Kardinali Adam Kozlowiecki, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Lusaka Zambia, alisadaka maisha yake kwa miaka 60 kwa ajili ya utume wa kimisionari nchini Zambia. Kardinali Adam Kozlowiecki, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Lusaka Zambia, alisadaka maisha yake kwa miaka 60 kwa ajili ya utume wa kimisionari nchini Zambia. 

Hayati Kardinali Adam Kozlowiecki: Mmisionari, Lusaka, Zambia!

Kardinali Adam Kozłowiecki alijisadaka kwa ajili ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Akajenga Makanisa, Shule, Hospitali na Vituo vya wazee, watoto yatima na wale waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu. Mfano wa maisha na utume wake, uwe ni changamoto kwa waamini kufungua macho na masikio yao ili kusikiliza na kujibu kilio cha maskini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake baada ya Katekesi, Jumatano tarehe 23 Oktoba 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, amewashukuru na kuwapongeza wale wote walioandaa Onesho la maisha ya Kardinali Adam Kozłowiecki, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Lusaka, Zambia, lililozinduliwa rasmi tarehe 22 Oktoba 2019 kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, kilichoko mjini Roma. Huyu ni kiongozi wa Kanisa aliyeonja suluba mara baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Akafungwa kwenye kambi ya mateso ya Auschwitz na miezi sita baadaye akahimishwa kwenye kambi ya mateso ya Dachau. Kwa miaka 60 akatangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mungu Barani Afrika, lakini zaidi nchini Zambia. Alisimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Kardinali Adam Kozłowiecki akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Akajenga Makanisa, Shule, Hospitali na Vituo vya wazee, watoto yatima na wale waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu. Mfano wa maisha na utume wake, uwe ni changamoto kwa waamini kufungua macho na masikio yao ili kusikiliza na kujibu kilio cha maskini. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Adam Kozłowiecki alizaliwa kunako tarehe 1 Aprili 1911 huko nchini Poland. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kitawa na Kikasisi kama Myesuiti, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 24 Juni 1937. Tarehe 4 Juni 1955 akateuliwa kuwa Askofu na kuwekwa wakfu tarehe 11 Septemba 1955.

Tarehe 25 Aprili 1959 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa kwanza wa Jimbo kuu la Lusaka nchini Zambia. Baada ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo kuu la Lusaka kwa takribani miaka 10, akaona kwamba, kulikuwa na haja ya kuwaachia Maaskofu wazalendo kuanza kushika usukani wa uongozi wa Kanisa kama sehemu ya utekelezaji wa changamoto za maisha na utume wa Kanisa zilizoibuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Kutokana na muktadha huu, mwaka 1969 akang’atuka kutoka madarakani na kuendelea na utume wake nchini Zambia kama Mmisionari. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa na kumsimika kuwa Kardinali tarehe 21 Februari 1998. Akafariki dunia tarehe 28 Septemba 2009 akiwa Jimbo kuu la Lusaka, nchini Zambia.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na mahujaji na wageni kutoka Poland amewakumbusha kwamba, tarehe 22 Oktoba 2019 ameadhimisha kumbu kumbu ya Mtakatifu Yohane Paulo II, changamoto na mwaliko wa kumuiga Mtakatifu Yohane Paulo II, mwalimu wa imani, maisha ya Kiinjili na mfano wa upendo kwa Kristo Yesu pamoja na watu wote wa Mungu. Baba Mtakatifu katika maadhimisho ya Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba, 2019, Mwezi huu maalum kwa ajili ya kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari anawaombea waamini kujikita katika mchakato wa majadiliano; kwa kujenga utamaduni wa kukutana, kujadiliana na kusikilizana katika ukweli na uwazi; ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa upendo wa Mungu kwa waja wake. Ni mwaliko kwa mahujaji wote kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Kardinali Adam

 

23 October 2019, 15:09