Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi yake tarehe 16 Oktoba 2019 amekutana na watu mbalimbali na kusalimiana nao Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi yake tarehe 16 Oktoba 2019 amekutana na watu mbalimbali na kusalimiana nao  (Vatican Media)

Papa Francisko:Mtakatifu Luka anaonyesha vizuri moyo na huruma ya Yesu!

Mara baada ya katekesi yake,katika salam mbalimbali kwa mahujaji na waamini wote kutoka pande zote za Dunia,amewakumbusha juu ya Sikukuu ya Mtakatifu Luka mwinjili,inayofanyika tarehe 18 Oktoba na kwamba Mt.Luka anaonyesha vizuri roho na huruma ya Yesu,kwa maana hiyo awasaidie kugundua furaha ya kuwa wakristo na mashuhuda wa mema ya Mungu.

Na Sr. Angela Rwezaula –Vatican

Mara baada ya katekesi yake Baba Mtakatifu Francisko kama kawaida yake ya kuwakaribisha mahujaji wote toka pande za dunia, pia  kutoa hata ujumbe mbalimbali kulingana na lugha zao, amewasalimia wote, lakini kwa namna ya pekee anawakumbuka vijana, wazee, wagonjwa na wanandoa wapya waliokuwapo wote na wanaofuatilia katika vyombo vya habari.

Sikukuu ya Mtakatifu Luka

Baba Mtakatifu Francisko pia amekumbusha waamini wote ya kuwa tarehe 18 Oktoba ni Sikukuu ya Mwinjili Luka ambaye anasema, anaonyesha vizuri moyo wa Yesu na huruma yake. Katika maadhimisho ya siku hiyo awasaide wote ili  kugundua furaha ya kuwa wakristo, mashuhuda wa wema wa Mungu.

Kazi ya Mungu

Mtakatifu Luka alizaliwa huko Antiokia,wakati huo chini ya utawala wa dola ya Warumi.Tukisoma katika Wakolosai 4:14, tunagundua pia kuwa Mtakatifu Luka alikuwa tabibu. Inaonesha wazi kwamba Mtakatifu Luka, alifuatana na mtume Paulo, kwenda sehemu mbalimbali kufanya uinjilishaji (rej Philemon 1:24). Na katika  barua ya 2 Tim 4: 11 tunaona hata   tabu zote alizokumbana nazo, lakini pamoja na hayo yote Mtakatifu Luka, hakumwacha Mtakatifu Paulo peke yake. Ili kujua mengi zaidi katika Biblia kwenye Agano jipua tunaona jinsi gani Mtakatifu  Luka alivyoandika miujiza mbalimbali ya Kristo, na ambayo haikuandikwa katika Injili zingine mbili zinazofanana na Injili yake.Pia katika Injili ya Mtakatifu Luka tunakutana  na maandiko kuhusu Mama Maria, na ambayo mambo mengi  hayapatikani katika Injili nyingine kama vile “Salamu Maria” kutoka kwa Malaika.  Mtakatifu Luka pamoja na kuandikia Injili ndiye anasadikiwa kuwa mwandishi wa kitabu cha Matendo ya Mitume.

Kitabu cha Matendo ya Mitume

Kinajulikana kwa jina hilo, kwa kuwa kinawatokeza hasa watu wawili ambao mwandishi aliwafahamu na kupenda kuwaenzi, yaani Petro mpaka sura ya 12, halafu Paulo. Kwa namna ya pekee alikuwa mwanafunzi wa Paulo akamfuata mpaka kifo chake: hivyo si ajabu kwamba alipenda kushuhudia kazi zake na mateso yake kwa ajili ya Yesu Kristo na uenezi wa imani. Mbali ya watu hao wawili, kitabu kinataja mwanzoni majina ya mitume 11 waliobaki baada ya kifo cha Yuda Iskarioti na kueleza jinsi Mtume Mathia alivyoshika nafasi yake, lakini hakuna habari zaidi juu ya wengi wao. Na kumbe kuna habari nyingi juu ya Wakristo wengine wa kwanza, hasa Stefano na Filipo. Pamoja na hayo, yote Mtakatifu Luka anasisitiza kuwa mhusika na mtendaji mkuu wa ustawi wa Kanisa si binadamu yeyote yule, hata kama ni shujaa, bali ni Mungu tu!

16 October 2019, 12:39