Papa Francisko asema, kilio cha maskini na kilio cha watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia kimewafikia Mababa wa Sinodi. Papa Francisko asema, kilio cha maskini na kilio cha watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia kimewafikia Mababa wa Sinodi. 

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Kilio cha maskini Amazonia

Mababa wa Sinodi wamepata nafasi ya kusikiliza kilio cha maskini; kutafakari hali ya maisha yao tete, yanayotishiwa na mifumo tenge ya maendeleo pamoja na kusikiliza kilio cha Dunia Mama. Haiwezekani kabisa watu wakajifanya kana kwamba, hawakusikiliza kilio cha Mababa wa Sinodi, kilio cha viongozi wa kidini, vijana na wanasayansi, wanaowachangamotisha watu kuwajibika!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumapili, tarehe 27 Oktoba 2019 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ili kufunga rasmi maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yaliyokuwa yanaongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Baba Mtakatifu wakati wa Tafakari kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amesema kwamba, Sala ya Maskini na dua yake itafika hima mbinguni, lakini sala na dua ya mtu mwenye kiburi, inabaki hapa hapa duniani kwa kumezwa na ubinafsi. Maskini ni watu ambao wamekita maisha yao katika hali ya unyenyekevu kwa kumpatia Mwenyezi Mungu nafasi ya kwanza kama amana na utajiri wao wa maisha ya kiroho. Katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, Mababa wa Sinodi wamepata nafasi ya kusikiliza kilio cha maskini; kutafakari hali ya maisha yao tete, yanayotishiwa na mifumo tenge ya maendeleo pamoja na kusikiliza kilio cha Dunia Mama.

Baada ya maadhimisho ya Sinodi kwa muda wa majuma matatu, haiwezekani kabisa watu wakajifanya kana kwamba, hawakusikiliza kilio cha Mababa wa Sinodi, kilio cha viongozi wa kidini, vijana na wanasayansi, wanaowachangamotisha watu wa Mataifa kuwajibika barabara kabla ya mambo hayajaharibika zaidi. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kufafanua maana ya “Sinodi” kuwa ni mchakato wa kutembea bega kwa bega na kwa ujasiri huku wakiwa wanafarijiwa na Mwenyezi Mungu. Mababa wa Sinodi wametembea bega kwa bega huku wakiangaliana machoni; wakasikilizana katika misingi ya ukweli na uwazi; wakabainisha matatizo, changamoto na fursa zilizopo Ukanda wa Amazonia; wakiwa tayari kusonge mbele, huku wakiwa wameungana kwa ajili ya kutumikia. Baba Mtakatifu amefanya rejea kwenye Waraka wa Pili wa Mtakatifu Paulo kwa Timotheo, akiwa anakiona kifo mbele yake, anamwandikia Timotheo kwamba “sasa alikuwa yuko tayari kumiminwa na wakati wa kufariki kwake ulikuwa umewadia”.

Katika hali ya majonzi na masikitiko makubwa anasema, Bwana alisimama pamoja naye na kumtia nguvu, ili kwa kazi yake, ujumbe wa Injili upate kutangazwa kwa utimilifu hata wasikie Mataifa yote. Mtakatifu Paulo mwishoni mwa maisha yake anatamani kuona kwamba, Injili inatangazwa na kushuhudiwa kwa watu wote wa Mataifa. Waamini wanakumbushwa kwamba, siku ya mwisho wataulizwa mema waliyotenda kwa ajili ya maisha yao. Ni wakati muafaka kwa kila mwamini kujiuliza, Je, amefanya kitu gani kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili? Haya ni kati ya maswali msingi ambayo Mababa wa Sinodi wamejiuliza, wakiwa na nia ya kuona Kanisa linafungua njia mpya kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa. Ikumbukwe kwamba, Injili inatangazwa kwa ukamilifu zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Kumbe, haya ni maisha yanayojikita kwa Kristo Yesu pamoja na Injili, kwa kujitahidi kutoka katika ubinafsi.

Mababa wa Sinodi wamehisi ndani mwao, kuchangamotishwa kutoka na kutweka hadi kilindini, si katika maji yaliyochafuliwa kwa tope za ukoloni wa kiitikadi, bali ni ile bahari ambayo Roho Mtakatifu anawaalika waamini kutupa nyavu zao. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa tafakari yake, amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuomba ulinzi na tunza ya Bikira Maria anayeheshimiwa sana Ukanda wa Amazonia. Safari hii mpya ikite mizizi yake katika mchakato wa utamadunisho! Kwa njia ya ujasiri na unyenyekevu wa kimama, amekuwa kweli ni mlinzi wa watoto wake. Hii ni nafasi kwa Kanisa kuziendea tamaduni za watu. Hakuna utamaduni ambao ni kipimo wala ulio safi kupita tamaduni nyingine zote, kiasi kwamba, utamaduni huo unaweza kutumika kwa ajili ya “kusafishia” tamaduni nyingine. Kinyume chake, kuna Injili safi kabisa inayoziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili kama ambavyo wamekazia Mababa wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Baba Mtakatifu amewaweka maskini na kilio cha Dunia Mama chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumtunza Mtoto Yesu pale Nazareti.

Papa: Kilio cha Maskini

 

27 October 2019, 12:11