Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko: Maaskofu wamepewa dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wanayo dhamana ya kuwaombea na kuwasindikiza katika hija ya maisha. Baba Mtakatifu Francisko: Maaskofu wamepewa dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wanayo dhamana ya kuwaombea na kuwasindikiza katika hija ya maisha. 

Maaskofu wakuu wateule kuwekwa wakfu, tarehe 4 Oktoba 2019

Maaskofu wateule ni: Antoine Camilleri ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa ni Katibu mkuu Msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican. Askofu mkuu mteule Paolo Rudelli alikuwa ni Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Ulaya. Askofu mkuu mteule Paolo Borgia, kabla ya uteuzi huu alikuwa ni Afisa mwandamizi Sekretarieti kuu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, inayoadhimishwa tarehe 4 Oktoba 2019, majira ya saa 11:00 za jioni kwa saa za Ulaya, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kuwaweka wakfu Maaskofu wakuu walioteuliwa hivi karibuni kuwa Mabalozi wa Vatican. Maaskofu wateule ni: Antoine Camilleri ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa ni Katibu mkuu Msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican. Askofu mkuu mteule Paolo Rudelli alikuwa ni Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Ulaya huko Strasbourg, nchini Ufaransa. Askofu mkuu mteule Paolo Borgia, kabla ya uteuzi huu alikuwa ni Afisa mwandamizi aliyekuwa anashughulikia masuala ya jumla kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican.

Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu mteule Antoine Camilleri alizaliwa tarehe 20 Agosti 1965 huko Silema, nchini Malta. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 5 Julai 1991 akapewa Daraja takatifu ya Upadre. Alijiendeleza na hatimaye, akajipatia shahada ya uzamivu kwenye Sheria na taratibu za uendeshaji wa kesi Mahakamani. Askofu mkuu mteule Antoine Camilleri alijiunga na utume wa kidiplomasia kunako tarehe 9 Januari 1999. Tangu wakati huo, ametekeleza utume huu nchini New Papua Guinea, Uganda, Cuba na hatimaye kwenye Kitengo cha mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican. Tarehe 22 Februari 2013 akateuliwa kuwa Katibu mkuu msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Askofu mkuu mteule Paolo Rudelli alikuwa ni Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Ulaya huko Strasbourg, nchini Ufaransa. Askofu mkuu mteule Paolo Rudelli alizaliwa tarehe 10 Julai 1970 huko Gazzaniga, Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 10 Juni 1995 akapewa daraja Takatifu ya Upadre. Katika masomo yake, amebahatika kupata shahada ya uzamili katika Sheria za Kanisa na Shahada ya uzamivu kwenye Taalimungu maadili. Askofu mkuu mteule Paolo Rudelli, alijiunga na utume wa kidiplomasia mjini Vatican kunako tarehe 1 Julai 2001. Na tangu wakati huo, ametekeleza utume huu nchini Equador, Poland na  kama afisa mwandamizi kitengo cha masuala ya kumla kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Tarehe 20 Septemba 2014 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Ulaya huko Strasbourg, nchini Ufaransa.

Askofu mkuu mteule Paolo Borgia, kabla ya uteuzi huu alikuwa ni Afisa mwandamizi aliyekuwa anashughulikia masuala ya jumla kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Atapangiwa kituo cha kazi, mara baada ya taratibu za kidiplomasia kukamilika. Askofu mkuu mteule Paolo Borgia alizaliwa huko Manfredonia, Foggia, nchini Italia hapo tarehe 18 Machi 1966. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa daraja Takatifu ya Upadre tarehe10 Aprili 1999. Ana shahada ya uzamivu katika Sheria za Kanisa. Tarehe 1 Desemba 2001 alijiunga na utume wa Kidiplomasia mjini Vatican na tangu wakati huo, ametekeleza utume wake huko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Mexico, Israel na Lebanon. Baadaye alibadilishiwa utume na kupelekwa kwenye kitengo cha mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican na mwishoni, tarehe 4 machi 2016 aliteuliwa kuwa afisa mwandamizi aliyekuwa anashughulikia masuala ya jumla katika Sekretarieti kuu ya Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anataka kuona Kanisa ambalo halina makuu, Kanisa linalojitosa kimasomaso kwa ajili ya kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Hawa ni maskini wa kiroho, hali na kipato. Kanisa ambalo uwezo na nguvu yake haitokani na mali au utajiri wake, bali neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hili ni Kanisa linalopaswa kuiga na kufuata mfano wa Yesu aliyekuwa: fukara, mtii na mseja kamili. Askofu ni alama ya utimilifu wa Daraja Takatifu ambamo Askofu anapewa dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ni dhamana inayofumbatwa katika unyenyekevu na upendo na kamwe Maaskofu wasijisikie kuwa ni wafalme. Askofu anapaswa kuwa ni mtu wa sala, kiongozi anayejipambanua kwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake adili na matakatifu.

Askofu ni kiongozi anayepaswa kuwa kweli ni mchungaji mwema, anayetambulikana pia kutokana na harufu ya kondoo wake, kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Kimsingi haya ndiyo mambo msingi ambayo yanapaswa kuoneshwa na Askofu au wale wanaotamani kufikia utimilifu wa Daraja Takatifu la Upadre ambalo kimsingi limegawanyika katika madaraja makuu matatu: Uaskofu, Upadre na Ushemasi, kadiri ya Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Haya si mambo mapya anabainisha Kardinali Marc Ouellet, kwani Askofu anapaswa kuwa ni shahidi aminifu wa Kristo na Kanisa lake; mtu wa sala na tafakari ya Neno la Mungu; kiongozi ambaye ataonesha kwa maneno na maisha yake kwamba, uongozi kwake ni huduma na wala si cheo!

Askofu kwa wanajimbo wake anapaswa kuwa kweli ni mfano wa Baba na Kaka; mpole na mnyenyekevu wa moyo, mwingi wa huruma na mapendo; mvumilivu na mwenye hekima. Baba mwema anayejitaabisha kuwachanga kondoo wake, kwa kuwaonesha dira na mwelekeo wa maisha; daima akikazia umoja, upendo na mshikamano, ili kati ya Kondoo wake, asiwepo anayepotea njia, Askofu awe kweli ni kiongozi anayekesha kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo, pasi na kumezwa na malimwengu. Askofu anayo dhamana ya kusali kwa ajili ya kuwaombea watu wote, kwa kutambua kwamba, kimsingi yeye ni mtu wa Mungu, aliyeteuliwa kati ya watu kwa ajili ya huduma, ili kuhakikisha kwamba, anakuza na kudumisha ibada na uchaji wa Mungu, mambo msingi katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Utume huu, umwezeshe kuwa kiongozi mkarimu, akitambua kwamba, Kristo Yesu ndiye anayewaita waja wake na kuwaweka wakfu ili kuendeleza kazi ya ukombozi! Wakleri wanatambua kwamba, wito ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si kwa ajili ya masitahili yao binafsi, kumbe, wanapaswa kuwa ni watu wa shukrani, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, chemchemi ya amana za maisha ya kiroho!

Papa: Maaskofu wakuu

 

03 October 2019, 16:35