Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na Watawa wa Shirika la Ndugu Wafrancisko Wakapuchini kutoka Kanda ya Marche, Italia amekazia ushuhuda wa maisha! Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na Watawa wa Shirika la Ndugu Wafrancisko Wakapuchini kutoka Kanda ya Marche, Italia amekazia ushuhuda wa maisha! 

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Ndugu Wafrancisko Wakapuchini

Papa amekazia kuhusu: Wito kutoka kwa Mwenyezi Mungu unaofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; changamoto za kimisionari kutokana na uhaba wa miito; tatizo la watawa kukengeuka, umuhimu wa Wakapuchini kukita maisha na utume wao katika Katiba ya Shirika; Ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu; pamoja kuwa na mvuto kwa vijana wa kizazi kipya.! UFUKARA!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 10 Oktoba 2019 amekutana na kuzungumza na Shirika la Ndugu Wafransisko Wakapuchini kutoka Kanda ya Marche, iliyoko nchini Italia. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia zaidi kuhusu wito kutoka kwa Mwenyezi Mungu unaofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; changamoto za kimisionari kutokana na uhaba wa miito; tatizo la watawa kukengeuka na kumezwa na malimwengu; umuhimu wa Wakapuchini kukita maisha na utume wao katika Katiba ya Shirika; umuhimu wa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu; pamoja na kuendelea kuwa ni mashuhuda wenye mvuto kwa vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu amepata fursa ya kuzungumza na ndugu zake Wakapuchini katika hali ya kawaida na udugu wa kibinadamu, kwa kukazia kuhusu jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anawaita waja wake kwa namna mbali mbali, akiwataka kutubu na kumwongokea, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu amewakumbusha kwamba, nguvu yao inasimikwa katika ushuhuda wa furaha. Amewataka Wakapuchini kujisadaka na kujiachia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao, vinginevyo, watakuwa ni watu wenye kuimba litania ya manung’uniko na ukosefu wa haki, hali ambayo kimsingi inakwenda kinyume cha wongofu wa ndani. Maisha ya kijumuiya yanafumbatwa katika wongofu endelevu na unyenyekevu, ari na utambulisho wa Wafranciskani. Kanisa linakabiliwa na uhaba mkubwa wa Wamisionari wanaopaswa kutoka kifua mbele kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Kwa kuwekwa wakfu kama watawa, wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa ni mashuhuda wanaotangaza na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo. Hakuna sababu ya wongofu wa shuruti ndani ya Kanisa. Watu wavutwe na ushuhuda wa matendo makuu ya Mungu katika maisha ya waja wake.

Wakapuchini wamtangaze Kristo Yesu Mfufuka kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Huu ni ushuhuda kama ule uliotolewa na Mama Theresa wa Calcutta. Wakapuchini watoe ushuhuda wao kwa njia ya nadhiri ya ufukara unaomwilishwa katika unyenyekevu na kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu. Baba Mtakatifu anasema, Shetani, Ibilisi anaweza kuwachanganya  na kuwavuruga kwa kutumia fedha, mali na vitu! Ufukara ni mama na ukuta wa maisha na utume wa kitawa. Baba Mtakatifu anawataka watawa wajizatiti zaidi kwa kusimama kidete kupambana na malimwengu, ili kamwe wasitumbukie huko kwani watalia na kusaga meno! Kristo Yesu alitambua madhara ya waja wake kumezwa na malimwengu, ndio maana akawaombea waishi kwa kutambua kwamba, wao wanaishi ulimwengu humu, lakini si wa ulimwengu huu. Wafranciskani wawe kweli ni wachungaji, wahudumu wa mafumbo na viongozi bora wa Kanisa. Huduma yao isaidie kuboresha maisha ya watu wa Mungu.

Wakapuchini wajitahidi kuhakikisha kwamba, wanafuata kikamilifu Katiba ya Shirika lao, ili kujenga na kudumisha umoja na udugu kielelezo cha nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu. Wakapuchini wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake; daima wakijitahidi kusamehe na kusahau. Wawasaidie waamini kwa njia ya Sakramenti ya Kitubio, kuweza kujipanisha na Mungu pamoja na jirani zao, lakini watambue pia kwamba, wao ni wadhambi ambao wamepata upendeleo wa pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Huruma na upendo ni nyenzo msingi katika mchakato wa uinjilishaji unaoliwezesha Kanisa kupata watoto wapya wanaozaliwa kwa Maji na Roho Mtakatifu katika Sakramenti ya Ubatizo. Kuna wanawake waliofundwa kikamilifu katika tunu msingi za maisha ya Kikristo kutoka nchi kama Ufilippini, wanaofanya kazi za nyumbani, lakini wamekuwa ni makatekista wa kwanza kwa watoto kutoka kwenye familia tajiri Barani Ulaya. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha hotuba yake kwa kulitaka Shirika la Ndugu Wafransisko Wakapuchini kuwa ni shuhuda kwa vijana wa kizazi kipya.

Kwa upande wake, Padre Sergio Lorenzini, Mkuu wa Kanda, Shirika la Ndugu Wafransisko Wakapuchini kutoka Marche, amesema, panapo majaliwa kunako mwaka 2028, Shirika litakuwa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 500 tangu kuanzishwa kwake. Wamemzawadia Baba Mtakatifu zawadi mbali mbali kutoka Afrika na Marche ambako amekwisha kutembelea mara mbili ili kuwatia shime waathirika wa tetemeko la ardhi nchini Italia.

Papa: Wakapuchini

 

11 October 2019, 17:09