Tafuta

Papa Francisko wakati wa Katekesi yake amefafanua kuhusu umuhimu wa Mtaguso wa Yerusalemu katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa uinjilishaji. Papa Francisko wakati wa Katekesi yake amefafanua kuhusu umuhimu wa Mtaguso wa Yerusalemu katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa uinjilishaji. 

Katekesi: Safari ya Injili Duniani: Mtaguso wa Yerusalemu

Katika mchakato wa uinjilishaji yakazuka mabishano huko Antiokia juu ya tohara na utatuzi wa mabishano haya ni maadhimisho ya Mtaguso wa Yerusalemu. Mtume Petro akashuhudia kwa ujasiri jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu alivyomtumia kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Watu wa Mataifa wakasikia Neno la Mungu na Roho Mtakatifu akawashukia na kukaa juu yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtume Paulo ni mfano bora wa waamini waliokutana na Kristo Mfufuka wakajizatiti katika utumishi kwa Mungu, huduma ya Neno na matendo ya huruma kwa jirani. Hii ni changamoto kwa waamini kuomba toba na wongofu wa ndani ili kuwaongoa wale wote wanaoendelea kuwatesa na kuwadhulumu Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, kwa kudhani kwamba, wanatekeleza mapenzi ya Mungu. Mzunguko wa Katekesi kuhusu Safari ya Injili Ulimwenguni mintarafu Kitabu cha Matendo ya Mitume ni fursa ya kupembua: mchango wa Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa la Mwanzo na uwepo wa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, uliozindua mchakato mzima wa uinjilishaji unaoendelezwa na Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 23 Oktoba 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amefafanua kuhusu mambo makuu ambayo Mwenyezi Mungu aliwatendea Mitume wake Paulo na Barnaba na ya kwamba, amewafungulia Mataifa mlango wa imani. Katika mchakato wa uinjilishaji yakazuka mabishano huko Antiokia juu ya tohara na utatuzi wa mabishano haya ni maadhimisho ya Mtaguso wa Yerusalemu. Mtume Petro akashuhudia kwa ujasiri jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu alivyomtumia kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Watu wa Mataifa wakasikia Neno la Mungu na Roho Mtakatifu akawashukia na kukaa juu yao. Watu wanaokolewa kwa neema ya Mwenyezi Mungu.

Kitabu cha Matendo ya Mitume ni Kitabu kinachoonesha safari ya Neno la Mungu linalotangazwa na kushuhudiwa sehemu mbali mbali za dunia. Madhulumu, vikwazo na kinzani, zinakuwa ni fursa ya kufafanua, kupandikiza na kueneza mbegu ya Neno la Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Mitume Paulo na Barnaba wanakaa Antiokia na Siria kwa muda wa mwaka mmoja, wakafundisha pamoja na kusaidia mchakato wa Jumuiya za Kikristo kuzamisha mizizi yake katika maisha ya watu wa Mungu. Antiokia ikageuka kuwa ni Kitovu cha Uinjilishaji na kwa mara ya kwanza wanafunzi waliitwa Wakristo hapo Antiokia. Ni katika Kitabu cha Matendo ya Mitume, asilia ya Kanisa inaibuliwa kwa kuonesha kwamba, liko kwa ajili ya kuinjilisha, kwa kuwatangazia na kuwashirikisha watu wote ile furaha ya Injili bila ubaguzi.

Hili ni Kanisa ambalo malango yake yako wazi kwa ajili ya watu wote, changamoto na mwaliko kwa Wakleri kuhakikisha kwamba, wanaacha malango ya Makanisa yao wazi, ili waamini waende humo ili kukutana na Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko anasema, malango ya Kanisa yalikuwa wazi kwa Wayahudi, lakini kwa njia ya neema na baraka, Mwenyezi Mungu akawafungulia pia wapagani mlango wa imani, hali ambayo ilisababisha mabishano makubwa, kwa kuwataka wapagani kwanza kabisa kutahiriwa kadiri ya desturi ya Musa, ndipo waokoke. Hotuba ya Mtakatifu Petro na Mtume Yakobo, nguzo za Mama Kanisa, ikasaidia kuweka mambo msingi yanayopaswa kufuatwa na wale wote wanaomwongokea Mwenyezi Mungu yaani: wajiepushe na unajisi wa sanamu, uasherati, nyama zilizosongelewa na damu.

Baada ya mabishano makali, Mitume wakapatana na kuanza kutembea njia ya umoja na mshikamano, kwa maamuzi haya kuwekwa katika Waraka wa Mtaguso wa Yerusalemu na kutumwa kwenda Antiokia. Mtaguso wa Yerusalemu ni kielelezo makini cha Kanisa jinsi ya kushughulikia matatizo na changamoto za maisha na utume wa Kanisa kwa kuzingatia ukweli katika upendo unaofumbatwa katika majadiliano; kwa kusikilizana na hatimaye, kufanya mang’amuzi chini ya mwanga wa Roho Mtakatifu anayewasaidia kupata mwelekeo mpya wa maisha unaosimikwa katika umoja wa Kanisa. Kwa njia ya nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, Kanisa likaanza kupata cheche za Sinodi katika maisha na utume wake. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili awasaidie Wakleri kuwajibika barabara katika mchakato wa ujenzi wa umoja unaofumbatwa katika majadiliano, kwa kukutana na kusikilizana kama ndugu wamoja katika imani, ili Kanisa liendelee kuwa ni chemchemi ya furaha kwa watoto wake!

Mtaguso wa Yerusalemu

 

23 October 2019, 15:28