Vatican News
2019.10.14 Papa Giani 2019.10.14 Papa Giani 

Papa aitembelea Familia ya Domenico Giani nyumbani kwake!

Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na Bwana Domenico Giani na familia yake. Amemshukuru kwa huduma, uhuru wake wa ndani na uwajibikaji, kama kielelezo cha heshima na huduma inayotolewa na vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican. Amemshukuru kwa unyenyekevu, moyo wa sadaka na majitoleo kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kipindi chote cha miaka 20.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumanne jioni, tarehe 15 Oktoba 2019 mara baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yanaongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani” alikwenda kumtembelea nyumbani kwake, Kamanda Mkuu Mstaafu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama mjini Vatican, Bwana Domenico Giani, aliyejiuzuru kwa hiyari yake mwenyewe kufuatia kashfa ya kuvuja kwa nyaraka za siri kuhusu baadhi ya watuhumiwa waliojihusisha na ubadhirifu wa fedha ya Kanisa, waliokuwa wamesimamishwa kazi ili kupisha mchakato wa uchunguzi dhidi ya shutuma zilizokuwa zinawakabili. Kitendo hiki kimevuta hisia kubwa kwa watu wengi na kumwona kweli Bwana Domenico Giani amefanya maamuzi magumu katika maisha yake, kielelezo cha upendo na uaminifu kwa Kanisa la Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu aliweza kukutana na kuzungumza kwa faragha na Bwana Domenico Giani, mke wake na binti yao.

Baba Mtakatifu ametumia nafasi hii kumshukuru kwa huduma, uhuru wake wa ndani na uwajibikaji, kama kielelezo cha heshima na huduma inayotolewa na vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican. Amemshukuru kwa unyenyekevu, moyo wa sadaka na majitoleo kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kipindi chote cha miaka 20 ya utumishi wake mjini Vatican. Daima ameonesha uaminifu, ukweli na uwazi na kwa hakika, amekuwa ni shuhuda wa huduma iliyotukuka kwa Kanisa na kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni kiongozi aliyeaminiwa na Baba Mtakatifu kiasi cha kujenga upendo na urafiki wa dhati. Amemshukuru kwa huduma zake ndani na nje ya Vatican, kazi ambayo ameifanya kwa nidhamu, weledi na uaminifu mkubwa. Wakati huo huo, Bwana Domenico Giani katika mahojiano maalum na Vatican News katika kipindi hiki tete cha maisha na utume wake anasema, amefanya maamuzi haya magumu  katika hali ya utulivu, akiwa ametiwa shime na imani kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko aliyomwonesha katika kipindi chote cha utume wake hapa mjini Vatican.

Kamanda Mstaafu Domenico Giani ni kiongozi ambaye kwa muda wa miaka 38 amekuwa katika “viwanja vya ulinzi na usalama”, kwanza kabisa nchini Italia na baadaye kwa miaka 20 mjini Vatican. Amekiri na kusema kwamba, ametumia karama, ujuzi na weledi wake kwa ajili ya kutekeleza dhamana na majukumu aliyokuwa amekabidhiwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro, kiasi hata cha kujisikia kuwa ni “Mtumishi asiyekuwa na faida, daima alitenda kile alichopaswa kutenda tu”.

Papa: Familia ya Giani
16 October 2019, 11:12