Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anatoa mwito kwa wadau na wajuu wa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti katika majadiliano ili kupata ufumbuzi wa mgogoro wa kivita huko Mashariki ya Kati. Baba Mtakatifu Francisko anatoa mwito kwa wadau na wajuu wa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti katika majadiliano ili kupata ufumbuzi wa mgogoro wa kivita huko Mashariki ya Kati.  (AFP or licensors)

Papa Francisko asikitishwa na mateso ya watu Siria na Equador!

Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza wahusika wote pamoja na wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kujielekeza zaidi katika mchakato wa kutafuta na kudumisha haki jamii, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu! Mababa wa Sinodi wanahofia hali ya kisiasa nchini Equador!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 13 Oktoba 2019 ameonesha masikitiko yake makubwa kutokana na vita inayoendelea huko Mashariki ya Kati na hasa nchini Siria ambayo kwa siku za hivi karibuni, imetumbukia katika vita. Taarifa zinaonesha kwamba, kuna umati mkubwa wa watu wa Mungu, Kaskazini- Mashariki mwa Siria ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao ili kutafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Kati yao, kuna umati mkubwa wa familia za Kikristo ambazo zimeendelea kuteseka kutokana na vita na dhuluma huko Mashariki ya Kati. Baba Mtakatifu Francisko kwa mara nyingine tena anapenda kutoa wito kwa wadau wote wanaohusika pamoja na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete katika njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kuweza kupata suluhu ya mgogoro huu wa kivita unaoendelea kusababisha maafa makubwa kwa wafu na mali zao.

Baba Mtakatifu Francisko kwa niaba ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia na hasa wale wanaotoka nchini Equador, anasema, wanaendelea kufuatilia kwa wasi wasi na hofu kubwa hali tete ya kisiasa ambayo imeibuka hivi karibuni nchini Equador. Baba Mtakatifu anaiweka Equador chini ya ulinzi na tunza ya watakatifu wapya waliotangazwa na Kanisa tarehe 13 Oktoba 2019. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha masikitiko na mshikamano wake wa dhati na wale wote wanaolia na kuomboleza kwa kuondokewa na ndugu zao bila kuwasahau majeruhi wanaoteseka kutokana na mgogoro huu. Baba Mtakatifu anawahimiza wahusika wote kujielekeza zaidi katika mchakato wa kutafuta na kudumisha haki jamii, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu! Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa awe ni mfano bora wa ukamilufu wa Kiinjili, na awasaidie waamini kufuata mifano bora ya watakatifu wapya wa Kanisa!

Papa: Mateso
13 October 2019, 15:35