Tafuta

Papa Francisko asema, Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia inafumbatwa katika masuala ya shughuli za: Kichungaji, Kisiasa, Kitamaduni na Kiekolojia. Papa Francisko asema, Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia inafumbatwa katika masuala ya shughuli za: Kichungaji, Kisiasa, Kitamaduni na Kiekolojia. 

Sinodi ya Maaskofu Amazonia: Kichungaji, Kisiasa & Kiekolojia!

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia inaongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Sinodi inazingatia mambo makuu manne: Shughuli za Kichungaji, Kitamaduni, Kisiasa na Kiekolojia; mambo yanayo ambatana na kukamilishana. Mababa wa Sinodi wanapaswa kupembua changamoto hizi kwa kutumia jicho ya Mitume wa Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6-27 Oktoba, 2019 yanaongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Hii ni Sinodi inayoadhimishwa kwa kuzingatia mambo makuu manne: Shughuli za Kichungaji, Kitamaduni, Kisiasa na Kiekolojia; mambo yanayo ambatana na kukamilishana. Mababa wa Sinodi wanapaswa kupembua changamoto hizi kwa kutumia jicho ya Mitume wa Yesu. Watambue kwamba, wanawajibishwa na upendo wa Mungu uliomiminwa ndani mwao kwa njia ya Roho Mtakatifu, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, inayofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Hii ni changamoto kwa Mababa wa Sinodi kuheshimu na kuthamini: historia, tamaduni, mtindo wa maisha, kwa kuthamini utambulisho wao, hekima na busara inayowaongoza katika maisha.

Hii ni sehemu ya hotuba elekezi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kwenye Ukumbi wa Sinodi za Maaskofu mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 7 Oktoba 2019. Baba Mtakatifu anasema, wazawa wanapaswa kuwa ndio wadau wakuu katika mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kuwa karibu na familia ya Mungu Ukanda wa Amazonia, unaonyemelewa kwa kiasi kikubwa na ukoloni wa kiitikadi unaotaka kupekenya utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi sanjari na kuharibu mazingira nyumba ya wote! Ukoloni wa kiitikadi unajikita katika sera na mikakati ya maendeleo isiyozingatia wala kuthamini: historia, utamaduni, utu na heshima yao.

Kanisa linapaswa kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina na utamadunisho, ili kupambana na ukoloni wa kiitikadi, ili Kanisa liweze kuwatambua, kuwakubali na kuwashangaa kutokana na utajiri na amana waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Mababa wa Sinodi wanapaswa kuwa makini na watu wanaojitafutia umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Umaarufu huu umekuwa ni chanzo cha kuwagawa, kuwanyonya na kuwadhulumu watu haki zao msingi. Kanisa linawajibika kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili kwa kuzingatia uhalisia wa maisha ya wananchi mahalia. Kanisa linataka kuhakikisha kwamba, Ukanda wa Amazonia unajikita katika maendeleo fungamani ya binadamu, kwa kulinda na kutunza tunu msingi za maisha ya watu mahalia: kitamaduni na kichungaji kwa kuibua mbinu mkakati wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; maboresho ya maisha ya watu na utu wao pamoja na kuwajengea uwezo wa kupambana na hali pamoja na mazingira yao!

Kinachohitajika anasema Baba Mtakatifu ni wongofu wa kiekolojia na ule wa shughuli za kichungaji, ili kuweza kuwahudumiwa kwa ukamilifu zaidi watu wa Mungu, Ukanda wa Amazonia. Yote haya yatatekelezwa kwa kujadiliana na kusikilizana katika ukweli na uwazi kwa kutambua kwamba, Sinodi ni muda wa sala, tafakari na mang’amuzi ya kina na wala si mahali pa kuoneshana “ubabe katika matumizi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii”. Kanisa Takatifu Katoliki na la Mitume linajengeka katika mfumo wa Hierakia na kwamba, Sinodi maana yake ni familia ya Mungu kuweza kutembea kwa pamoja chini ya ulinzi na uongozi wa Roho Mtakatifu na kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu katika maadhimisho haya na kamwe Mababa wa Sinodi wasithubutu kumtupilia mbali na maadhimisho haya. Mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi hauna budi kufuatwa na kutekelezwa kwa dhati; kwa kuwajibika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu, Ukanda wa Amazonia.

Papa: Ufunguzi

 

07 October 2019, 16:23