Kardinali Roger Marie Élie Etchegaray, Rais Mstaafu wa Baraza la Kipapa la haki na amani & Cor Unum amefariki dunia tarehe 4 Septemba 2019 akiwa na umri wa miaka 97. Kardinali Roger Marie Élie Etchegaray, Rais Mstaafu wa Baraza la Kipapa la haki na amani & Cor Unum amefariki dunia tarehe 4 Septemba 2019 akiwa na umri wa miaka 97. 

Tanzia: Kardinali Roger Etchegaray, mjumbe wa haki na amani amefariki dunia!

Kardinali Roger Etchegaray alizaliwa mwaka 1922. Akapewa daraja takatifu ya Upadre mwaka 1947. Mwaka 1969, Mtakatifu Paulo VI akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Paris. Mwaka 1970 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Marsiglia hadi mwaka 1984. Mwaka 1979 akateuliwa kuwa Kardinali na mwaka 1984 akateuliwa kuwa Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa kwa taarifa za kifo cha Kardinali Roger Etchegaray, Rais mstaafu wa Baraza la Kipapa la haki na amani pamoja na Baraza la Kipapa lililokuwa linaratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor unum, kilichotokea tarehe 4 Septemba 2019. Kardinali Etchegaray amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 97 na Ibada ya mazishi yake, itafanyika, Jumatatu tarehe 9 Septemba 2019 kwenye Kanisa kuu la “Santa Maria huko Bayonne, Ufaransa. Baba Mtakatifu katika salam zake za rambi rambi kwa Askofu Marc Aillet wa Jimbo Katoliki la Bayonne, Ledcar na Oloron, anasema, anapenda kujiunga kwa njia ya sala na wale wote wanaoomboleza kwa msiba wa Kardinali Etchegaray, ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kumpokea katika Makao yake ya milele. Kardinali Etchegaray tangu mwanzo wa utume wake kama Askofu amejipambanua kuwa ni kiongozi na mchungaji mahiri, aliyependwa na kuheshimiwa na watu. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa chombo cha kutangaza na kushuhudia Injili ya haki na amani sehemu mbali mbali za dunia.

Ni mshauri aliyesikilizwa sana, akaheshimiwa na kuthaminiwa na viongozi mbali mbali hasa nyakati zile ambazo Kanisa lilikuwa linakumbana na changamoto na matatizo mbali mbali katika maisha na utume wake Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani na baadaye, akamteuwa pia kuwa Mwenyekiti wa Cor Unum. Baba Mtakatifu anamkumbuka sana Kardinali Etchegaray ambaye kwa sasa amepumzika katika usingizi wa milele, kwamba, alikuwa ni mtu mwenye imani thabiti, daima akawa tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Baada ya kuhitimisha safari ya maisha yake hapa duniani, ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Kristo Yesu ataweza kumpokea mtumishi na mjumbe wake wa haki na amani hapa duniani, ili aweze kushiriki katika furaha na maisha ya uzima wa milele.

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Roger Etchegaray alizaliwa tarehe 25 Septemba 1922. Akapewa daraja takatifu ya Upadre tarehe 13 Julai 1947. Mwaka 1969, Mtakatifu Paulo VI akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Paris, Ufaransa. Mwaka 1970 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Marsiglia hadi mwaka 1984. Mwaka 1979 akateuliwa kuwa Kardinali na mwaka 1984 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani hadi mwaka 1998 na Mwenyekiti wa Cor Unum hadi mwaka 1995. Alichangia sana katika mchakato wa haki, amani na upatanisho sehemu mbali mbali za dunia. Mwaka 1994 akateuliwa Rais wa Kamati kuu ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu. Mwaka 2005 akateuliwa kuwa Makamu wa Dekano wa Baraza la Makardinali.

05 September 2019, 19:08