Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni 2019: Idadi ya Makatekista inazidi kuongezeka katika maisha na utume wa Kanisa! Bara la Afrika linaongoza! Maadhimisho ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni 2019: Idadi ya Makatekista inazidi kuongezeka katika maisha na utume wa Kanisa! Bara la Afrika linaongoza! 

Siku ya Kimisionari Ulimwenguni 2019: Utume wa Makatekista!

Makatekista ni kati ya mihimili ya uinjilishaji ndani ya Kanisa kwani jukumu lao kubwa ni kuwaandaa Wakatekumeni ili waweze kupokea vyema Sakramenti za Kanisa. Makatekista wengi wamekuwa ni mfano bora na mwanga kwa jumuiya zinazowazunguka. Kanisa linaendelea kuwashukuru Makatekista kwa mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa, sasa wawezeshwe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kubatizwa na Kutumwa Kutangaza Injili: Kanisa la Kristo katika Umisionari Duniani: ndiyo kauli mbiu ambayo inaongoza maadhimisho ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni iliyofikia kilele chake kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 20 Oktoba 2019. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kupanda Mlima wa Bwana, ili kukutana na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao katika hali ya ukimya na sala sanjari na kugundua uzuri wa watu wa Mungu kukaa kwa pamoja katika amani, upendo na utulivu. Hii ni fursa ya kugundua mambo msingi na kuyapatia kipaumbele cha pekee yaani: Mungu na jirani. Baba Mtakatifu anasema, hii ni fursa ya kupambana na ubinafsi, uchoyo na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahitaji ya jirani. Huu ni mchakato wa sadaka ya maisha inayomwilishwa katika huduma ya upendo, ili wote waweze kuokoka.

Waamini wanakumbushwa kwamba, wamepewa dhamana ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Kila mwamini anao utume anaopaswa kuutekeleza kadiri ya hali ya maisha na mazingira yake. Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume "Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari”. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni Waraka ambao umepyaisha maisha na utume wa Kanisa mintarafu mchakato wa uinjilishaji. Kristo Yesu mwingi wa huruma na upendo ndiye aliyeshinda dhambi na mauti; tumaini linashinda woga; udugu wa kibinadamu unashinda dhana ya uadui. Kristo Yesu ni amani na umoja wa waja wake na kiini cha wokovu wa watu wote. Jambo la msingi kwa waamini ni kuendelea kusali daima, kwa ajili ya kuamsha ari na moyo wa shughuli za kimisionari sehemu mbali mbali za dunia! Makatekista ni kati ya mihimili ya uinjilishaji ndani ya Kanisa kwani jukumu lao kubwa ni kuwaandaa Wakatekumeni ili waweze kupokea vyema Sakramenti za Kanisa.

Makatekista wengi wamekuwa ni mfano bora na mwanga kwa jumuiya zinazowazunguka. Kanisa linaendelea kuwashukuru Makatekista kwa mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa. Hili ni kundi ambalo linahitaji kupatiwa majiundo ya kina na endelevu, ili liweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake ndani ya Kanisa. Lakini, Makatekista wanapaswa kulindwa na kuheshimiwa, kwani mfanyakazi mwaminifu katika shamba la Bwana anastahili kupata ujira wake. Makatekista wanaendelea kuchangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanatoa ushuhuda wa imani tendaji kwa njia ya maisha na matendo yao adili, kwa kuwajali wote bila ubaguzi. Ni mwaliko wa kumwilisha Injili na Mafundisho ya Mababa wa Kanisa, ili kutoa Katekesi safi na ya kina kwa watu wao; wakiwaongoza kwa moyo wa Sala na Ibada. Kama sehemu ya viongozi wa Kanisa, Makatekista wanapaswa kutekeleza wajibu wao kwa ujasiri, bidii, ari na moyo mkuu, ili kuchangia utakatifu wa maisha ya familia ya Mungu inayowajibika. Hivi ndivyo alivyoandika Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake wa kichungaji, “Africae Munus” yaani “Dhamana ya Afrika”.

Makatekista wanapaswa kuwezeshwa kikamilifu ili waweze kufundisha kwa umakini mkubwa kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili pamoja na maisha ya sala, ili waamini waweze kupata neema zinazotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho haya. Makatekista wanao wajibu wa kuwasaidia waamini kumwilisha imani yao katika uhalisia wa maisha kwa njia ya ushuhuda unaoleta mvuto na mguso. Ni watu wanaopaswa kuwasaidia waamini kujenga na kuimarisha moyo wa sala na ibada kama njia ya kuzungumza na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao. Takwimu zilizotolewa kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni kwa Mwaka 2019 zilizotolewa na Shirika la Habari za Kimisionari, FIDES zinaonesha kwamba, kumekuwepo na ongezeko kubwa la waamini walei wanaojitaabisha katika maisha na utume wa Kanisa, ili kuyatakatifuza malimwengu kwa tunu msingi za Kiinjili.

Hatima ya maisha na utume wa Kanisa kwa siku za usoni, iko mikononi mwa Makatekista na waamini walei katika ujumla wao. Makatekista ni wahamasishaji, watangazaji na mashuhuda wa Neno la Mungu “Kerygma” linalomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao. Ni watu ambao kwa hakika wamekuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huduma; faraja na matumaini kwa wale waliokata tamaa. Kuna Makatekista wanatoa huduma kwa watu zaidi ya bilioni 1.3 sawa na asilimia 17.7% ya Idadi ya watu bilioni 7.4 duniani kote.  Idadi ya waamini wa Kanisa Katoliki Barani Afrika inaendelea kuongezeka maradufu! Lakini muhimu zaidi ni ushuhuda wa imani. Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu anasisitiza kwamba, Makatekista katika Makanisa ya kimisionari ni nguzo ya uinjilishaji na utamadunisho wa Kanisa; dhamana ambayo wamekabidhiwa na viongozi wa Makanisa mahalia. Kutokana na uhaba wa wakleri, wao wanaongoza Ibada bila Padre; wanawaandaa watoto kupokea na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa.

Makatekista ni vyombo na mashuhuda wa majadiliano ya kidini na kiekumene; sehemu ya vinasaba na utambulisho wa Mama Kanisa. Wakleri, watawa na waamini walei wamekuwa na mchango mkubwa sana katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima:kiroho na kimwili. Kanisa limewekeza sana katika huduma ya elimu bora kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Kanisa linamiliki na kuendesha vituo vya watoto wadogo vipatavyo 71, 000, shule za msingi ni 101, 000, shule za Sekondari ni 48, 000. Vituo, shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu ni majukwaa ya majadiliano ya kidini na kiekumene. Takwimu zinaonesha kwamba, Kanisa Katoliki linamiliki na kuendesha miundo mbinu mbali mbali ya huduma ya afya ipatayo, 105, 000: kati yake kuna hospitali 5, 000, Zahanati ni 16, 000, Vituo vya wagonjwa wa Ukoma ni 646 na nyumba za wazee ni takribani 15, 000 na zaidi ya vituo 10, 000 kwa ajili ya watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu. 

Huduma ya Injili ya upendo kwa watu wa Mungu Barani Afrika ni chemchemi ya matumaini mapya. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, waendelee kuchangia kwa hali na mali kazi za kimisionari sehemu mbali mbali za dunia! Mchango wa kwanza iwe ni sala endelevu!

Makatekista
21 October 2019, 09:18