Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko ameridhia Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama mjini Vatican Bwana Domenico Giani kujiuzuru kutoka madarakani kama uwajibikaji wa maadili ya kazi. Baba Mtakatifu Francisko ameridhia Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama mjini Vatican Bwana Domenico Giani kujiuzuru kutoka madarakani kama uwajibikaji wa maadili ya kazi. 

Papa Francisko aliridhia uamuzi wa Kamanda wa Usalama Kujiuzuru!

Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama mjini Vatican Domenico Giani amejiuzuru kutoka madarakani kufuatia kashfa ya kuvuja kwa nyaraka za siri kuhusu baadhi ya watuhumiwa waliojihusisha na ubadhirifu wa fedha ya Kanisa, waliokuwa wamesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi dhidi ya shutuma zilizokuwa zinawakabili. Papa Francisko ameridhia uamuzi huu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi la aliyekuwa Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama mjini Vatican Domenico Giani kujizuru kufuatia kashfa ya kuvuja kwa nyaraka za siri kuhusu baadhi ya watuhumiwa waliojihusisha na ubadhirifu wa fedha ya Kanisa, waliokuwa wamesimamishwa kazi ili kupisha mchakato wa uchunguzi dhidi ya shutuma zilizokuwa zinawakabili. Kung’atuka kwa Bwana Domenico Giani kutoka madarakani ni kielelezo cha moyo wa upendo na uaminifu wake kwa Kanisa na kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.  Ameamua kuchukua uamuzi huu kama sehemu ya uwajibikaji hata kama yeye binafsi hakuhusika moja kwa moja na uvujishaji wa nyaraka hizi, ambazo zilichapishwa kwenye magazeti mbali mbali nchini Italia, tarehe 2 Oktoba 2019. Taarifa hizi zilichafua kwa kiasi kikubwa utu na heshima ya wale wote waliokuwa wanachunguzwa kwa shutuma za ubadhirifu wa mali ya Kanisa pamoja na vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican.

Kung’atuka kwa Bwana Domenico Giani kutasaidia kuendelea kwa mchakato wa kutafuta ukweli, ili sheria iweze kushika mkondo wake na hatimaye, haki iweze kutendeka. Inasikitisha kuona kwamba, habari iliyochapishwa iliambatana pia na picha za watuhumiwa, jambo ambalo kimsingi ni ukosefu wa haki. Hizi ni picha ambazo zilikuwa mikononi mwa vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican kwa ajili ya uchunguzi wa ndani. Baba Mtakatifu Francisko alikemea vikali sana taarifa hizi kwa kusema kwa hakika hii ilikuwa ni dhambi ya mauti kwa wale wote waliohusika. Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kukaa na kuzungumza na Bwana Domenico Giani kwa kipindi kirefu na ametumia fursa hii kumshukuru kwa huduma, uhuru wake wa ndani na uwajibikaji, kama kielelezo cha heshima na huduma inayotolewa na vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican. Amemshukuru kwa unyenyekevu, moyo wa sadaka na majitoleo kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kipindi cha miaka 20 ya utumishi wake mjini Vatican.

Daima ameonesha uaminifu, ukweli na uwazi na kwa hakika amekuwa ni shuhuda wa huduma iliyotukuka kwa Kanisa na kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni kiongozi aliyeaminiwa na Baba Mtakatifu kiasi cha kujenga upendo na urafiki wa dhati. Amemshukuru kwa huduma zake ndani na nje ya Vatican, kazi ambayo ameifanya kwa nidhamu, weledi na uaminifu mkubwa. Wakati huo huo, Bwana Domenico Giani katika mahojiano maalum na Vatican News katika kipindi hiki tete cha maisha na utume wake anasema, amefanya maamuzi haya magumu  katika hali ya utulivu, akiwa ametiwa shime na imani kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko aliyomwonesha katika kipindi chote cha utume wake hapa mjini Vatican. Ni kiongozi ambaye kwa muda wa miaka 38 amekuwa katika “viwanja vya ulinzi na usalama”, kwanza kabisa nchini Italia na baadaye kwa miaka 20 mjini Vatican. Ametumia karama, ujuzi na welezi wake kwa ajili ya kutekeleza dhamana na majukumu aliyokuwa amekabidhiwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro, kiasi hata cha kujisikia kuwa ni “Mtumishi asiyekuwa na faida, daima alitenda kile alichopaswa kutenda tu”.

Kamanda Mstaafu Giani anasema, amesikitishwa sana kwa watuhumiwa kuchafuliwa: majina, sifa, utu na heshima yao, wakati uchunguzi bado ulikuwa unaendelea na kwamba, bado walikuwa hawajatiwa hatiani. Uamuzi wake wa kung’atuka kutoka madarakani ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya ulinzi na usalama kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kiasi hata cha kuweza kuyasadaka maisha yake, ikiwa kama itambidi kufanya hivyo. Huu ni uamuzi wa kishujaa unaoweza kutekelezwa na Kamanda peke yake, ili kulinda heshima ya taasisi anayoiongoza. Anakiri kwamba, Baba Mtakatifu amepokea kwa masikitiko makubwa uamuzi wake na anatambua fika changamoto ambazo amekabiliana nazo katika kipindi chote cha uongozi wake kama Kamanda mkuu wa vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican. Bwana Domenico Giano anakiri kwamba, pengine hili ni kosa lenye heri kwani kwa sasa anatapata muda mwingi zaidi wa kuweza kukaa pamoja na familia yake, daima akiwa na matumaini ya kuweza kukabiliana na changamoto za mbeleni kwa imani na matumaini katika kazi zake, baada ya uzoefu na mang’amuzi haya ya pekee kabisa.

Kamanda Mstaafu Domenico Giani amemhudumia Mtakatifu Yohane Paulo II hadi dakika yake ya mwisho hapa duniani. Akamsindikiza Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika maisha na utume wake, hadi pale alipong’atuka kutoka madarakani na hatimaye, Papa Francisko pamoja na mtindo wake wa maisha wa kuwa karibu na watu wa Mungu. Kwa hakika imekuwa ni changamoto kubwa kwa ulinzi na usalama wa Baba Mtakatifu Francisko. Anakumbuka hija yake ya kwanza Lampedusa, Kusini mwa Italia, kielelezo cha upendo na mshikamano kwa wakimbizi na wahamiaji; Maadhimisho ya Siku ya Vijana nchini Brazil bila kusahau hali tete ilivyokuwa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Katika utume wake, amewasindikiza viongozi wa Kanisa katika hija za kimataifa 70, bila kuhesabu hija za kichungaji zilizotekelezwa na viongozi wakuu wa Kanisa ndani ya Italia. Jambo la kujivunia katika kipindi chote cha uongozi wake kama Kamanda mkuu wa Vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican ni huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, changamoto changamani kutoka katika Injili ya Kristo!

Kamanda Mstaafu Domenico Giani anasema, wosia wake kwa wanajeshi wa vikozi vya ulinzi na usalama mjini Vatican ni huu: nidhamu kazini; weledi, udugu wa kibinadamu; upendo, utu na heshima kwa wote, daima wakiwa wameungana na kushikamana katika utekelezaji wa dhamana na utume wao kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa ushirikiano na wasaidizi wake wa karibu, daima amejitahidi kuwafunda wanajeshi ili waweze kuwa waaminifu kwa taaluma yao, lakini pia waamini wema. Ni matumaini yake kwamba, Kamanda atakayeteuliwa na Baba Mtakatifu baada yake, ataweza kupata msingi mzuri wa kuendeleza dhamana na utume wa ulinzi na usalama kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Anamshukuru na kumpongeza mke wake Chiara na watoto wake Luca na Laura ambao wamebahatika kupata mengi katika maisha, lakini pia wakajifunza kutoa sadaka kubwa iliyojikita katika uvumilivu. Mwishoni anasema, ya Mungu mengi, hatima ya maisha yake iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu, anajiachia mikononi mwake kama mtoto mchanga kifuani pa mama yake!

Domenico Giani

 

15 October 2019, 08:23