Tafuta

Papa Francisko anawataka watawa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa watu duniani. Papa Francisko anawataka watawa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa watu duniani. 

Papa: Watawa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini duniani

Ushuhuda wa utume unafumbatwa katika misingi mikuu minne: Msaada kwa wahitaji; Sala kwa waliokata tamaa; Mshikamano kwa wale wanaoteseka; Kusali pamoja na Kanisa, ili kumngojea Roho Mtakatifu aweze kuwashukia Mitume wa Yesu! Shirika lilianzishwa na waamini wanne waliozamisha maisha yao kwa kujiweka wakfu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Wahudumu wa Bikira Maria, “Ordo Servorum Mariae”, kuanzia tarehe 7-27 Oktoba 2019 linaadhimisha Mkutano Mkuu wa Shirika wa 214 unao ongozwa na kauli mbiu “Wahudumu wa matumaini katika ulimwengu unaobadilika”. Mkutano mkuu ni fursa ya kufanya tathmini ya kina kuhusu maisha na utume wa Shirika. Ni wakati wa sala na tafakari; kupanga na kujiwekea sera na mikakati ya maisha na utume wa Shirika kwa siku za usoni. Wajumbe wa mkutano mkuu, Ijumaa tarehe 25 Oktoba 2019 amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Lengo ni kuweza kuwaimarisha katika imani; kuwatia shime katika ushuhuda na huduma kwa watu wa Mungu kwa kuiga mfano wa Bikira Maria. Ushuhuda wa utume unafumbatwa katika misingi mikuu minne: Msaada kwa wahitaji; Sala kwa waliokata tamaa; Mshikamano kwa wale wanaoteseka; Kusali pamoja na Kanisa, ili kumngojea Roho Mtakatifu aweze kuwashukia Mitume wa Yesu!

Baba Mtakatifu anasema, Shirika lilianzishwa kunako Karne ya XIII huko Firenze, nchini Italia na waamini wanne waliozamisha maisha yao katika biashara na majitoleo; kwa kujiweka wakfu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu. Wakajitahidi katika hija ya maisha yao kumwilisha tunu msingi za maisha ya Bikira Maria katika maisha na utume wao; wakaendeleza utume huu kwa kufundisha katika Kitivo cha Taalimungu cha Chuo Kikuu cha “Marianum”. Tunu msingi zinazobubujika kutoka katika maisha ya Bikira Maria ziwe ni chachu ya kujibu changamoto mamboleo zinazotolewa na Mama Kanisa na Shirika lao katika ujumla wake mintarafu kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Mkutano mkuu wa 214. Baba Mtakatifu anawaalika Wanashirika kupanda katika Mlima wa Bwana, ili kukutana na Kristo Yesu, chemchemi ya matumaini. Kama ilivyokuwa kwa waasisi wa Shirika, baada ya kupanda kwenda mjini Firenze, wawe na uthubutu wa kuteremka na kuwaendelea watu wale waliosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama vyombo na mashuhuda wa huduma kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Watawa wajitahidi kuishi mintarafu mwanga wa Injili kama ilivyokuwa siku ile Kristo Yesu alipong’aa uso wake mbele ya Mitume wake, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa matumaini kwa watu  wa nyakati hizi. Watawa wawe tayari “kufyekelea” mbali woga na wasi wasi unaoweza kuota mizizi yake hata katika maisha ya watawa kutokana na: uhaba wa miito; ukosefu wa uaminifu kwa Yesu, Injili na Kanisa. Kwa njia hii, wataweza kujisadaka zaidi kwa ajili ya kuchuchumilia utakatifu wa maisha kwa kuthamini na kuhimiza mwelekeo chanya katika jamii; kwa kuthamini na kudumisha upya unaobubujika kutoka katika tamaduni na maisha ya watu wanaowatangazia na kuwashuhudia Injili. Ili kuwa vyombo na mashuhuda wa matumaini wanapaswa kukoleza moyo wa majadiliano, umoja na udugu kama chemchemi ya utakatifu wa maisha. Watawa wawe na ujasiri wa kupambana na changamoto mamboleo kwa kuwa na matumizi sahihi na yanayowawajibisha kwa vyombo vya mawasiliano ya jamii; vinavyoweza wakati mwingine kuharibu utu na heshima ya watu; kwa kuchafua maisha ya kiroho pamoja na kujeruhi maisha ya kidugu katika jumuiya. Watawa wajitahidi kujifunza kutumia vyombo vya mawasiliano ya jamii kwa ajili ya kuinjilisha.

Jumuiya za kitawa ziwe ni maabara ya utamadunisho, kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaowafumbata watu wote bila ya ubaguzi, ili kupata maisha na uzima wa milele. Maisha ya kijumuiya yanachangamoto zake, lakini inawezekana kabisa kuishi kwa umoja na upendo katika jumuiya za kitawa, ikiwa kama watamwachia nafasi Roho Mtakatifu katika maisha yao, ili aweze kuwa ni chachu ya furaha ya maisha ya kijumuiya. Jumuiya zao za kitawa ziwe ni alama ya umoja wa kidugu duniani; shule za ukarimu zinazojengeka katika msingi wa mafungamano ya kijamii. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni changamoto na mwaliko wa kuondokana na kinzani, maamuzi mbele, tabia ya baadhi ya watawa kutaka “kujimwambafai” kwa kujikita katika: lugha, ukabila na utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko na hatimaye, kujenga kuta za utengano kati ya watu. Watawa wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa umoja, udugu na mshikamano kama walivyokuwa waasisi wa Shirika lao!

Papa: Matumaini

 

25 October 2019, 17:14