Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko: Furaha ya Injili ni chachu ya Uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Baba Mtakatifu Francisko: Furaha ya Injili ni chachu ya Uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. 

Papa Francisko: Furaha ya Injili, chachu ya uinjilishaji mpya!

Baba Mtakatifu anakazia maisha na utume wa Mtakatifu Don Bosco miongoni mwa vijana, kiasi kwamba, akafanikiwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili miongoni mwa vijana wa kizazi kipya! Utakatifu ulikuwa ni chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka katika maisha ya Kikristo kama anavyokaza kusema Mtakatifu Yohane Paulo II katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anawaalika waamini kujikita katika mchakato wa uinjilishaji mpya wenye mhuri wa furaha ambayo daima ni mpya na ambayo waamini wanapaswa kuwashirikisha jirani zao, baada ya kukutana na Kristo Yesu katika maisha yao. Hii ni furaha inayoinjilisha, inayopendeza na kufariji. Furaha ya Injili ni chachu ya kutangaza na kushuhdia imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu anakazia ari na mwamko wa kimisionari ndani ya Kanisa; mambo yanayopaswa kujikita katika shughuli za kichungaji zinazofumbatwa katika majadiliano, toba na wongofu wa kichungaji na kimisionari. Jumuiya za Kikristo zinapaswa kusoma alama za nyakati, tayari kujibu changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo, hasa uchu wa mali na madaraka; uvunjifu wa utu, heshima na haki msingi za binadamu; tayari kujikita katika mchakato wa utamadunisho na ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo, kwa kutambua kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wote wanashiriki: Unabii, Ufalme na Ukuhani wa Kristo Yesu. Kumbe, wote ni wafuasi wamisionari! Tafakari ya Neno la Mungu, Ibada kwa Bikira Maria, Katekesi ya kina na endelevu ni kati ya mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa! Anasema, mchakato wa uinjilishaji hauna budi kuwa na mwelekeo wa kijamii, kwa kukazia Mafundisho Jamii ya Kanisa; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kujikita katika kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Juhudi zote hizi zinakwenda sanjari na majadiliano ya kidini, kiekumene, kitamaduni na kisiasa ili kukuza uhuru wa kidini, utu na heshima ya binadamu! Huu ndio msukumo mpya wa wainjilishaji waliojazwa nguvu ya Roho Mtakatifu, kwa kuwa na ari na mwelekeo mpya wa kimisionari. Kwa ufupi haya ndiyo mawazo makuu yanayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amekubali kuandika utangulizi wa Kitabu kuhusu “Furaha ya Injili na Mtakatifu Don Bosco” kilichohaririwa na Padre Antonio Carriero. Hapa Baba Mtakatifu anakazia maisha na utume wa Mtakatifu Don Bosco miongoni mwa vijana, kiasi kwamba, akafanikiwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili miongoni mwa vijana wa kizazi kipya! Utakatifu ulikuwa ni chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka katika maisha ya Kikristo kama anavyokaza kusema Mtakatifu Yohane Paulo II katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Hii ni changamoto ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii kama alivyofanya Don Bosco kwa kuwasaidia vijana waliokuwa wanatoka katika familia maskini na wale waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu. Don Bosco aliweza kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, mitaani kati pamoja na vijana; magerezani kwa wafungwa; pamoja na kwenye maeneo ya kazi.

Huko akawafunda namna ya kuwa ni raia wema, waaminifu na watakatifu wa Mungu. Don Bosco katika maisha na utume wake, akajitahidi kuunda mazingira ya kifamilia yaliyokuwa na mvuto wa chemchemi ya utakatifu na furaha ya maisha; katika masomo na kazi, kiasi hata cha vijana wengi kujiamimisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, ni kati ya urithi mkubwa ambao Don Bosco amewaachia vijana wake, sanjari na upendo kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Francisko anawataka Wasalesiani wa Don Bosco kusoma alama za nyakati, kufanya mang’amuzi ya kina na kujibu kilio cha mahangaiko na matamanio halali ya vijana wa kizazi kipya. Wasalesiani wathubutu kutoka kifua mbele ili kuwaendelea wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na changamoto za kiuchumi, kifamilia na kitamaduni!

Hawa ni watu wenye madonda makubwa yanayopaswa kugangwa kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini; tayari kuwashirikisha katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Hii ndiyo falsafa ya Msamaria mwema, inayopaswa kumwilishwa katika maisha na utume kwa vijana. Wasalesiani wa Don Bosco, wawe ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Huyu ndiye Kristo anaendelea kujifunua kati ya maskini na wale wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ndio ushuhuda amini na endelevu unaotolewa na watakatifu kutoka katika familia ya Don Bosco. Ni watu ambao wamewaachia wengine chapa ya upendo na huruma ya Mungu katika akili na nyoyo zao. Karama ya Wasalesiani inajikita katika huduma ya elimu, dira na mwongozo kwa vijana ili kupambana na hali pamoja na mazingira yao, ili ulimwengu uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Papa: Furaha ya Injili

 

 

23 October 2019, 16:48