Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 5 Oktoba 2019 amewasimika Makardinali wapya 13 walioteuliwa hivi karibuni: Ushuhuda wa umoja, utume na umisionari wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 5 Oktoba 2019 amewasimika Makardinali wapya 13 walioteuliwa hivi karibuni: Ushuhuda wa umoja, utume na umisionari wa Kanisa.  (AFP or licensors)

Wasifu wa Makardinali Wapya, 13 wanaosimikwa 5 Oktoba 2019

Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mkesha wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, Jumamosi, tarehe 5 Oktoba 2019 amewasimika Makardinali 13 aliowateua hivi karibuni, ili kushuhudia upendo na huruma ya Mungu kwa watu wa Mataifa. Makardinali ni wasaidizi na washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, jioni tarehe 5 Oktoba 2019, kama sehemu ya mkesha wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, amewasimika Makardinali 13 aliowateua hivi karibuni, ili kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu kwa watu wa Mataifa.

1. Askofu mkuu Miguel Ángel Ayuso Guixot, M.C.C.I, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini. Alizaliwa tarehe 17 Juni 1952 huko Sevilla, nchini Hispania. Tarehe 2 Mei 1980 akaweka nadhiri zake za daima kwenye Shirika la Wamisionari wa Comboni wa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Tarehe 20 Septemba 1982 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 19 Machi 2016 baada ya kuteuliwa kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, akawekwa wakfu kuwa Askofu. Tarehe 25 Mei 2019 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini. Ni kiongozi ambaye sehemu kubwa ya maisha na utume wake, ameutekeleza nchini Misri na Sudan kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam.

2. Askofu mkuu José Tolentino Calaça de Mendonça, Mhifadhi mkuu wa Nyaraka za Kanisa na Mkutubi mkuu wa Maktaba ya Kanisa Katoliki. Alizaliwa tarehe 15 Desemba 1965 nchini Ureno. Akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 28 Julai 1990. Papa Francisko akamteuwa kuwa Mhifadhi mkuu wa Nyaraka za Kanisa na Mkutubi mkuu wa Maktaba ya Kanisa Katoliki na kumpandisha hadhi ya kuwa Askofu mkuu na kuwekwa wakfu tarehe 28 Julai 2018. Amewahi kuwa Gombera wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wareno kilichoko mjini Roma. Kwa miaka mingi amekuwa ni Jaalim, mlezi na kiongozi kwenye Vyuo vikuu vya Kipapa huko Brazil na tangu mwaka 2011 amekuwa ni mjumbe wa Baraza la Kipapa la Utamaduni.

3. Askofu mkuu Ignatius Suharyo Hardjoatmodjo, wa Jimbo kuu la Jakarta, Indonesia. Alizaliwa tarehe 9 Julai 1950 huko Semerang. Tarehe 26 Januari 1976 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Jimbo la Semarang na kuwekwa wakfu tarehe 22 Agosti 1997. Tarehe 2 Januari 2006 akateuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Askofu wa Jimbo ka Kijeshi la Indonesia na hatimaye, tarehe 28 Juni akamteuwa tena kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Jakarta, Indonesia. Kwa sasa ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Indonesia.

4. Askofu mkuu  Juan de la Caridad  García Rodríguez wa Jimbo kuu la San Cristóbal, Havana, Cuba. Alizaliwa tarehe 11 Julai 1948. Akapewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 25 Januari 1972. Tarehe 17 Juni 1997 akateuliwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo Kuu la Camaguey, nchini Cuba. Tarehe 10 Juni 2002 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Camaguey. Tarehe 26 Aprili 2016 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la San Cristóbal, Havana, Cuba.

5. Askofu mkuu Fridolin Ambongo Besungu, O.F.M. Cap. wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC. Alizaliwa tarehe 24 Januari 1960 huko Boto. Kunako mwaka 1987 akaweka nadhiri za daima. Tarehe 14 Agosti 1988 akapewa Daraja takatifu ya Upadre. Tarehe 6 Machi 2005 akawekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Bokungu-Ikela. Kwa sasa ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, CENCO. Takwimu zinaonesha kwamba, huyu ni Mkapuchini wa kwanza kuteuliwa kuwa Kardinali kutoka Barani Afrika.

6. Askofu mkuu Jean-Claude Hollerich SJ., wa Jimbo kuu la Luxembourg. Alizaliwa kunako tarehe 9 Agosti 1958 huko Differdange. Baada ya kuteuliwa na Baba Mtakatifu Benedikto XVI kuwa Askofu mkuu akawekwa wakfu tarehe 16 Oktoba 2011. Kwa sasa ni Rais wa Shirikisho la Makanisa ya Ulaya, COMECE.

7. Askofu Álvaro Leonel Ramazzini Imeri, wa Jimbo Huehuetenango, nchini Guatemala. Alizaliwa tarehe 16 Julai 1947. Akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 27 Juni 1971. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la San Marcos na kuwekwa wakfu tarehe 6 Januari 1989. Ni Mwenyekiti wa Tume ya Mawasiliano na Huduma za kichungaji kwa wafungwa magerezanii katika Baraza la Maaskofu Katoliki Guatemala. Ameshiriki kikamilifu katika Mkutano wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, CELAM huko Aparecida kunako mwaka 2007 pamoja na Sinodi ya Maaskofu wa Amerika ya Kusini, iliyoadhimishwa mjini Vatican kunako mwaka  1997.

8. Askofu mkuu Matteo Maria Zuppi, wa Jimbo kuu la Bologna, Italia. Alizaliwa tarehe 11 Oktoba 1955, Roma. Akapewa Daraja Takatifu ya Upadre 9 Mei 1981. Tarehe 31 Januari 2012 akateuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Roma na kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 14 Aprili 2012 na Kardinali Augostino Vallini. Tarehe 27 Oktoba 2015 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bologna, Italia. Katika maisha na utume wake kama Padre, kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2012 alikuwa ni Mshauri wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye makao yake makuu mjini Roma. Jumuiya ambayo inaendelea kujipambanua kwa ajili ya huduma kwa maskini, wakimbizi pamoja na mchakato wa huduma ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa mbali mbali.

9. Askofu mkuu Cristóbal López Romero, SDB, wa Jimbo kuu la Rabat, Morocco. Alizaliwa tarehe 19 Mei 1952 huko Hispania. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kitawa, akaweka nadhiri zake za daima tarehe 2 Agosti 1974 na kupewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 19 Mei 1979. Tangu wakati huo, katika maisha na utume wake kama Padre amekuwa: mhudumu wa wakimbizi na wahamiaji; amejihusisha na utume kwa vijana; Paroko na Mkurugenzi mkuu wa Jalida la Wasalesiani huko Asunciòn. Padre Mkuu wa Kanda na Mkuu wa Jumuiya. Mara kadhaa amekuwa pia katika malezi na Jaalim kwenye vyuo vikuu kadhaa ndani na nje ya Morocco. Tarehe 29 Desemba 2017, akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Rabat, Morocco na kuwekwa wakfu kama Askofu mkuu hapo tarehe 10 Machi 2019. Tarehe 24 Mei 2019 akateuliwa kuwa ni Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Tanger na Morocco.

10. Askofu mkuu Michael Czerny, S.J., Katibu mkuu msaidizi, Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu. Alizaliwa tarehe 18 Julai 1946 huko Brno, nchini Czechoslovakia ya zamani. Mwaka 1963 akajiunga na Shirika la Wayesuit na kupewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 9 Juni 1973. Kwa miaka mingi katika maisha na utume wake, amekuwa mstari wa mbele katika masuala ya haki jamii. Amewahi kuwa pia Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha “Central America University, UCA”. Kati ya mwaka 1992 hadi mwaka 2002 aliteuliwa kuwa Katibu wa masuala ya haki jamii kwenye Makao makuu ya Shirika la Wayesuit. Ni muasisi wa mtandao wa Wayesuit dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi Barani Afrika, “Jesuit AIDS Network”.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akatambua mchango wake katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika na kunako mwaka 2009 akamteuwa kuwa Mtaalam msikilizaji wakati wa Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Bara la Afrika. Kuanzia mwaka 2010 akateuliwa kuwa ni mshauri wa Baraza la Kipapa la Haki na Amani. Tarehe 14 Desemba 2016 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Katibu mkuu msaidizi, Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu na kunako mwaka 2018 akateuliwa kuwa ni mjumbe wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana iliyoadhimishwa mwezi Oktoba hapa mjini Vatican.

Askofu mkuu Michael Czerny, hivi karibuni aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa mmoja wa Makatibu Maalum wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Anasema, Kanisa kama mfano wa Msamaria mwema, linataka kujikita zaidi katika mchakato wa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; Ukanda wa Amazonia, kwa kuanzisha majadiliano katika ukweli na uwazi na hatimaye, kufanya maamuzi magumu katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema, katika kundi hili la Makardinali wateule, amewaongeza pia Maaskofu wastaafu waliojipambanua kwa huduma katika Kanisa la Kristo. Hawa ni pamoja na:

11. Askofu mkuu Mstaafu  Michael Louis Fitzgerald, ambaye amewahi kuwa ni Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini na pia Balozi wa Vatican nchini Misri na Mwakilishi wa Vatican kwenye Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu. Kardinali mteule Michael Louis Fitzgerald ambaye sasa ana umri wa miaka 82, alizaliwa kunako tarehe 17 Agosti 1937 huko Walsall, Uingereza. Akapewa Daraja takatifu ya Upadre 3 Februari 1961. Tarehe 16 Desemba 1991 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu na kuwekwa wakfu kama Askofu hapo tarehe 6 Januari 1992. Tarehe 1 Oktoba 2002 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu mkuu. Huyu ni kati ya viongozi wa Kanisa waliojisadaka bila ya kujibakiza katika kujenga na kudumisha misingi ya majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na waamini wa dini ya Kiislam, leo hii matunda yanaanza kuonekana. Baba Mtakatifu Francisko ametambua na kuthamini mchango wake katika mchakato wa majadiliano ya kidini.

12. Askofu mkuu mstaafu Sigitas Tamkevičius SJ., wa Jimbo kuu Kaunas nchini Lithuania. Alizaliwa tarehe 7 Novemba 1938 huko Krikstonys, Lithuania. Akapewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 18 Aprili 1962.  Mwaka 1968 akajiunga na Shirika la Wayesuit. Kunako mwaka 1983 akakamatwa na kufungwa gerezani kwa muda wa miaka 10. Huko akatumikia kifungo na adhabu ya kazi ngumu, kama “njia ya kulishikisha adabu Kanisa”. Mwaka 1988 akapelekwa uhamishoni huko Siberia kwenye baridi kali hadi alipoachiliwa huru. Mwaka 1990 akateuliwa kuwa Gombera wa Seminari kuu ya Kaunas. Tarehe 8 Mei 1991 akateuliwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Kaunas, Lithuania na kuwekwa wakfu hapo tarehe 19 Mei 1991. Tarehe 4 Mei 1996 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kaunas na hatimaye, akang’atuka kutoka madarakani hapo tarehe 11 Juni 2015. Kati ya mwaka 2005 hadi mwaka 2014 alikuwa ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Lithuania! Usione vinaelea…!

13. Askofu mstaafu Eugenio Dal Corso, P.S.D.P., Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Benguela, nchini Angola. Alizaliwa huko “Lugo di Valpantena di Grezzana, nchini Italia kunako tarehe 16 Mei 1939. Akapewa Daraja Takatifu ya Upadre 7 Julai 1963. Tarehe 15 Desemba 1995, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo Katoliki la Saurimo, nchini Angola. Tarehe 3 Machi 1996 akawekwa wakfu kuwa Askofu na tarehe 15 Januari 1997 akasimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Saurimo. Tarehe 18 Februari, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Benguela na tarehe 26 Machi 2018, Baba Mtakatifu Francisko akaridhia ombi lake la kutaka kung’atuka kutoka madarakani.

Ni kiongozi ambaye alisadaka maisha na ujana wake wote ili kushiriki katika utume wa kimisionari tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Amewahi kufanya utume wake nchini Argentina, lakini kilele cha utume huu ni pake alipojisadaka na kutembea bega kwa bega na maskini na wale waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya watu wa Mungu nchini Angola. Kwa ufupi huu ndio wasifu wa Makardinali wateule wanaosimikwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 5 Oktoba 2019.

Makardinali wapya

 

 

 

05 October 2019, 14:30