Baba Mtakatifu Francisko asema, ile Sanamu ya "Pachamama" iliyokuwa imeibiwa na kutupwa mtoni, imepatikana. Baba Mtakatifu anaomba msamaha kwa wale waliotikiswa kwa kitendo hiki! Baba Mtakatifu Francisko asema, ile Sanamu ya "Pachamama" iliyokuwa imeibiwa na kutupwa mtoni, imepatikana. Baba Mtakatifu anaomba msamaha kwa wale waliotikiswa kwa kitendo hiki! 

Papa Francisko: Sanamu ya "Pachamama" imepatikana!

Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii, kuomba msamaha kwa wale wote waliojeruhiwa na kusikitishwa kwa tukio hili, ambalo limepewa uzito wa pekee kwenye vyombo vya habari kitaifa na kimataifa. Sanamu hii kwa sasa inahifadhiwa kwenye Kituo cha Polisi wa Italia na uchunguzi bado unaendelea ili kuwabaini waliohusika, ili hatimaye, waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, Ijumaa jioni, tarehe 25 Oktoba 2019 amewaambia Mababa wa Sinodi kwamba, ile Sanamu ya “Pachamama” yaani “Dunia Mama” inayomwonesha mwanamke mwenye mimba, alama ya uhai na utakatifu wa maisha, iliyokuwa imeibiwa kutoka kwenye Kanisa la “Santa Maria in Trasportina”, liliko mjini Roma na kutupwa kwenye Mto Tevere, Jumatatu, tarehe 21 Oktoba 2019 imepatikana. Sanamu ile ni alama ya uhai, zawadi ya maisha na kilio cha “Dunia Mama” iliwekwa Kanisani si kwa nia ya kuwataka waamini kuiabudu! Tukio hili la kusikitisha na kuhuzunisha limetokea mjini Roma! Baba Mtakatifu kama Askofu wa Jimbo la Roma, ametumia fursa hii, kuomba msamaha kwa wale wote waliojeruhiwa na kusikitishwa kwa tukio hili, ambalo limepewa uzito wa pekee kwenye vyombo vya habari kitaifa na kimataifa.

Sanamu hii kwa sasa inahifadhiwa kwenye Kituo cha Polisi wa Italia na uchunguzi bado unaendelea ili kuwabaini waliohusika, ili hatimaye, waweze kuchukuliwa hatua za kisheria. Baba Mtakatifu ameonesha nia yake ya kuiweka Sanamu hii tena kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati wa kufunga rasmi maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda waAmazonia, Jumapili tarehe 27 Oktoba 2019. Itakumbukwa kwamba, Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake kuhusu tukio hili la kusikitisha anakaza kusema, ni uhalifu wa hali ya juu kabisa unaoonesha ile dhana ya baadhi ya watu kutaka “kujimwambafai” katika jamii kama walivyoshuhudia katika video ya tukio hilo ambayo imesambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Hawa ni wi watu wanaojidai kwamba, ni “wana harakati na watetezi wa Mapokeo ya Kanisa”. Lakini cha kushangaza ni kitendo cha kuiba na kuitupa Sanamu hii mtoni; Sanamu inayoonesha zawadi ya uhai na utakatifu wa maisha. Hii ni alama muhimu sana kwa watu wa Ukanda wa Amazonia, wanaotumia alama hii kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya kazi ya Uumbaji. Hii ni changamoto kwa wale waotaka “kujimwambafai” kuwa ni “wanaharakati wa kutunza na kuendeleza Mapokeo ya Kanisa” kujisomea tena changamoto iliyotolewa na Mtakatifu Kardinali John Henry Newman katika insha yake ijulikanayo kama “Essay on the Development of Christian Doctrine” iliyochapishwa kunako mwaka 1878. Katika insha hii Mtakatifu Newman anafafanua kuhusu mchakato wa Kanisa linalowajibika kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili ya Kristo Yesu katika maisha na vipaumbele vya watu, kwa kutumia: alama, mila, mavazi, desturi na tamaduni zao njema, bila kusahau siku kuu na maadhimisho kadiri ya kalenda ya maisha yao.

Kwa maneno mengine, huu ni mchakato wa Kanisa kusoma alama za nyakati. Watu hawa wanaojimwambafai kwa kujiita kuwa ni wanaharakati wamesahau kwamba, Kanisa katika maisha, utume na historia yake, limeendelea kuziinjilisha tamaduni, ili kuitamadunisha Injili ya Kristo. Kwa mfano wimbo wa “Kyrie Eleison” yaani “Bwana Utuhurumie” una asili yake katika tamaduni za kipagani!

Papa: Pachamama

 

 

26 October 2019, 11:05