Papa Francisko: Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani ni tarehe 29 Septemba 2019: Kauli mbiu: Si wahamiaji peke yao! Utu, heshima, haki msingi za binadamu na hatima ya familia ya binadamu! Papa Francisko: Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani ni tarehe 29 Septemba 2019: Kauli mbiu: Si wahamiaji peke yao! Utu, heshima, haki msingi za binadamu na hatima ya familia ya binadamu! 

Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani 2019: Ibada ya Misa!

Papa Francisko anasema: Tarehe 29 Septemba 2019, katika Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 4: 00 za asubuhi. Baba Mtakatifu anasema, hiki ni kipindi cha kuonesha ukaribu na mshikamano kwa wakimbizi na wahamiaji kwa njia ya sala, huduma na ukarimu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya 105 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2019 itaadhimishwa Jumapili,  tarehe 29 Septemba 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Si Wahamiaji peke yao”. Baba Mtakatifu  Francisko anasema, mambo yanayopewa kipaumbele cha pekee katika Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa ajili ya huduma endelevu na fungamani kwa wakimbizi na wahamiaji ni: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha. Hili si suala la wahamiaji na wakimbizi peke yake, bali linagusa na kutikisa misingi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni mwaliko wa kutowatenga watu kwa sababu ya maamuzi mbele, kwani kwa kufanya hivi, ni kuendeleza ukatili dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Baba Mtakatifu mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe  22 Septemba 2019 amewakumbusha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, Jumapili tarehe 29 Septemba 2019, katika Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 4: 00 za asubuhi kwa saa za Ulaya. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika tukio hili hata kwa kuonesha ukaribu na mshikamano kwa wakimbizi na wahamiaji kwa njia ya sala.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa Siku ya 105 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2019 anagusia kuhusu: madhara ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine na matokeo yake ni ubaguzi na watu kutengwa kutokana na sera za kibaguzi, hofu na wasi wasi zisizokuwa na mashiko hata kidogo. Anawahimiza waamini kufikiri na kutenda kama Msamaria mwema, kwa kuwaonea huruma wakimbizi na wahamiaji kama sehemu ya utekelezaji wa huduma ya upendo inayogusa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Katika muktadha huu, hakuna sababu inayoweza kupelekea watu kutengwa katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Huu ni mwaliko wa kuibua sera na mikakati ya kiuchumi inayotoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wanyonge katika jamii ili kuweza kushiriki kikamilifu na kuchangia katika mustakabali wa maendeleo yao.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, haya ni maendeleo yanayomgusa mtu mzima; kiroho na kimwili, ili kutoa nafasi ya ujenzi wa mji wa Mungu na mji wa binadamu kwa kukazia udugu wa kibinadamu, mshikamano, ukweli na uwazi. Huduma endelevu na fungamani kwa wakimbizi na wahamiaji inafumbatwa katika mambo makuu manne yaani: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha. Hili ni jibu makini katika kukabiliana na changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Kwani hapa, Kanisa linaangalia kwa umakini mkubwa hatima ya maisha ya familia ya binadamu kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, kwa kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuondokana na utandawazi wa kutowajali na kuwathamini wengine, ili hatimaye, kujenga ulimwengu unaokidhi vigezo vya mpango wa Mungu.

Papa: Siku ya Wakimbizi Duniani
23 September 2019, 15:59