Baba Mtakatifu Francisko ametuma salam na matashi mema kwa Jumuiya ya Waamini wa Dini ya Kiyahudi mjini Roma. Baba Mtakatifu Francisko ametuma salam na matashi mema kwa Jumuiya ya Waamini wa Dini ya Kiyahudi mjini Roma. 

Papa Francisko: Salam na matashi mema kwa Wayahudi wa Roma

Sherehe hizi ziwe ni chemchemi ya neema na baraka kutoka kwa Mungu, anayependa kuwakirimia watu wake: furaha na amani ya ndani. Mungu anayewapenda wale wote wanaojiaminisha kwake, na kuwasindikiza katika hija ya maisha yao, awasaidie waamini wote kumshuhudia kwa njia ya huduma kwa jirani zao, kwa kuendelea kujikita katika kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waamini wa dini ya Kiyahudi kila mwaka husherehekea Siku kuu ya Rosh Ha-Shanah, yaani Mwanzo wa Mwaka Mpya wa Kiyahudi. Hizi ni sherehe zinazoambatana na Siku kuu ya Yom Kippur, yaani: Sherehe ya toba na utakaso wa dhambi na hatima ya sherehe zote hizi ni Siku kuu ya Sukkot, yaani Sherehe ya vibanda ambayo inafahamika zaidi kuwa ni Sherehe ya mavuno. Kwa mwaka huu, sherehe hizi zote zinaadhimishwa kuanzia tarehe 13 Oktoba hadi tarehe 20 Oktoba. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amewatumia ujumbe wa matashi mema waamini wa dini ya Kiyahudi wanaoishi mjini Roma. Ujumbe huu umetumwa kwa Rabbi Riccardo Di Segni, Mkuu wa Jumuiya ya Wayahudi mjini Roma.

Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini, anapenda kutuma salam na matashi mema katika maadhimisho haya, ili yaweze kuwafikia waamini wote wa dini ya Kiyahudi, sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa kusema kamba, Sherehe hizi ziwe ni chemchemi ya neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, anayependa kuwakirimia waja wake ile furaha na amani ya ndani. Mwenyezi Mungu anayewapenda wale wote wanaojiaminisha kwake, na kuwasindikiza katika hija ya maisha yao, awasaidie waamini wote kumshuhudia kwa njia ya huduma kwa jirani zao, kwa kuendelea kujikita katika kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani!

Papa: Wayahudi
08 October 2019, 14:41