Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anasema, anafuatllia kwa hofu na mashaka makubwa machafuko ya kisiasa nchini Chile, anawataka wadau kuanza mchakato wa majadiliano. Baba Mtakatifu Francisko anasema, anafuatllia kwa hofu na mashaka makubwa machafuko ya kisiasa nchini Chile, anawataka wadau kuanza mchakato wa majadiliano.  (AFP or licensors)

Papa Francisko anafuatilia kwa makini hali tete ya kisiasa Chile

Ni matumaini ya Papa Francisko kwamba, wadau wote wanaohusika watasitisha maandamano ambayo yamekwisha sababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao na kuanza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi. Baba Mtakatifu anawasihi wadau wote kutafuta suluhu ya kudumu ili kuokoa maisha ya watu dhidi ya mateso wanayokabiliana nayo kwa wakati huu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake Jumatano, tarehe 23 Oktoba 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewaambia mahujaji na wageni kwamba, anafuatilia kwa wasi wasi mkubwa hali tete ya Chile kwa wakati huu. Ni matumaini yake kwamba, wadau wote wanaohusika watasitisha mara moja maandamano ambayo yamekwisha sababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao na kuanza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi. Baba Mtakatifu anawasihi wadau wote kutafuta suluhu ya kudumu ili kuokoa maisha ya watu dhidi ya mateso wanayokabiliana nayo kwa wakati huu.

Taarifa kutoka Chile zinaonesha kwamba,  waandamanaji katika miji mbali mbali nchini humo wamebomoa na kuchoma maduka makubwa makubwa. Hadi sasa zaidi ya watu 13 wamekwisha kupoteza maisha na wengine 240 kujeruhiwa vibaya. Serikali imetangaza hali ya hatari na kwamba, hali ngumu na ukata ni kati ya mambo yaliyowakasirisha watu na kuanza kufanya maandamano dhidi ya Serikali. Katika miaka ya hivi karibuni, nchini Chile, kumeibuka matabaka ya watu wachache wanaohodhi utajiri mkubwa wa nchi na kundi la maskini, licha ya Chile kuwa ni kati ya nchi zenye uchumi mzuri kwenye Nchi za Amerika ya Kusini.

Papa: Chile
23 October 2019, 14:56