Tafuta

Katekesi: Safari ya Injili Duniani. Mtakatifu Paulo, Mtume na mwalimu wa Mataifa ni chombo kiteule cha Mungu kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Katekesi: Safari ya Injili Duniani. Mtakatifu Paulo, Mtume na mwalimu wa Mataifa ni chombo kiteule cha Mungu kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. 

Katekesi: Safari ya Injili Duniani: Sauli: Chombo kiteule cha Mungu

Mtume Paulo ni mfano bora wa waamini waliokutana na Kristo Mfufuka wakajizatiti katika utumishi kwa Mungu, huduma ya Neno na matendo ya huruma kwa jirani. Hii ni changamoto kwa waamini kuomba toba na wongofu wa ndani ili kuwaongoa wale wote wanaoendelea kuwatesa na kuwadhulumu Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, kwa kudhani wanatekeleza mapenzi ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mzunguko wa Katekesi kuhusu Safari ya Injili Ulimwenguni mintarafu Kitabu cha Matendo ya Mitume ni fursa ya kupembua: mchango wa Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa la Mwanzo na uwepo wa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, uliozindua mchakato mzima wa uinjilishaji. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, siku ya Jumatano, tarehe 9 Oktoba 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amechambua kuhusu wito wa Sauli aliyelidhulumu Kanisa la Kristo na hatimaye, akamwongokea Kristo Yesu na kuwa ni “chombo kiteule cha Mungu” ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, lakini pia atapaswa kuteswa kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Fundisho kuu linalotolewa na Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa ni kwamba, wale wote wanaobahatika kukutana na Kristo Mfufuka wanapata mabadiliko ya ndani katika maisha yao. Mtume Paulo ni mfano bora wa wale waamini waliokutana na Kristo Mfufuka wakajizatiti katika utumishi kwa Mungu, huduma ya Neno na matendo ya huruma kwa jirani.

Hii ni changamoto kwa waamini ili waweze kumwomba Mwenyezi Mungu zawadi ya toba na wongofu wa ndani, ili kuwaongoa wale wote wanaoendelea kuwatesa na kuwadhulumu Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, kwa kudhani kwamba, kwa kutenda vile, wanatekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu wakati wa Katekesi yake amefafanua kwamba, tangu siku ile Mtakatifu Stefano, Shahidi “alipotwangwa kwa mawe” hadi kufa, Sauli alikuwa akiona vyema kwa kuuwawa kwake na akawa amedhamiria kuliharibu Kanisa, akiingia katika kila nyumba, na kuwaburuta watu na kuwatupa gerezani. Lakini Sauli mtesi, akageuka kuwa ni chombo kiteule cha Mungu ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Sauli alipewa kibali na Kuhani mkuu ili “kuwasaka na kuwafundisha adabu”, akidhani kwamba, alikuwa anasimama kidete kulinda na kutetea Sheria ya Bwana. Aliwaza ndani mwake jinsi ya kuwauwa Mitume wa Yesu, akagubikwa mawazo ya mauaji na wala si maisha tena!

Sauli, hakuwa ni mtu mwenye huruma kwa wale wote waliokuwa kinyume cha mawazo, utambulisho, siasa na imani yake, hali ambayo hadi sasa inawapekenya baadhi ya watu duniani anasema Baba Mtakatifu Francisko. Sauli akachanganya kati ya masuala ya kidini, kisiasa na kijamii. Ni baada ya toba na wongofu wa ndani, kwa kukutana na Kristo Mfufuka, ataweza kuwafundisha watu kwamba, wanapaswa kushindana katika imani na wala si juu ya damu na nyama. Wanapaswa kushindana juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza, juu ya majeshi ya pepo wabaya. Kimsingi wanapaswa kupambana na uovu na wala si watu. Baba Mtakatifu anasema, hii ni changamoto kwa Wakristo wote kujiuliza jinsi ambavyo wanajitahidi kuuishi Ukristo wao; kama kweli wanataka kujenga utamaduni wa kukutana na wengine, au kwenda kinyume cha jirani zao. Watu wema na wabaya, ni sehemu ya maisha ya Kanisa; kwani kuna wale wanao mwabudu Mungu wa kweli katika uhalisia wa maisha yao na kuna wale ambao wamebaki kwenye vitabu, kiasi cha kushindwa kuungama na kuimwilisha imani yao katika matendo, kielelezo cha imani tendaji.

Huu ni mwaliko wa kujenga na kudumisha utamaduni wa maridhiano hata na wale ambao wanatofautiana kwa mambo msingi. Wakati Sauli akiendelea kuwatenda jeuri Wakristo, Kristo Mfufuka alikuwa “anakula naye sahani moja”, akiwa njiani kwenda Dameski, Kristo Mfufuka akagusa undani wa maisha yake, akatubu na kumwongokea, baada ya kuona mwanga na sauti ya ufunuo wa Kristo Mfufuka, anayejiambatanisha na wafuasi wake, kama sehemu ya Fumbo la Mwili wake. Sauli akapelekwa mjini Dameski huku akiwa anaongozwa njiani. Sauli aliyekuwa jeuri, mbabe, mwenye nguvu na mtu aliyejiamini kupita kiasi akanyong’onyea na kuwa mdogo kuliko hata “kidonge cha piliton”, akawa tegemezi kwa wengine kutokana na upofu wake uliokuwa umekita mizizi katika undani wa maisha yake, kiasi hata cha kushindwa kuona ukweli na mwanga halisi wa maisha, ambao kimsingi ni Kristo Yesu.

Sauli baada ya kukutana mubashara na Kristo Mfufuka, anaanza hija ya Pasaka binafsi, ili kumtafuta na kumwambata Kristo Mfufuka, chemchemi ya maisha mapya. Sauli akabatizwa na kupewa jina jipya, Paulo, mwanzo wa maisha mapya, uso wa huruma na upendo wa Mungu kwake, ukamsaidia kuwaona na kuwathamini wengine, ili kujenga na kudumisha umoja na urafiki ndani ya Kristo na hivyo kuondokana na dhana ya uadui. Mwishoni mwa Katekesi yake, Baba Mtakatifu amewasihi wamini kumwachia Mungu nafasi kama ilivyokuwa kwa Sauli, ili waonje huruma na upendo wake katika maisha yao, ili kubadilisha moyo wa jiwe uweze kuwa ni moyo wa nyama, ili kupokea na kukumbatia mawazo ya Kristo Mfufuka katika maisha yao!

Papa: Wongofu wa Sauli
09 October 2019, 14:31