia ekolojia fungamani.

Lengo la Sinodi hii ni kubainisha njia mpya za uinjilishaji Ukanda wa Amazonia, kwa kusikiliza kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini; kwa kupembua matatizo, changamoto na fursa zilizopo ili kutoa mapendekezo yatakayofanyiwa kazi na Kanisa. Baba Mtakatifu hadi wakati huu, amefurahishwa na mchango wa mawazo, tafakari na mang’amuzi yanayotolewa na Mababa wa Sinodi.

Papa: Mauaji Halle

 

 

10 October 2019, 14:31